Na Ripota Wetu,Globu ya jamii

MBUNGE wa Jimbo la Kahama Mjini Jumanne Kishimba (CCM), ameamua kumshauri Waziri wa Madini au Spika wa Bunge Job Ndugai kuunda Tume au Kamati ambayo itajikita kuchunguza gharama za uzalishaji katika Mgodi wa Buzwagi.

Kwa mujibu wa Kishimba ameliambia Bunge kuwa mgodi huo unatakiwa kufungwa au kufukiwa wakati bado una kiwango kikubwa cha dhahabu.

Akizungumza Bungeni Mjini Dodoma wakati akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Madini wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka 2019/2020 amesema mbali na kuipongeza Wizara hiyo kwa kazi nzuri, lakini wakati wa ziara ya Makamu wa Rais kwenye mgodi huo, Meneja wa Mgodi huo aliwaambia wanataka kuufunga kutokana na ukubwa wa gharama za uzalishaji.

Kishimba ameelezea kusikitishwa kwake na uamuzi wa kutaka kwenda kuufunga au kuufukia mgodi huo wa Buzwagi wakati bado una kiwango kikubwa cha dhahabu.Pamoja na uamuzi huo meneja huyo aliwaambia kiasi cha dhahabu kilichopo ndani ya mgodi huo. Kwa mujibu wa Kishimba kiasi hicho ni sawa na tani 31 za dhahabu.

Kishimba amesema kuwa alichodai meneja huyo wa mgodi ni kwamba gharama zao za uzalishaji ni kubwa na kwamba tani 31 za dhahabu ni sawa dola za Marekani bilioni moja na laki mbili ambazo ni sawa na Sh.trilioni 28.

"Kuufukia mgodi wa dhahabu wenye Sh. trilioni 28 wakati tuna uwezo wa kufunga Mto Rufiji tukapata umeme ni jambo la kushangaza. Mheshimiwa Spika lazima lawama tuzipeleke kwa wataalamu wetu.

"Kweli ni wavivu wa kufikiri, hauwezi kuletewa ripoti na mtu mmoja tena mwenye mgodi ukakubali kuufukia mgodi wako wenye thamani ya Sh. trilioni 28 ndani wakati wewe una shida ya kujenga treni ya mwendo kasi (SGR) na unataka kuziba Mto Rufiji.

"Haiwezekani Spika, kitu ambacho kinahuzunisha sana Serikali kwenye sheria yetu mpya ina asilimia 16 mle ndani, ina maana na Serikali itapoteza kodi, lakini alichosema meneja wa mgodi ni kuwa gharama zao ni kubwa,"amesema Kishimba.

Ameongeza kuwa "Nitoe ombi kwa Waziri au wewe Spika iundwe Tume au kamati ndogo ambayo itakwenda kuangalia gharama za uzalishaji katika mgodi huu zile ambazo zinaweza kuondolewa, ziondolewe.

"Lakini Serikali kwa upande wake ifikirie, maana Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) peke yake inapata Sh.bilioni 2 kwa mwezi, Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) zaidi ya Sh.bilioni 20, Idara ya Maji tunapata zaidi ya Sh. bilioni 4, hawa na wao wanaweza kupunguza viwango vyao maana kama mgodi utafungwa maana yake na wenyewe hivi viwango vyao havitafanya kazi popote."

Mbunge huyo ambaye amekuwa akisimama imara kutetea wananchi wa jimbo lake na Watanzania kwa ujumla kwenye masuala ya kitaifa, amesema kuhusu mgodi huo amekuwa akizungumza na Waziri mara kwa mara, lakini bado anawasiwasi wataalam waliopo ni wavivu. 

Pamoja na hayo Kishimba ametumia nafasi hiyo kuzungumzia suala zima la madini ambapo amesema utajiri wa Waraabu ni mafuta na wanapata utajiri pale mafuta yanapopanda bei.

"Kwetu sisi tunayo dhahabu, wahasibu wetu wanachanganya bei ya kiwanda na madini, dhahabu haipandi kwa ajili ya gharama za uzalishaji...inapanda kulingana na hali inavyoendelea duniani,"amefafanua Kishimba na kwamba Duniani kote kama kuna hofu au tatizo lolote dhahabu nayo lazima itapanda.

Mbunge huyo amesema kilichoongezeka hapo si kwa sababu ya uzalishaji, bali kwa sababu ya mahitaji duniani tofauti na kiwanda na kuongeza Serikali ya Tanzania kama wahasibu au wataalamu waliopo watakubali, basi kuna utajiri mkubwa pale bei ya dhahabu inapopanda.

Amesisitiza kuwa "Hii fedha Spika siyo fedha ya mwenye mgodi na hawezi kuidai kwa sababu hata dhahabu isipopanda yeye anaendelea na uzalishaji na faida anapata. Waarabu wanatajirika pale bei ya mafuta inapopanda, ile tofauti yote inatakiwa kuwa mali ya Serikali na si ya mwenye mgodi, maana hicho ni akiba ya hiyo nchi si ya mwenye mgodi," amesema.

Kishimba wakati anazungumza Bunge lilikuwa likimsikiliza kwa umakini ambapo pamoja na kuomba kuundwa kwa tume ya kuchunguza mgodi huo amesisitiza umuhimu wa watalaam kuchangamka na kuondoa uvivu uliopo kwani kwa upande wake anaona baadhi ya watalaamu ni tatizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...