Asisitiza wafanye kazi waliyopewa na
Mheshimiwa Rais
Na John
Mapepele, Simiyu
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amepiga marufuku makongamano ya
wafugaji yenye lengo la kumpongeza Rais Dk John Magufuli kwa uamuzi aliochukua
wa kuwasaidia badala yake ametaka watumie kipindi hiki kifupi walichopewa
kuanisha maeneo ambayo yamepoteza sifa za uhifadhi yaweze kuchukuliwa kwa
ajili ya malisho ya mifugo.
Hivyo ametaka wafugaji kote nchini kujipanga na kupendekeza maeneo yaliyopoteza
sifa za uhifadhi, mashamba yasiyoendelezwa ili wafugaji waweze kuyapata kwa
ajili ya malisho ya mifugo yao kama sehemu ya kuunga mkono uamuzi uliotolewa wa
kusaidia sekta hiyo.
Akizungumza katika mkutano wa kuwasilikiza wananchi waishio kando ya Hifadhi ya
Pori la Akiba la Maswa wilayani Meatu mkoani Simiyu kwenye ziara ya Kamati ya
mawaziri nane, Waziri Mpina alisema tangu mwaka 2000 tume zaidi ya 27 ziliundwa
na Bunge na Serikali kushughulikia migogoro zaidi ya 1,095 lakini asilimia 99
ya mapendekezo ya tume hizo hayajatelezwa hadi leo.
Mpina alisema tume nyingi zilizoundwa miaka ya nyuma kushughulikia migogoro
hiyo zilichakachuliwa hata kabla ya kukabidhi matokeo ya mambo waliyobaini kwa
kuwa kwenye migogoro hiyo wako baadhi ya viongozi wa Serikali wako nyuma wana
manufaa binafsi wanayopata ndio maana mapendekezo yaliyotolewa ya kutatua
migogoro hiyo hayajawahi kutekelezwa hadi leo.
Alisema baadhi ya watendaji wa Serikali walilazimika hata kutoa rushwa ili
kubadilisha maamuzi ya tume zilizokuwa zinaundwa kushughulikia migogoro hiyo
kwa sababu wananufaika na migogoro hiyo.
“Mhe John Pombe Magufuli akasema hapana nitaunda tume ambayo haitapokea rushwa
timu ya Lukuvi mnaiona ina sura ya kupokea rushwa? Vichwa vya kina Mpina
unaweza ukawapa nini wakakubali, akasema wananchi wangu watahangaika mpaka
lini, watauana mpaka lini mifugo mingi imedhulumiwa kwa kivuli cha uhifadhi,
Mhe Rais akasema nitaunda tume ndio hii sasa ya mawaziri 8”alisema Mpina
Mpina aliwahakikishia wananchi kuwa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi
yatafika kwa Rais tofauti na tume zingine zilizotangulia zilikuwa hazina uwazi
wa namna ya kuchukua maoni na namna ya kufikisha mapendekezo serikalini.
“Mhe Rais akasema nitaunda timu ambayo itaandaa waraka wa baraza la mawaziri
ili waraka ule uamuliwe na Serikali hapo ndipo utaona huyo ndio Dk John Pombe
Joseph Magufuli ambaye amejipambanua katika kuhakikisha kwamba matatizo ya
wananchi yanashughulikiwa na yanamalizika”alisema Mpina
Kufuatia hali hiyo Waziri Mpina ameagiza wafugaji wote nchini kusitisha
makongamano na maandamano ya kumpongeza Rais kwa sasa kwani Rais amewapa kazi
wakulima, wafugaji, wavuvi kuangalia maeneo ambayo yamepoteza sifa yaweze
kupendekezwa ili wafugaji wayapate.
“Sisi kama wafugaji tusipoteze muda wa makongamano na kumshangilia Mhe Rais
wakati ametupa kazi kubwa ya kupendekeza maeneo hayo ili mwisho tuyapate,
yafutwe tuweze kufanya shughuli kilimo, ufugaji”alisema
Hivyo Waziri Mpina amekataa kuhudhuria makongamano ya vyama vya wafugaji ambao
wamemualika kuhudhuria sherehe hizo na kuwataka kujipanga vizuri kupendekeza
ili kuitumia vizuri nafasi ya pekee waliyopewa na Rais Dk Magufuli.
“Hakuna kiongozi mwingine yoyote katika historia ya Tanzania ambaye amekuwa na
mtizamo wa kutatua kero za wananchi wake kama Mhe Dk John Pombe Magufuli, Rais
huyu historia itaandika ya Tanzania na hata ya dunia kwa mtazamo wake ambapo
wananchi wengi wakitaka kupaza sauti zao wanazuiwa na watu wachache ambao
walikuwa na masilahi katika mambo hayo sasa hayo yote yamefika
mwisho”alisisitiza Waziri Mpina.
Akiwasilisha maelezo na mapendekezo ya wananchi waishio Kando ya Pori la Akiba
la Maswa mmoja wa wananchi hao, Deus Martin alisema hadi sasa jumla ng’ombe 75
wanashikiliwa katika Kituo cha Buturi kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi 4 bila
kuachiwa na kurudishiwa wenyewe.
Alisema mpaka uliopo sasa uliwekwa mwaka 1984 bila kuwashirikisha wananchi
ambapo katika kipindi hicho wananchi walikuwa wanaishi zaidi ya kilomita 10
kutoka mpaka uliowekwa sasa hivyo wananchi walihamishwa kwa nguvu na
kusababisha ukosefu wa malisho hadi sasa.
Hivyo wameomba kupewa maeneo hayo waliyoyaacha ndani ya hifadhi ili wayatumie
kwa ajili ya malisho kwa kipindi cha kuanzia Novemba hadi Juni.Pia wameomba
Sheria ya kuwazuia ndani ya mita 60 kutoka kwenye kingo za mito ifutwe ili
waweze kutumia maeneo hayo kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Maalum na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, William Lukuvi aliwahakikishia wananchi walioondolewa kupisha mita 500
warudi waendelee na shughuli zao kwani Rais Dk John Magufuli alishasitisha
zoezi la kuwaondoa wananchi hao.
Lukuvi aliwahakikishia wananchi waishio pori la Akiba la Maswa kuwa mapendekezo
waliyotoa ya kuomba kuongezewa eneo la malisho wamechukua na watayasilisha kwa
Rais kama yalivyo kwa uamuzi zaidi.
Mawaziri wanaounda timu hiyo mbali na Mpina na Lukuvi ni pamoja na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Suleiman Jafo, Waziri wa Maji, Profesa Makame
Mbarawa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamish Kigwangala, Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary
Mgumba na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Mussa
Sima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...