Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mashindano ya mbio za Heart Marathon zitakazofanyika siku ya jumapili 28 Aprili 2019 katika viwanja vya Coco Beach kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo leo katika ukumbi wa taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI Naiz Majani.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Naiz Majani akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu mashindano ya mbio za Heart Marathon zitakazofanyika Jumapili 28, 2019 katika viwanja vya Coco Beach kwa ajili ya kuchangia matibabu ya watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji wa moyo leo katika ukumbi wa taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Ukusanyaji Damu kutoka Damu salama kanda ya mashariki Judith Goshashi. Picha na JKCI.

Na Zawadi Masinde- JKCI

25/04/2019 Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam pamoja na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki katika mashindano ya Heart Marathoni ili waweze kuchangia matibabu ya moyo kwa watoto. Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi wakati akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu mashindano ya mbio hizo yatakayofanyika tarehe 28/04/2019.

Prof. Janabi alisema mtoto anaweza kuwa na ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nayo hii inatokana na sababu za kurithi, mama kutokupata chanjo wakati akiwa mjamzito, unywaji wa pombe pamoja na uvutaji wa sigara. Lakini pia mtoto anaweza kupata ugonjwa wa moyo kwa njia ya mfumo wa hewa au chakula ambapo mtoto asipopata matibabu kwa wakati bakteria wanashambulia valvu za moyo.

“Kwa upande wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nao kila watoto 100 wanaozaliwa hai mmoja anatatizo la moyo. Kwa mwaka Taasisi yetu inapokea zaidi ya watoto 1000 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo na ya kuambukizwa . Kwa sasa watoto 512 wako katika orodha ya kufanyiwa upasuaji wa moyo”,.

“Mwananchi akishiriki mbio za Heart Marathoni kwa kujisajili kwa Tshs. 30,000/= au kumthamini mtoto mmoja kati ya hao 1000 kwa kumlipia gharama ya upasuaji wa Tshs. 2,000,000/= kutapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya watoto wanaosubiri kufanyiwa upasuaji”, alisema Prof. Janabi.

Prof. Janabi alimalizia kwa kusema lengo kuu la mashindano hayo ni kupata fedha za kuchangia matibabu ya watoto walio na matatizo ya moyo ambao wazazi wao hawana uwezo.

Naye Mkuu wa Idara ya ukusanyaji Damu kutoka Damu Salama kanda ya Mashariki Judith Goshashi aliwaomba wananchi kujitokeza siku hiyo ili waweze kuchangia damu kwa ajili ya watoto watakaofanyiwa upasuaji wa moyo. Alisema mtoto mmoja anayefanyiwa upasuaji wa moyo anatumia chupa tano hadi saba za damu hivyo basi kujitoa kwa wananchi kuchangia damu kutasaidia kuokoa maisha ya watoto watakaofanyiwa upasuaji.

Judith alisema, “Kuna baadhi ya makundi ya damu ni adimu kupatikana na yamekuwa yakituletea changamoyo pindi anapotokea mgonjwa mwenye kundi hili la damu, makundi hayo ni O-,B- na AB- . Ninawaomba wananchi wenye makundi haya ya damu waje kuchangia damu kwa ajili ya watoto wetu”.

Mgeni rasmi katika mashindano hayo atakuwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga pamoja na mwenyeji wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu .

Washiriki wote wa mashindano hayo watapewa zawadi za medali pamoja na T- shirt ambapo washindi wa kwanza hadi wa tatu kwa Km. tano na kumi watapewa fedha taslimu. Mshindi wa kwanza hadi wa kumi kwa Km. 21 kukimbia na kuendesha baiskeli watapewa fedha taslimu. Kwa upande wa watoto watakaoshiriki mbio za mita 700 mshindi wa kwanza hadi wa tatu watapewa fedha taslimu.

Kauli mbiu ya mashindano hayo ni “KIMBIA SAIDIA WATOTO WENYE UGONJWA WA MOYO”,.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...