WACHIMBAJI na wadau wa madini wa Mkoa wa Manyara, wanatarajia kuandamana kesho jumamosi kwa lengo la kumshukuru Rais John Magufuli kwa kukubali kusaini muswaada wa dharura wa marekebisho ya sheria za fedha, kupunguza na kufuta kodi zilizolalamikiwa.
Maandamano hayo ya kilomita tatu yataanzia kwenye lango la Magufuli la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite hadi kwenye uwanja wa Barafu wa CCM mji mdogo wa Mirerani.
Kaimu Mwenyekiti wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (Marema) Tawi la Mirerani, Shwaibu Mushi (Bahati) alisema maandalizi ya maandamano hayo yatakayopokelewa na mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti yanaendelea vizuri.
Mushi alisema Maandamano hayo yatawahusisha wachimbaji wote wa madini wa mkoa wa Manyara, kutoka wilaya zote za Simanjiro, Kiteto, Babati, Hanang' na Mbulu. Alisema wanampongeza Rais Magufuli kwa kuwakubalia ombi hadi wabunge wakapitisha sheria hiyo baada ya mkutano wa kisekta wa wadau wa madini uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es salaam.
Alisema kauli mbiu ya maandamano hayo ni 'Rais wetu, madini yetu, uchumi wetu' ambapo wadau mbalimbali wa madini wakiwemo wachimbaji, wamiliki wa migodi na wazamiaji (WanaApolo) watashiriki. "Pia wadau wengine wanaonufaika na madini wakiwemo wafanyabiashara, madalali na wanunuzi wa madini mbalimbali watashiriki maandamano hayo ya kumpongeza Rais Magufuli," alisema Mushi.
Alisema wanaandamana kumpongeza Rais Magufuli baada ya kupita siku 17 tangu mkutano wake na wadau wa madini kufanyika na kisha kupitishwa kuwa sheria na bunge. Alisema wao wenyewe kama wadau wa madini hawana cha kumpa Rais Magufuli hivyo wanatumia maandamano hayo kwa lengo la kumuunga mkono na kuonyesha kuwa wapo naye pamoja katika uongozi wake.
"Maandamano hayo yanatarajia kuanzia saa mbili asubuhi na kumalizika saa nne asubuhi ambapo itasomwa risala ya kumpongeza Rais Magufuli kudhibiti utoroshwaji madini, ulipaji kodi na kumuunga mkono," alisema Mushi. Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara Agostino Senga alisema maandamano kama hayo huwa yanaruhusiwa kufanyika mradi wahusika wawe na kibali kutoka kwa mkuu wa polisi wa wilaya husika.
Kamanda Senga alisema hivi karibuni yalifanyika maandamano kama hayo ya wafugaji na wakulima kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwatetea hivyo hata hayo ya wadau wa madini watayaruhusu wakiomba kibali.
Kaimu Mwenyekiti wa Marema Tawi la Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Shwaibu Mushi (Bahati) akizungumza na waandishi wa habari juu ya maandamano ya kumpongeza Rais John Magufuli kesho jumamosi.
Wazamiaji wa migodi ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara (WanaApolo) wakipanga viroba vilivyotolewa mgodini, ambapo kesho jumamosi wanaandamana kwa ajili ya kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuwajali na kuwatetea.
Baadhi ya wanaApolo wa mgodi wa madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakisomoa viroba mgodini, huku wakijiandaa kwa ajili ya kuandamana kesho jumamosi ili kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuwajali wachimbaji madini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...