Na Moshy Kiyungi, Dar es Salaam

Aprili 2, 2019

Ili kufikia lengo tarajiwa, mtu anahitajika kutanguliza nia ya dhati bila kuogopa viwazo vinavyoweza kujitokeza ili kukukwamisha.

Katika makala haya yanamzungumzia mwanamama maarufu Dorothy Masuka ambae kama yu hai, basi ni bibi wa umri wa miaka 84 kwa sasa. Pasi shaka kutajwa kwa jina hilo nitawagusa wengi waliokuwa vijana wa miaka ya nyuma.

Masuka ni mwanamuziki aliyezaliwa katika mji wa Bulawayo, nchini   Zimbabwe (zamani South Rhodesia) mwaka 1935.

Baba yake alikuwa na asili ya Zambia wakati mama yake ni wa kabila la Zulu toka Afrika ya Kusini. Akiwa msichana mdogo wa miaka 12, familia yake ilihamia nchini Afrika ya Kusini, ambako kwa bahati nzuri alifanikiwa kuingizwa katika shule ya bweni ya Wakatoliki katika jiji la Johannesburg.

Kadri alivyokuwa akiendelea kukua, talanta yake ya uimbaji ilikubalika katika kipindi kifupi, akaanza kufanya matamasha ya shuleni kwake. Masuka alikuwa akihusudu sana na muziki wa Jazz ya Wamarekani pia muziki wa Kiafrika hususani wakati ambao mwanamuziki wa Kiafrika Dolly Rathebe, alipopata umaarufu mkubwa.

Kampuni iliyokuwa imeanzishwa ya kurekodi nyimbo ilikuwa na jina la Troubador, ilimwalika Dorothy kurekodi nyimbo ambazo ziliweza kufanikiwa. Hiyo ndiyo ilikuwa kengele ya mwazo ikiashiria kufikia mafanikio aliyokuwa akiyapenda.

Masuka wakati fulani akiwa na umri wa miaka 16, alikataliwa kuingia shule ya bweni hivyo akalazimika kwenda mjini Durban, nchini Afrika ya Kusini ambako alijiunga katika shule iliyojulikana kwa majina ya African Ink Spots, ikimilikiwa na  Philemon Mogotsi.

Licha ya uongozi wa shule na pamoja na familia yake kumtaka kubakia katika shule hiyo, yeye aliamua kurudi tena Bulawayo, nchini Zimbabwe. Alipofika huko wawezeshaji pamoja na Kampuni ya kurekodi walimuwezesha kufikia adhma yake ya uimbaji.

Wakati akiwa safarini akirudi  Johannesburg, Masuka alitunga wimbo ukapewa jina la 'Hamba Notsokolo'.

Alipotimiza umri wa miaka 20, picha zake zilianza kuonekana juu ya majarida mbalimbali. Aidha alipata fursa ya kutalii na kushiriki onesho nchini Afrika ya Kusini, likiwajumuisha wanamuziki wakubwa toka Afrika. Katika onesho hilo aliweza kukutana na wanamuziki wakubwa akiwemo Miriam Makeba, bendi maarufu ya African Jazz na nyingine nyingi.

Makeba alimtaja Dorothy na kumuimba katika wimbo wake wa 'Kulala' wakati wa onesho lake  lililorekodiwa katika album. Hata hivyo mwanamuziki mwingine toka Afrika ya Kusini Aura Msimang, pia aliuimba wimbo huo. Baadhi ya nyimbo zake zilizokuwa na ujumbe mkali, ambazo mamlaka husika ilizilizuia zisichezwe.

Dorothy Masuka alikuwa katika mji wa  Bulawayo mwaka 1961, wakati ambapo alinyang’anywa kwa nguvu moja wa nyimbo zake alizorekodi. Baadae alishauriwa kutorudi mjini humo hadi atakapohakikishiwa usalama wake.

Mnamo mwaka 1965 Dorothy aliwahi kuwa mkimbizi na kufanya kazi katika nchi za Malawi na hapa nchini Tanzania. Mwaka huohuo alirejea tena katika mji wa Bulawayo, nchini Zimbabwe. 

Hakuchukuwa kipindi kirefu akatoroka tena na akurudi nchini humo hadi pale nchi hiyo ya Zimbabwe ilipoundwa mwaka 1980. Dorothy Masuka alirekodi album iliyotikisa ulimwengu ya ‘Pata Pata’ mwaka 1990.

Baadae alirudi tena katika mji aliokuwa akiupenda mno wa Johannesburg, ambako lirekodi album nyingine ya Magumede.

Mwaka 2001 album yake Mzilikazi ilirekodiwa. Mwanamama huyo bado huweza kusafiri na kucheza muziki sehemu mbalimbali duniani.

Aidha alitembelea miji wa London na mwaka 2002, alikuwa katika jiji la New York nchini Marekani ambako aliungana kupiga muziki jukwaa moja na kundi la Mahotella Queens.

Desemba 2002, Dorothy alifanya onesho huko London kwa nia ya kuitangaza CD yake mpya ya ‘The Definitive Collection’

Mwisho.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0784331200, 0713331200, 0736331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...