Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg wakiminya kitufe kwa pamoja kuashiria uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimshukuru Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg mara baada ya uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu wa umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg wakiangalia mradi huo wa umeme utakavyosambaza umeme katika maeneo mbalimbali kutoka kutoka Makambako hadi Songea
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg, Waziri wa Nishati Medard Kalemani wakielekea eneo la uzinduzi wa mradi huo mkubwa wa usafirishaji wa umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Balozi wa Sweden hapa nchini Anders Sjoberg wakipungia mikono wananchi waliohudhuria katika sherehe hizo za uzinduzi wa mradi wa umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi katika uzinduzi wa mradi wa Ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme KV 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na vituo vya kupooza umeme KV 220/33 katika sherehe zilizofanyika Songea mkoani Ruvuma.
Moja ya kituo cha kupooza umeme cha Songea.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizindua kituo Kikuu cha Mabasi cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kituo Kikuu cha Mabasi cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Sehemu ya wananchi wa Songea mkoani Ruvuma wakiwa ndani ya Uwanja wa mpira wa Majimaji kumsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli. PICHA NA IKULU
===== ======== ======== =======
Majira
ya jioni, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Majimaji ambapo amewahakikishia
kuwa Serikali anayoiongoza inatekeleza miradi hii mikubwa ili kuimarisha ustawi
wa wananchi na kuwawezesha kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali
zikiwemo ujenzi wa viwanda.
===== ======== ======== =======
Rais Magufuli aendelea na ziara Ruvuma azindua mradi wa umeme na aweka jiwe la msingi la stendi na barabara
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 06
Aprili, 2019 amezindua mradi wa njia ya umeme ya msongo wa KV 220 kutoka
Makambako hadi Songea na ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mabasi
na barabara za lami katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.
Sherehe
za uzinduzi wa mradi wa njia ya umeme zimefanyika katika kituo cha kupoza na
kusambaza umeme kilichopo Unangwa Mjini Songea na zimehudhuriwa na viongozi
mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Balozi wa Sweden hapa
nchini Mhe. Anders Sjöberg,
Mawaziri, Wabunge na viongozi wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Kaimu Mkuu wa
Mkoa huo Mhe. Godfrey Zambi.
Mradi
huo umehusisha ujenzi wa njia ya umeme yenye urefu wa kilometa 245, upanuzi wa
kituo cha kupoza umeme cha Makambako, ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza
umeme vya Madaba na Songea na usambazaji wa umeme wa msongo wa kilovoti 33
zenye urefu wa kilometa 900 zilizounganishwa kwa wateja 22,700 katika Wilaya za
Njombe, Ludewa, Mji wa Makambako, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na
Mbinga.
Ujenzi
wa mradi huo umegharimu shilingi Bilioni 216 na Milioni 941, fedha ambazo
zimetolewa kwa mkopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Sweden na Serikali ya
Tanzania, na baada ya kukamilika kwake Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezima mitambo
ya kuzalisha umeme kwa mafuta katika vituo 5 na hivyo kuokoa shilingi Bilioni
9.8 kwa mwaka.
Waziri
wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutilia
mkazo wa kuhakikisha mradi huo unaanza kutekelezwa mara alipoingia madarakani
na kwamba hivi sasa Mkoa wa Ruvuma wenye mahitaji ya megawati 12 za umeme
unapata megawati 48 zitakazowezesha uanzishaji wa viwanda na vijiji vyote
kupatiwa umeme ifikapo mwaka 2012.
Mhe.
Kalemani amebainisha kuwa tangu Mhe. Rais Magufuli aingie madarakani idadi ya
vijiji vilivyopatiwa umeme kupitia Wakala wa Umeme Vijiji (REA) imeongezeka
kutoka 2,018 hadi kufikia 6,464 (sawa na ongezeko la asilimia 214).
Balozi
wa Sweden hapa nchini Mhe. Andrers Sjöberg
ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri na Sweden
ambao umesaidia kutekelezwa kwa miradi mingi ya maji tangu miaka ya 90 na
baadaye kufuatiwa na miradi ya kupeleka umeme vijijini ambako wananchi wengi
wamenufaika hususani wanawake.
