Na Sylvester Raphael
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali
Marco E. Gaguti amemaliza mgogoro wa wakulima na wafugaji uliodumu kwa zaidi ya miaka
kumi na moja katika Kijiji cha Kahundwe kata Chanika Tarafa Kituntu Wilayani Karagwe,baada ya kukutana nwa wananchi wa kijiji hicho na kutoa msimao wa Serikali
na kuonya juu ya uvunjifu wa amani uliowahi kutokana na mgogoro huo mwaka 2008.
Awali kabla ya kwenda Kijijini
Kahundwe Februari 26, 2019 kuwasikiliza wananchi hao wakulima (wavamizi) na
Wafugaji na kumaliza mgogoro huo Mkuu wa Mkoa Gaguti aliunda timu ya wataalam
kupitia nyaraka mbalimbali kuhusu kijiji hicho na kuwasikiliza wananchi pande
zote mbili ili kubaini ukweli na chanzo cha mgogoro ambapo timu hiyo ilifanya
kazi yake na kuwasilisha majibu kwake.
Mkuu wa Mkoa Gaguti baada ya kupitia
taarifa ya timu aliyoiunda na kuwasili Kijijini Kahundwe na kusikiliza pande
zote mbili za Wakulima (Wavamizi) na wafugaji aliwaeleza wananchi hao kuwa
tayari Serikali ilishabaini ukweli wa ni nani mmiliki halali wa eneo hilo la
Kijiji cha Kahundwe kati ya Wakulima na Wafugaji.
“Mwaka 1987 mamlaka za vijiji vinne
zilikaa na kukubaliana kutenga eneo la kufugia mifugo yao na lilitengwa eneo la Kijiji
Kahundwe kuwa eneo la wafugaji na kusajiliwa kisheria, lakini kuanzia mwaka
2008 hadi 2015 baadhi ya wananchi kutoka maeneno mengine walivamia eneo hilo na
wavamizi sita walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria na kupatikana na
hatia na kufungwa jera miezi sita kila mmoja.” Alieleze Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Mkuu wa Mkoa Gaguti aliendelea
kuwaeleza wananchi kuwa tangu wakati huo kumekuwa na uvamizi wa wakulima kutoka
nje ya Kijiji hicho na kuleta mgogogro mkubwa kati yao na wafugaji. Aidha,
alisema kuwa Serikali tayari imebaini ukweli wa uhalali wa nani anatakiwa kuwa
katika eneo hilo na itasimamia ukweli huo wa mwaka 1987 na kama kutakuwa kuna wananchi wanataka
mabadiliko wafuate sheria kama wenzao walivyofanya katika kutenga eneo hilo
kuwa la wafugaji.
“Hapa hakuna mgogoro wa ardhi
bali ni uvunjifu wa sheria tu, nitahakikisha namaliza uvunjifu huu kuanzia sasa
na sitaki kusikia jambo hili linaendelea. Lengo la kuja hapa ni kusimsmia
msimamo wa Serikali kwa njia ya amani na utulivu. Natambua kuwa kuna wakazi au
wafugaji 200 lakini 43 kati ya hao ni wavamizi si wenyeji nataka jambo hilo
liishe mara moja.” Alitoa msimamo wa Serikali Mkuu wa Mkoa Gaguti.
MAAGIZO
Mkuu wa Mkoa
Gaguti alimwagiza na kumpa wiki moja Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Godfrey Mheluka kuanzia
tarehe 27/02/2019 kufanya uhakiki na utambuzi
wa wafugaji wadogo ambao walisajiliwa katika Kijiji hicho cha Kahundwe na
kuwaondoa wavamizi ambao ni wakulima na wafugaji wakubwa waliotoka maeneo
mengine.
Pili Mkuu wa Wilaya ya Karagwe
Godfrey Mheluka na timu yake wafanye uhakiki wa mifugo ili kubaini wafugaji
ambao kwanza si raia wa Tanzania na pili kubaini wingi wa mifugo kusudi kama kuna
wafugaji wakubwa wenye mifugo mingi waondolewe ili wafuate sheria za kuomba
vitalu vya kufugia kama wafugaji wakubwa au wawekezaji katika vitalu.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha
Kahundwe walimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuwa mgogoro huo unachochewa na
Diwani wa Kata ya Chanika kwasababu wakati wa Kampeini ya mwaka 2015 aliwahidi
baadhi ya wananchi hao wavamizi kuwa akipata madaraka atahakikisha wanalichukua
eneo la Kijiji cha Kahundwe kama eneo lao la kilimo.
Naye Bw. Bernard Sau Afisa Ardhi
Wilaya ya Karagwe akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Mkoa Gaguti alisema kuwa
kijiji cha Kahundwe kilisajiliwa mwaka 1987 kwa GN namba 620 kama Kijiji cha
wafugaji na wakati huo ilikuwa Wilaya moja ya Karagwe kabla ya kutengwa Wilaya
mbili za (Karagwe na Kyerwa) na baada ya kutenga Wilaya mbili kijiji cha
Kaundwe kilibaki Wilaya ya Karagwe na kijiji hicho kina jumla ya Hekta 20,000
za kufugia.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...