Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
RUGE Mutahaba ni kielezo cha mfano na ameacha alama!Ndivyo Mbunge Mwigulu Nchemba anavyomuelezea Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba ambaye amefariki dunia jana nchini Afrika Kusini.
Mwigulu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anaelezea kusikitishwa kwake na kifo cha Ruge Mutahaba ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa pamoja na kwamba Ruge ametanguliwa mbele ya haki lakini ameacha alama kutokana na mambo ambayo ameyafanya kwa ajili ya nchi yetu.
"Nilikutana na Ruge kwa mara ya kwanza baada ya mimi kuteuliwa na Chama changu cha CCM kuwa mweka Hazina.Tulioonana tulizungumza mengi na alinipa ushauri ambao hakika ulinisaidia katika kufanya kazi zangu ndani ya Chama.Alikuwa akisaidia vijana kutimiza ndoto zao, aliamsha fikra za watu waliolala,"amesema.
Ameongeza kwa kazi nzuri ambayo ameifanya Ruge kwa ajili ya nchi yake itabaki kuwa kilelezo cha kijana bora na mzalendo kwa Taifa letu."Maisha ya Ruge ni kitabu kutokana na aina ya maisha ambayo ameyaishi.Nachoweza kusema amethibitisha kuwa kuishi muda mrefu sio kipimo cha mafanikio kwani Ruge ameishi muda mfupi lakini amefanya mambo makubwa yenye mafanikio ya hali ya juu."
Ametumia nafasi hiyo kutoa pole kwa wazazi, familia, Kampuni ya Clouds Media Group kutokana na msiba wa Ruge na kuongeza kuwa kauli yake ya kwamba akifa watu washerehekee inaonesha ni kwa namna gani ambavyo alijua anayoyafanya yabaki ya kukumbwa na Watanzania wengi hasa kwa kuzingatia vijana wengi wamepita kwenye mikono yake.
Wakati huo huo, viongozi wa ngazi mbalimbali na wananchi wamefika nyumbani kwa wazazi wake Ruge Mutahaba ili kutoa pole ambapo idadi kubwa ya watu wamefika nyumbani hapo. Wakizungumzia Ruge Mutahaba baadhi ya wananchi waliofika msibani hapo wamesema kifo chake kimeacha pigo kubwa kwani enzi za uhai wake alijitoa kimaisha kusaidia wengine.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mbunge Mwigulu Nchemba alipokwenda kuhani msiba wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba kwa niaba ya Serikali, nyumbani kwa wazazi wa marehemu Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...