Kwa
upande wake, Mhe. Rais Magufuli ameishukuru nchi ya Sweden kupitia SIDA kwa
ufadhili wake katika mradi huo na ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo pamoja
na mradi mkubwa ambao Tanzania inaujenga hivi sasa wa kuzalisha umeme katika
mto Rufiji utasaidia kuinua uchumi kupitia viwanda na pia utasaidia kuokoa
mazingira kwa kuwa wananchi watatumia umeme badala ya kuni na mkaa ambao
unapatikana kwa kukata miti.
“Takwimu
zinaonesha ekari 400,000 za miti huvunwa kila mwaka kwa lengo kupata kuni na
mkaa wa kupikia, hii yote inasababishwa na umeme kidogo na wa gharama kubwa
tulionao, tunapotekeleza miradi hii tutaokoa uharibifu huu wa mazingira, kwa hiyo
nakuomba Mhe. Balozi ukawaeleze Mabalozi wenzako kuwa Tanzania tunapotekeleza
miradi hii tunataka kuimarisha uchumi wetu na pia kuokoa misitu yetu” amesema
Mhe. Rais Magufuli.
Ametoa
wito kwa Sweden na wadau wengine wa maendeleo kuendelea kushirikiana na
Tanzania katika uzalishaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali
vikiwemo gesi, makaa ya mawe, urani, upepo na joto ardhi, na pia amewataka
Watanzania waongeze juhudi katika utunzaji wa mazingira.
Kabla
ya kuzungumza na wananchi wa Manispaa ya Songea katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika uwanja wa Majimaji, Mhe. Rais Magufuli ameweka jiwe la msingi
katika mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi katika eneo la Shule ya Tanga, na
ujenzi wa barabara za Manispaa hiyo ambapo ameagiza miradi hiyo ikamilike kwa
wakati na kwa ubora unaotakikana.
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani
Jafo amesema ujenzi wa mradi huo ulioanza tarehe 25 Machi, 2018 unatarajiwa
kukamilika tarehe 30 Septemba, 2019 kwa gharama ya shilingi Bilioni 6.2 na
utahusisha ujenzi wa kilometa 2 za barabara, eneo la kuegesha mabasi 92 na ujenzi
maegesho ya magari mengine na huduma mbalimbali. Manispaa ya Songea ni miongoni
mwa Halmashauri 18 zinazotekeleza mradi kama huo hapa nchini.
“Juzi nimefungua
barabara ya Mtambaswala – Mangaka – Nakapanya – Tunduru yenye urefu wa kilometa
202, jana nimefungua barabara ya Tunduru – Namtumbo yenye urefu wa kilometa
193, leo nimezindua mradi mkubwa wa umeme ambao umewaletea umeme mwingi kupita
mahitaji yenu na sasa tunaanza maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Lumecha –
Londo – Ifakara, hizi zote ni juhudi za kuimarisha fursa za uchumi, nataka
mnufaike” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mawaziri
wengine waliongozana na Mhe. Rais Magufuli wamewahakikishia wananchi wa Ruvuma
kuwa Serikali imeanza kuchukua hatua za kuhakikisha wanapata pembejeo za kilimo
za kutosha na kwa gharama nafuu, kuimarisha miundombinu ya barabara na
ukarabati wa uwanja wa ndege.
Akiwa
uwanjani Majimaji, Mhe. Rais Magufuli amezungumza na wanafunzi wa shule ya
Sekondari ya Wasichana ya Songea ambapo ametoa shilingi Milioni 5 kwa ajili ya
shule hiyo na ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha inatatua tatizo la mabweni na
vyoo.
Mhe.
Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mhe. Mama Janeth Magufuli kesho
anaendelea na ziara yake hapa Mkoani Ruvuma ambapo ataweka jiwe la msingi la
ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay na kuzungumza na wananchi.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Songea
06
Aprili, 2019
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...