Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Mbunge wa Mtwara Vijijini Hawa Ghasia pamoja na Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Mtwara wakivuta utepe kuashiria uwekaji wa jiwe la Msingi la mradi wa Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara hafla iliyofanyika leo tarehe 2 Aprili 2019 mkoani humo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakwanza kutoka kulia pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Ujenzi, Wabunge pamoja na viongozi wa mkoa, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mitambo itakayotumika katika ujenzi wa mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika eneo la uwanja wa ndege wa Mtwara kabla ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa upanuzi wa uwanja huo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na wananchi waliofika katika uwanja wa ndege wa Mtwara mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la mradi wa Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara hafla iliyofanyika leo tarehe 2 Aprili 2019 mkoani humo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipiga makofi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa kushoto pamoja na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Isaack Kamwelwe kulia wakati Kwaya ya Chuo cha Utumishi wa Umma tawi la Mtwara na Dar es Salaam ilipoku wa ikitumbuiza uwanjani hapo. PICHA NA IKULU
===============================
===============================
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02
Aprili, 2019 ameanza ziara ya kikazi ya siku 3 Mkoani Mtwara ambapo mara baada
ya kuwasili ameweka jiwe la msingi katika upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mtwara
na kuzungumza na wananchi.
Uwanja
huo unafanyiwa upanuzi ikiwa ni miaka 67 tangu ulipojengwa mwaka 1952 ambapo
upanuzi unahusisha kuongeza upana wa njia ya kurukia kutoka meta 30 hadi 45, kuongeza
urefu wa njia ya kurukia kutoka meta 2,258 hadi 2,800, kujenga maegesho mapya
ya ndege, kujenga barabara na maegesho ya magari, kuweka vifaa vya zimamoto na
usalama, kujenga uzio na kuweka mfumo wa umeme wa akiba.
Upanuzi
huo umeanza Juni 2018 na utakamilika Septemba 2020 kwa gharama ya shilingi
Bilioni 50.4, fedha ambazo zimetolewa na Serikali ya Tanzania.
Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)
Mhandisi Christianus Ako amesema upanuzi huo ukikamilika utauwezesha uwanja wa
ndege wa Mtwara kupokea ndege za daraja 4E ambapo ndege kubwa na ndogo zitakuwa
na uwezo wa kutua na kuruka.
Akizungumza
katika sherehe hizo Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano imemua
kuupanua uwanja huo ili kufungua fursa nyingi zaidi za kiuchumi katika mkoa wa
Mtwara na kwamba upanuzi kama huo unafanywa katika viwanja vingine 11 hapa
nchini.
Kuhusu
kuchelewa kuanza kwa kazi za upanuzi huo kutokana na Mkandarasi M/S Beijing Construction Engineering Group Company
Ltd
kutopatiwa sehemu ya malipo ya awali, Mhe. Rais Magufuli ametoa siku 5 kwa
Mawaziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Fedha na
Mipango kuhakikisha asilimia 15 ya awali ambayo ni sawa na shilingi Bilioni 7
zinalipwa, lakini amemuonya Mkandarasi huyo kuhakikisha anafanya kazi vizuri (usiku na mchana) na kwa
kuzingatia muda kwa kuwa taarifa zinaonesha Mkandarasi huyo hajafanya kazi ya
kuridhisha katika uwanja wa ndege wa Mwanza.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amezungumzia ununuzi wa korosho uliofanywa na Serikali baada
ya wanunuzi binafsi kutaka kununua korosho kwa bei ya chini ya shilingi 2,000
na kueleza kuwa baada ya Serikali kuamua kununua korosho hizo kwa shilingi
3,300 kwa kilo, jumla ya tani 156,865 zenye thamani ya shilingi Bilioni 578.7
kutoka kwa wakulima 373,149 zimenunuliwa na hivyo kuwaokoa wakulima hao
wasipoteze mapato makubwa.
Kufuatia
baadhi ya wenye korosho zinazozidi kilo 1,500 kukiri na kuomba radhi baada ya
kushindwa kuuza korosho zao kwa Serikali kutokana na kuzikusanya kwa njia
zisizokubalika (Kangomba),
Mhe. Rais Magufuli amekubali kuwasamehe na ameagiza Wizara ya Fedha na Mipango
kutoa shilingi Bilioni 50 katika siku 2 zijazo ili waanze kulipwa.
Hata
hivyo ameonya kuwa watakaoruhusiwa kuuza ni wale wanaozimiliki korosho hizo bila
dosari nyingine na ametaka mchezo wa kununua korosho kwa mtindo wa Kangomba
ukome.
“Najua kuna
watu 18,000 wakiwemo wale wasiokuwa na mashamba 780 hawajalipwa, nimeshatoa
maagizo zitolewe shilingi Bilioni 50 ili waanze kulipwa, nafanya hivi kwa
sababu wamekiri na wameomba radhi kwa kufanya kangomba, sasa msirudie tena
mchezo huu, achene kuwanyonya wakulima”
amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Katika
mkutano huo Mhe. Rais Magufuli amewaonya viongozi wa Mkoa wa Mtwara kuacha
kugombana wao kwa wao na badala yake amewataka washirikiane kusukuma mbele
gurudumu la maendeleo la mkoa huo. Pia amewaomba viongozi wa Dini wasaidie
kuwaunganisha viongozi hao.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Mtwara
02
Aprili, 2019
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...