Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akizungumza na Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Sweden na Tanzania. Lugola alimwambia Balozi huyo, nchi ipo salama na imara na ayapuuze maneno ya baadhi ya watu wanaoichafua nchi wakiwa na maslahi yao binafsi. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Waziri Lugola, jijini Dodoma leo. Picha zote na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsikiliza Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg alipokuwa akimfafanulia jambo wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika ofisini kwa Waziri huyo, jijini Dodoma, leo. Viongozi hao walijadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Sweden na Tanzania. Pia Waziri Lugola alimwambia Balozi huyo, nchi ipo salama na imara na ayapuuze maneno ya baadhi ya watu wanaoichafua nchi wakiwa na maslahi yao binafsi. Mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi ya Waziri Lugola, jijini Dodoma leo.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema Tanzania ni kisiwa cha amani na pia ipo imara katika Bara la Afrika licha ya uwepo wa baadhi ya watu wachache wanaichafua taswira yake kwa maslahi yao binafsi.
Lugola ameyasema hayo jijini Dodoma leo, alipokua anazungumza na Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg, ofisini kwake alimueleza kuwa, Rais Dk John Magufuli anaendelea kuiongoza nchi vizuri, na mpaka sasa Tanzania ipo imara na itaendelea kuwa imara, na wageni mbalimbali wanakaribishwa kuja nchini kuwekeza, kufanya utalii pamoja na masuala mbalimbali ambayo yatawezesha nchi kupata maendeleo zaidi.
“Mheshimiwa Balozi nchi yetu ipo salama na tunaendelea kuijenga kwa juhudi zote, Sweden na Tanzania ni marafiki kwa miaka mingi, yangu kipindi cha uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, hivyo tutaendelea kushirikiana nanyi ipasavyo, nakukaribisha sana Dodoma na hapa ndio makao makuu ya nchi,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, anaikaribisha Serikali ya Sweden pamoja na wananchi wake wafike nchini kuwekeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo utalii, pamoja na masuala ya biashara.
Waziri na Balozi huyo, pia walijadiliana masuala ya ushirikiano katika kuendelea kuimarisha usalama nchini, huku Lugola akimwambia Balozi huyo mikakati ya nchi katika kuimarisha ulinzi ambapo Serikali inatarajia kufunga kamera usalama (CCTV) katika Jiji la Dar es Salaam, Mwanza na Arusha kwa lengo la kuimarisha ulinzi zaidi.
Waziri Lugola alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Tanzania itaendelea kuwa salama kwa kuwa Wizara yake imejipanga vizuri kuendelea kuwalinda raia na mali zao pamoja na wageni wote waishio nchini.
“Mheshimiwa Balozi nashukuru sana kwa kunitembelea, najisikia furaha kwa ujio wako na karibu sana wakati wowote, Wizara yangu pamoja na nchi yangu kwa ujumla tutaendelea kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali,” alisema Lugola.
Hata hivyo, Balozi Sjoberg alifurahi kuonana na Waziri huyo pamoja na kufika Makao Makuu ya Serikali jijini Dodoma ikiwa ni mara yake ya pili tangu alipofika nchini kwa ajili ya kuiwakilisha nchi yake, pia alimuhakikishia ushirikiano zaidi kati ya Sweden na Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...