Mkurugenzi wa Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma. Mkutano wa Msemaji Mkuu wa Serikali na waandishi wa habari ni wa kwanza kwa mwaka huu ambao ameutumia kuwaelezea wananchi juhudi mbalimbali za kimageuzi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano.


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO 

DODOMA 

Serikali imetoa notisi ya siku 24 kwa wamiliki wa machapisho (magazeti na majarida) ambayo bado hayajahuisha leseni zao kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kuhakikisha wanahuisha leseni hizo hadi ifikapo Machi 21, 2019 vinginevyo hayataruhusiwa kuchapishwa. 

agizo hilo limetolewa na Mkurugenzi Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi leo Jijini Dodoma wakati akiongea na Wanahabari kuhusu utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Serikali ikiwemo utekelezaji wa Sheria ya Huduma ya Habari. 

"Kwa mujibu wa Sheria mpya ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, wamiliki wote wa magazeti na majarida wanapaswa kuhuisha leseni zao kila mwaka na tulitoa notisi kwa ambao hawajahusiha, wapo walioitikia wito na wapo waliokaidi, orodha kamili imewekwa katika www.maelezo.go.tz" ameeleza Dkt. Abbasi. 

Aidha, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa, utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari unaendelea hivyo wakati wowote kuanzia sasa chombo cha kwanza cha kusimamia wanahabari yaani BODI YA ITHIBATI itaundwa ambapo kazi yake kubwa ni kusajili wanahabari, kuwapa vitambulisho vya kitaaluma na kusimamia maadili yao. 

katika kuhakikisha kuwa Waandishi wa Habari wanatekeleza majukumu yao bila vikwazo na pia wananchi wanapata taarifa mbalimbali, Dkt. Abbasi ametoa wito kwa Watendaji mbalimbali wa Serikali katika ngazi zote kutoa habari na kueleza utekelezaji wa ahadi mbalimbali za Serikali kwani ni takwa la Katiba na Sheria. 

"Natumia mkutano huu kuwakumbusha watendaji mbalimbali wa Serikali katika ngazi zote kuwa, isipokuwa kama habari husika imezuiwa kisheria, kwa sasa kutoa habari na kueleza utekelezaji wa ahadi tulizoahidi ni takwa la Katiba na Sheria na si utashi mtu binafsi. Tutaanza kufuatilia watendaji wanaokaidi matakwa haya ya kikatiba" amefafanua Dkt. Abbasi. 

Mbali na hayo Dkt. Abbasi amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza kwa kasi wajibu wake kwa umma ikiwemo kuhakikisha hali ya amani, utulivu, kusimamia utawala bora na utawala wa sheria.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...