Na Robert Hokororo

Hivi karibuni Serikali ilipiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko aina ya plastiki maarufu kama ‘rambo’ inayotumika kubebea bidhaa.

Katazo hilo lililotangazwa bungeni jijini Dodoma Aprili 9, 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa tayari limeanza kutekelezwa na ifikapo Juni mosi, 2019 ni mwisho wa matumizi yote ya mifuko hiyo. 
 
Katika kusimamia katazo hilo na kuhakikisha linatekelezwa kwa ufanisi, Ofisi ya Makamu wa Rais yenye dhamana ya kusimamia utunzaji wa Mazingira imeunda kikosi kazi ambacho kinaundwa na taasisi mbalimbali za Serikali.

Ni heri kuzuia kuliko kuponya hivyo Serikali imechukua hatua za kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ili kuepusha athari mbalimbali za kiafya zinazoendelea kujitokeza.

Imezoeleka kutumika kwa mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali hususan za vyakula bila kujali athari za mifuko hiyo kwa afya za binadamu, wanyama na mazingira.

Mifuko hii baada ya matumizi imekuwa ikitupwa ovyo na hata ikitupwa kwenye mashimo ya taka huweza kupeperushwa kwa upepo na kusambaa hivyo husababisha uchafuzi wa mazingira. Hata ikichomwa moshi wake una athari kwa binadamu.

Pia mifuko ya plastiki haiwezi kuoza kwa haraka katika mazingira wanadamu walipo kwani inakadiriwa kuweza kudumu hadi zaidi ya miaka 500 na hivyo kuleta athari za muda mrefu n ahata ikichomwa huleta madhara ya kiafya.

Madhara mengine yanayoweza kutokea ni kusababisha mafuriko katika maeneo ambayo kuna mifereji kutokana na kuziba kwa miundombinu ya majitaka na mifereji ya mvua.


Aidha, wanyama ikiwemo mifugo hufa pindi wanapokula na kumeza mifuko hiyo la na kuimeza mifuko hiiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba anafafanua kuwa Serikali inahakikisha katazo hilo linakuwa na nguvu kisheria.

Anasema Serikali imeandaa kanuni za katazo hilo zitakazotangazwa katika gazeti la Serikali chini ya Sheria ya Mazingira na kutoa adhabu ya faini au kifungo kwa mtu atakayekiuka utaratibu uliowekwa.

Waziri Makamba anabainisha kuwa katazo hilo la mifuko ya plastiki si la kushtukiza kwani limekuwa ni shirikishi kwa wada yaani wananchi.

Anasema kuwa Ofisi yake tayari ilisharatibu mikutano katika maeneo kadhaa nchini na kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu katazo hilo la mifuko ya plastiki.

Waziri Makamba anasisitiza Serikali itasimamia kikamilifu katazo hilo ifikapo tarehe hiyo ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakilalamika kipindi kilichotolewa ni kifupi.

Itakumbukwa kuwa awali Serikali ilitangaza kuzuia matumizi yote ya mifuko ya plastiki kuanzia Januari mosi, 2017.

Baada ya mashauriano na Shirikikisho la la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na umma ilikubali kusogeza mbele hadi Desemba 31, 2017 ili kutoa muda kwa wajasiriamali, umma na CTI kujiandaa na utekelezaji wa katazo hilo.

Kwa kutambua umuhimu na ukubwa wa jambo hilo, Serikali haikuanza kulitekeleza Januari mosi, 2018 ili kutoa muda wa ziada kwa wadau hao kujipanga zaidi.

Hivyo kutokana na hilo katazo lilisogezwa mbele hadi kufikia Juni mosi, 2019 kama ambavyo imetangazwa na kutoa muda wa kutosha wa matayarisho  

Serikali imeunda kikosi kazi kitakachoratibu utekelezaji wa zoezi hilo ambacho kinajumuisha watendaji kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Mapato Tanzaniana Idara ya Uhamiaji.

Taasisi zingine ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Hata hivyo hivyo, Waziri Makamba anawaondoa hofu wananchi kwa kusema kuwa katazo hilo la mifuko ya plastiki halitahusu baadhi ya vifungashio vya bidhaa zikiwemo maziwa, mikate.

Vifungashio vingine ni vya pembejeo za kilimo, ujenzi, dawa na baadhi ya vyakula kama korosho na vinywaji vikiwemo maziwa ambavyo ni ni lazima vikidhi viwango vilivyowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 
 Ng’ombe wakila mifuko ya plastiki iliyozagaa kitengo ambacho husababisha vifo kwa mifugo hiyo na pia haiwezi kuharibika kwa haraka hivyo husababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Mifuko ya plastiki iliyokatazwa matumizi yake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...