Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Godfrey Ndalahwa (katikati),akizungumza na waandishi wa habari wakati Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemeni Jafo (wa pili kilia), akitembelea tawi la benki hiyo mjini Dodoma leo. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Masoko na Mawasiliano, Rahma Ngassa na Meneja wa DCB Dodoma, Joseph Njile.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo ameipongeza Benki ya Biashara ya DCB kwa kujiendesha kwa faida licha ya changamoto mbalimbali zinazozikabili taasisi za fedha.
Pongezi hizo alizitoa wakati akitembelea tawi la benki hiyo la mjini Dodoma ambapo ameonesha furaha aliyonayo ni kuona DCB imeunga mkono kwa vitendo juhudi za Mheshimiwa Rais wa awamu ya tano ya kuhamia Dodoma.
Alisema ni imani yake sasa manufaa ilizopata manispaa za Jiji la Dar es Salaam hususani vikundi vidogodogo vya wajasiriamali itahamia sasa katika Jiji la Dodoma.
“Nawapongeza pia kwa kukamilisha zoezi la uuzaji wa hisa zenu kwani zilichangamkiwa vizuri sana na nilielekeza manispaa za Dar es Salaam ziwe za kwanza, na wakaitikia wito vizuri.
"Mwito wangu kwa halmashauri nyingine ikiwemo Jiji la Dodoma kuwekeza benki hii halisi ya watanzania yenye malengo na muelekeo wa kusaidia wajasiriamali wadogo wadogo ambayo inaenda sambamba na malengo ya manispaa kwani benki hii ilianzishwa na manispaa
“Mnafanya kazi nzuri, endeleeni kufanya vizuri, sijapata malalamiko, ongezeni juhudi ya kuhudumia wateja wenu kwa ufanisi na kutanua huduma zenu hadi katika majiji na manispaa nyingine,” ameongeza Waziri Jafo.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfery Ndalahwa alisema benki hiyo iliyoanzishwa miaka 16 iliyopita kwa agizo la Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa, imekuwa ikijiendesha kwa mafanikio makubwa hadi 2012 ilipobadili leseni yake na kuwa Benki ya Biashara DCB badala ile ya Benki ya Watu wa Dar es Salaam.
Amesema imewekeza vizuri katika asuala ya kidigitali ikiwa na mawakala zaidi ya 1000 nchini kote ikiwa na mfumo ambao unakuwa rahisi kwa mteja kupata huduma mahali popote.
“DCB imekuwa ikijiendesha kwa faida, hadi sasa tumelipa gawio kwa manispaa za Dar es Salaam ambao ni wanahisa waanzilishi kiasi cha shs bilioni 4.4 huku kwa mwaka 2018 benki ikitengeneza faida ya shs bilioni 1.9”, alisema.
Kuhusu zoezi la uuzaji wa hisa lililoanza Novemba 2018 na kumalizika Januari 31,Ndalahwa alisema zoezi lilikamilika na wanasubiri kukamilika kwa taratibu za ndani ili kuweza kuendelea na michakato mingine.
DCB iliyoanzishwa miaka 16 iliyopita ikijulikana kama Benki ya Watu wa Dar es Salaam ilibadili leseni yake na kuitwa Benki ya Biashara DCB ikiwa na matawi saba moja likiwa jiijini Dodoma huku ikiwa mbioni kufungua matawi katika mikoa mingine.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...