MKUU wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Simbalimile Mofuga
amempongeza Rais John Magufuli kwa kufanya maendeleo makubwa kwenye
uongozi wake wa awamu ya tano mithili ya Rais aliyekaa madarakani kwa
muda wa miaka 40.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya
halmashauri hiyo linalojengwa na Kampuni ya Mzinga Holding Ltd, katika
kata ya Dongobesh litakalogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.7
Mofuga alisema Rais Magufuli amewatendea mengi watanzania.
Alisema pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati aliyoitekeleza ikiwemo
ya ujenzi wa barabara za juu, kununua ndege, elimu bila malipo na
mradi mkubwa wa umeme pia amefanikisha miradi ya maendeleo kwenye
elimu, afya na maji.
Alisema kwa muda wa miaka minne ya utawala wa awamu ya tano serikali
ya awamu ya tano imefanyika maendeleo mengi kwenye kila sehemu hapa
nchini huku wilaya ya Mbulu ikiwa na miradi mingi ya maendeleo.
"Tunawashukuru sana viongozi wa dini kwa kumuombea Rais Magufuli kwani
maendeleo aliyoyafanya Tanzania utadhani amekaa madarakani kwa muda
mrefu wa zaidi ya miaka 40," alisema Mofuga.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo, Hudson Kamoga
alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa jengo
hilo litakalokuwa mfano wa majengo bora mapya ya halmashauri nchini.
Kamoga alisema Rais John Magufuli ameipendelea halmashauri ya wilaya
ya Mbulu kwani ameiwezesha kufanikisha miradi mingi ya maendeleo.
"Pamoja na jengo jipya la halmashauri ya wilaya litakalogharimu
shilingi bilioni 4.7 pia amewezesha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji
Dongobesh na fedha kwenye idara za afya, elimu na miundombinu,"
alisema Kamoga.
Mbunge wa jimbo la Mbulu Vijijini, Flatei Maasay alimshukuru Rais
Magufuli kwa kufanikisha mradi huo na ujenzi wa hospitali ya Wilaya,
kituo cha afya Dongobesh, kwani ndiyo faida ya kuchagua kiongozi
anayetekeleza ilani ya uchaguzi.
Massay alisema wanamshukuru Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi
mingi ya maendeleo ya elimu, afya, maji, miundombinu ikiwemo na ujenzi
huo ambao utasogeza huduma ya jamii karibu zaidi na wananchi wa jimbo
hilo.
Alisema ili mwananchi wa Haydom afike Mbulu mjini makao makuu ya
halmashauri hiyo atakwenda kilomita 86 na Dongobesh kilomita 52 hivyo
hapo patakuwa karibu zaidi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Joseph Mandoo alisema
madiwani wa halmashauri hiyo ndiyo waliamua makao makuu yawe Dongobesh
baada ya wataalamu kupendekeza eneo hilo.
Mandoo alisema wataalamu hao waliagizwa na madiwani wafanye utafiti wa
kata inayofaa kuwa makao makuu ya halmashauri hiyo nao wakapendekeza
kata ya Dongobesh.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Simbalimile Mofuga akizungumza na wananchi wa kata ya Dongobesh wakati akizindua ujenzi wa jengo la makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya hiyo lenye thamani ya shilingi bilioni 4.7.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Stanley Kamoga (kushoto) akimuangalia mzee wa Kata ya Dongobesh aliandika historia ya eneo la ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Simbalimile Mofuga (watatu kushoto) akichimba kwa sururu wakati azindua ujenzi wa jengo jipya la makao makuu ya halmashauri ya wilaya hiyo lenye thamani ya shilingi bilioni 4.7 kwenye kata ya Dongobesh litakalojengwa na kampuni ya Mzinga Holding Ltd.
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Simbalimwile Mofuga
(katikati) akizungumza wakati akikagua ramani ya jengo jipya la
Halmashauri ya Wilaya hiyo linalojengwa na Kampuni ya Mzinga Holding
Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 4.7 katika kata ya Dongobesh,
kushoto ni mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini Flatei Maasay na kulia ni
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Joseph Mandoo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...