Na Moshy Kiyungi
SAMBA MAPANGALA ni mtunzi na mwimbaji maarufu wa kimataifa aliyejizolea sifa tele Afrika ya Mashariki na Kati hususani katika nyimbo zake za ‘Vunja Mifupa’ na ‘Dunia tunapita’

Ni mwanamuziki mwenye kipaji cha aina yake, anaye kula ‘Kuku’ katika jiji la Washington DC nchini Marekani. Alimfanyia kampeni rais Barack Obama wa Marekani mwaka 2008.

Alizaliwa huko Matadi katika mkoa uliojulikana kama Bas-Congo huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Miaka ya 1970 alipiga muziki na bendi nyingi katika jiji la Kinshasa wakati akiwa katika masomo ya Sekondari.

Kipaji cha Mapangala kigundulika kupitia tungo zake ambazo kila wimbo una ujumbe mzito masikioni mwa msikilizaji. Mfano wa karibu ni wimbo wa ‘ Dunia tunapita’ Wimbo huu unaelezea juu ya jamaa ambaye hawezi kufanya chochote kile bila kupita kwa waganga.

Kunyooka kwa Safari ya Samba Mapangala katika masuala ya muziki kulianza kuonekana mapema miaka ya 1970 alipoondoka Matadi kwenda katika Jiji la Kinshasha kwa ajili ya masomo ya Sekondari.

Sifa kubwa aliyonayo Mapangala ni ya kuweza kutunga, kuimba nyimbo kwa lugha za Lingala na Kiswahili pia uwezo mkubwa alionao wa kumiliki Jukwaa.

‘Kizuri chajiuza kibaya chajitembeza’ Usemi huu ulijidhihirisha kwa Mapangala baada ya kuonyesha umahiri mkubwa kupitia sauti yake nyororo kulipelekea kupata kazi ya kupiga muziki kwenye bendi za Bariza, Super Tukina, Bella Bella na Saka Saka katika jiji la Kinsahasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Juhudi zake katika muziki zilimfikisha kusafiri na wanamuziki wenzake kwenda Mashariki mwa Kongo mwaka 1975. Mwaka iliofuatia wa 1976 walivuka mpaka kwenda Kampala nchini Uganda hako wakaunda bendi ya Le Kinois.

Akiwa mwimbaji Kiongozi Samba Mapangala na bendi yake ya Les Kinois ilihamisha makazi toka Kampala na kwenda jiji la Nairobi nchini Kenya mwaka 1977.

Licha ya kuwa na ushindani mkali toka bendi zingine kubwa katika jiji katika hilo la Nairobi, bado Les Kinois walifanikiwa kuliteka jiji hilo kwa kasi kubwa.

Wakati huo jiji la Nairobi kulikuwa na bendi za Super Mazembe, Orchestra Les Mangelepa, Les Wanyika, Orchestra Moja One , Baba Gaston na nyingine nyingi.

Ili kuonyesha ukomavu katika muziki, Samba aliamua kujitegemea mwenyewe kwa kuunda bendi yake na kuipa jina la Orchestra Virunga mwaka 1981 bendi ambayo kwa kipindi kifupi ikakubalika na wapenzi wa muziki na kuwa moja kati ya bendi maarufu Afrika Mashariki.

Samba Mapangala hupiga muziki wake ukiwa na mchanganyiko wa staili za rumba na Soukous kutoka Kongo. Ili kuwaridhisha wapenzi wa muziki wa Nairobi na vitongoji vyake walipiga muziki kwa staili za watu wa Kenya. Rekodi ya kwanza ya Virunga iliyoitwa ‘It's Disco Time with’ ilitoka mwaka 1982.

Mapangala na bendi yake ya Virunga walisafiri kwenda nchini Uingereza mwezi Aprili 1991 na huko walifanya maonyesho makubwa takribani 23. Baada ya kufurahia mafanikio ya safari yao, walifanya safari nyingine ya mwisho mwaka 1997 wakipitia nchi za Afrika hadi Marekani ya Kaskazini.

