Na: Moshy Kiyungi, Dar es Salaam

Machi, 2019.

Majina ya Sam Mangwana siyo mageni masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki na Kati. Ni mwanamuziki mwenye vipaji vya utuzi na kuimba nyimbo za muziki wa dansi.

Wasifu wa Sam Mangwana unaeleza kuwa alizaliwa Februari 21, 1945, katika mji wa Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Wazazi wake walikuwa wahamiaji ambapo baba yake alikuwa raia toka nchini Zimbabwe, wakati mama yake raia wa  Angola. Mangwana aliwahi kuwa mwanachama, mtunzi na mwimbaji katika bendi ya T.P. OK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Franço Luambo Makiadi.

Nguli huyu alipitia kupiga muziki katika bendi zilizokuwa zikiongozwa na Tabu Ley Rochereau za African Fiesta, African Fiesta National na Afrisa Internationale.

Weledi wake katika muziki ulijulikana zaidi mwaka 1963, alipokuwa akipiga muziki wa rhumba katika bendi ya African Fiesta, iliyokuwa ikimilikiwa na na kuongozwa na Tabu Ley Rochereau.

Baadae Sam Mangwana alivuka mto Kongo akaingia katika mji wa Brazzaville, nchini Kongo Brazzaville.

Nchi hizo mbili za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kongo Brazzaville, zinapakana na kutenganishwa na mto Kongo. Sam alipofika katika jiji hilo, aliunda bendi ya Los Batchichas, ambayo haikudumu kwa kipindi kirefu.
Aliwahi kufanya kazi katika bendi zilizoanzishwa za Negro Band na Orchestra Tembo mjini Brazzaville. Baadae akarejea kwao DRC katika jiji la Kinshasa, ambako aliungana na Tabu Ley, kupiga muziki katika bendi ya African Fiesta National.

Mwaka 1967, Mangwana kwa mara nyingine tena aliamua kuunda bendi yake akaipa majina ya Festival des Maquisards. Bendi hiyo ilisheheni wanamuziki wakiwemo mwimbaji Dalienst, mpiga  gitaa Dizzy Mandjeku na Michelino  aliyekuwa akipiga gitaa la solo.

Miaka miwili baadae, Sam Mangwana aliondoka tena akaenda kujiunga na mpiga gitaa maarufu aliyekuwa akiitwa Jean Paul "Guvano" Vangu, hadi mwaka 1972.

Mwaka huohuo wa 1972, alikwenda kujiunga katika bendi ya  T.P.OK. Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luambo Makiadi. Mwaka 1973 Sam Mangwana alifuatana na bendi ya T.P.OK Jazz, walikuja katika jiji la Dar es Salaam kuporomosha burudani.
Yaelezwa kwamba Mangwana alifanywa mkarimani wa muda, akiwasaidia sana wanamuziki wenzake ambao walikuwa hawafahamu lugha yya Kiswahi.

Aidha alishirikiana vyema kuimba nyimbo zilizotungwa na mpiga gitaa wa bendi ya T.P. OK. Jazz, Lutumba Simaro Massiya, ambapo umaarufu wake ukapanda haraka wakati huo. Ushirikiano wake na Simaro, waliweza kuachia vibao vikali vya"Ebale ya Zaire", "Cedou", "Mabele" na nyingine nyingi.

Mangwana aliicha bendi ya T.P. OK. Jazz na kurudi tena kwenye bendi ya Tabu Ley ya Afrika Interantionale. Hata hivyo hakudumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo, ya  Leyu, akaenda katika mji wa  Abidjan, nchini Ivory Coast, Afrika ya Magharibi.

Mwaka 1978 Mangwana pamoja na wanamuziki wengine waliunda bendi  iliyoitwa African All Stars. Mwaka mmoja baadaye bendi hiyo ilisambaratika mwaka 1979, Mangwana akaamua kuwa mwanamuziki wa kujitegemea.

Aliweza kurekodi na kufanya ziara nchi mbalimbali akiwajumuisha wanamuziki wenye vipaji mchanganyiko.
Akiwa na wanamuziki hao, alirekodi wimbo za  "Maria Tebbo" mwaka 1980, "Cooperation wa mwaka 1982, akiwa na Franco, "Canta Moçambique" wa mwaka 1983, akishirikiana na Mandjeku.

Baadhi ya nyimbo za nguli huyu ni Suzana, Fati Mata, Kabibi, Lokolo ya mwaka 1989, For Ever ya mwaka 1984, Aladji ya 1987, Waka Waka ya 1978, Bonne Anne ya mwaka 1983, Tchimurenga Zimbabwe, Maria Tebbo  na Matinda za mwaka 1979 na nyingine nyingi.

Sam Mangwana bado yu hai akipiga muziki wa kujitegemea.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...