Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
WATALAAM wa sekta ya afya na hasa
katika upande wa ununuzi wa dawa kutoka nchi za SADC wamekutana nchini Tanzania
kwa lengo la kujadili pamoja na kutoa muongozo utakaosaidia kufanikisha mfumo wa ununuzi wa
dawa kwa pamoja kwa nchi hizo.
Jukumu la kununua na kusambaza dawa
hizo kwa nchi za SADC limekabidhiwa kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini ya Tanzania
baada ya kukidhi vigezo na sifa ambazo zilikuwa zimewekwa na nchi hizo.
Akizungumza leo Machi 21,2019 jijini
Dar es Salaam Mgeni rasmi wa mkutano huo wa watalaam wa sekta ya afya kwa nchi
za SADC na hasa upande wa manunuzi ya dawa, Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud
Msasi amesema mkutano huo ni muhimu kwani utatoa muongozo wa namna bora ya
kufanikisha ununuzi wa dawa wa pamoja.
Amesema jukumu la kununua dawa hizo na
kuzisambaza kwa nchi za SADC lipo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na hivyo kabla
ya kuanza kwa utaratibu huo watalaam wamekutana kuweka mkakati utakaofanikisha ili
kufikia lengo.
"Hiki
nikao cha kitalaam ambacho lengo lake ni kujadili namna bora ya kufanikisha
ununuzi wa dawa kwa pamoja.Pia ni kikao kitakachotoa muongozo ili kufanikisha
mfumo huo ambao ni mpya ingawa kwa nchi nyingine duniani wamekuwa wakiutumia
kwa baadhi ya dawa,"amesema.
Kuhusu lini mfumo huo utaanza, Msasi
amejibu utaanza baada ya kikao hicho cha watalaam kujadiliana na kwa upande wa MSD
ipo tayari kwani walishajipanga kwa kazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi wa MSD
Abdul Mwanja amesema wao wamejipanga na
wako tayari kuanza kazi hiyo ya ununuzi
wa dawa wa pamoja ambao faida ya nyingi na kubwa utasaidia kukunua dawa kwa bei
nafuu.
"Mnaponunua dawa kwa pamoja, wenye
viwanda vya kuzalisha dawa watapunguza bei na hivyo kumuwezesha mwanchi
anayehitaji dawa kuzipata kwa gharama ya chini. Hivyo ni mfumo ambao utasaidia
nchi hizo kununua dawa wa gharama ya chini,"amesema.
Alipoulizwa kuhusu MSD wamewezaje kuaminiwa
na kupewa jukumu hilo, amejibu kulikuwa na vigezo ambavyo viliwekwa na kazi
nzuri ambayo imefanywa na MSD ikiwemo ya kusambaza dawa katika hospitali zote
nchini Tanzania imewapa nafasi ya kupewa kazi hiyo.
Kuhusu changamoto za mfumo huo,amesema
kwa sasa ni mapema mno maana bado hawajaanza , hivyo iwapo zitajitokeza
wataangalia namna ya kukabiliana nazo lakini kwa namna ambavyo wamejipanga wana
matumaini watatimiza jukumu hilo kikamilifu."Na kwa uwekezaji ambao
umefanyika MSD inaweza kuifanya kazi hiyo kwa miaka mitano."
Ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa MSD
miaka miwili iliyopita walikuwa wananunua dawa kwa wazalishaji wa dawa 10
lakini sasa hivi wananunua kwa wazalishaji
148 ambao wameingia nao mkataba."Hii itasaidia kupata dawa kwa gharama nafuu kwani
hakuna mtu wa kati tena na tumekubaliana kila nchi itakuwa na fedha zake lakini
anayenunua kwa niaba ya nchi hizo ni MSD."
Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daudi Msasi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufungua mkutano wa kujadili mwongozo wa huduma ya ununuzi wa pamoja wa dawa kupitia kupitia MSD.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...