Album za Samba Mapangala zilizopo ni pamoja na Virunga Volcano ya mwaka 1990, Evasion ya 1983, Feet on Fireya ya 1991, na Karibu Kenya iliyofyatuliwa mwaka 1995 zilizorekodiwa katika jiji la Paris nchini Ufaransa akiwashirikishwa wanamuziki toka bendi ya Les Quarters Etoiles na wanamuziki wengine nguli waliokuwa hapo Paris.

Album ya Vunja Mifupa iliyotoka mwaka 1997 ilichukua soko kubwa la mauzo hususani Afrika ya Mashariki ikizingatiwa Ujumbe unatolewa kwa lugha ya Kiswahili. Virunga Roots Volume 1, ulijumisha nyimbo zilizo katika kumbukumbu Virunga na kutolewa mwaka 2005.

Samba kwa kawaida ni mpole na mcheshi, mwaka 2000, alialikwa kwenye Sherehe ya siku ya Jamhuri ya watu wa Kenya katika jiji la London, ambapo muziki waliopiga ‘uliwachengua’ watu wote waliofika katika sherehe hiyo. Mzee wa ‘Vunja Mifupa’ Samba Mapangala alikuja Tanzania mwezi Mei 2004 kwa ziara ya wiki mbili na kufanya maonyesho kadhaa.

Nguli huyu hupenda kushirikina na wanamuziki wengine ili kubadilishana ujuzi na uzoefu. Aliwahi kupiga muziki akiwa na safu ya wanamuziki nyota toka nchi za Kenya na Tanzania.

Album yake mpya ya Song and Dance iliyorekodiwa mwaka 2006 katika Studio za Virunga reocords, wakimshirikisha mwanamuziki Bopol na wangine wakali toka bendi yake ya Orchestra Virunga. Abum hiyo iliyokuwa na nyimbo nyingi ilizinduliwa rasmi walipokuwa kwenye ziara nchi za Ulaya mwezi March 2006.

Mwezi Juni 4 2006 Samba alikuwa nchini Kenya kawa ajili shughuli maalumu ya Ecofest, Wakati wa Kampeni ya Urais wa Marekani mwaka 2008, Samba Mapangala alionyesha ni jinsi gani wananchi wa Kenya wanavyomshabikia mgombea wa kiti hicho Barack Obama. Alifyatua wimbo maalumu wa kumtakia heri Obama ulioitwa 'Obama Ubarikiwe'

SambaMapangala na bendi yake ya Orchestra Virunga walirejea Afrika ya Mashariki mapema mwaka 2009, na kutoa burudani katika jiji la Nairobi na Zanzibar ambako alialikwa katika tamasha la Sauti za Busara .

Mwishioni mwa mwaka 2009 Samba aliuongezea nguvu mfuko wa World Wildlife Fund kwa kutunga na kutoa bure wimbo wa ‘ Mlima wa Magorila’ uliokuwa ukitoa wito kusaidia kuwalinda magorila waliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Wanyamapori ya Virunga ya nchini Kenya ambako wanyama hao adimu hupatikana.

Mangwana anakumbukwa na wapenzi wa muziki wa dansi katika nchi za Afrika ya mashariki na Kati pale wasikiapo nyimbo za Hadija, Marina Nyama Choma, Alimasi, Dunia haina mwisho na Dunia tunapita. Nyingine ni Jaffar, Mapenzi hayana macho, Muniache, Virunga, Vijana, Ufunguo, Vunja mifupa, Siri na Vidonge uliopigwa kwa staili ya mduwara. Nyimbo zote zimeimbwa kwa lugha ya Kiswahili.

Samba Mapangala na familia yake wanaishi katika jiji la Washington DC nchini Marekani. 

 Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200 na 0713331200

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...