Shirika la ndege la Precision Air limetangaza kuanzishwa kwa safari zake kati ya Mwanza na Dodoma kuanzia tarehe 3 Juni 2019.

 Hatua hiyo inakuja ikiwa ni sehemu ya mikakati wa shirika hilo katika kuunganisha mji mkuu wa Dodoma na mikoa mingineyo nchini Tanzania.

Kuanzishwa kwa safari hizi kutarahisisha safari  za watu, mizigo, biashara, na huduma mbali mbali za kijamii kati ya miji hiyo miwili na kwengineko hususan baada ya uamuzi uliofanywa na serikali ya Tanzania wa kuhamisha shughuli zake za kiserikali jijini Dodoma, na kuwepo kwa bandari katika Jiji la Mwanza linalopakana na nchi jirani za Kenya na Uganda.

Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja Masoko na Mahusiano, Hillary Mremi alisema, “Kuanzia tarehe 3 Juni 2019 kutakuwepo na ndege ya asubuhi kutoka Mwanza kuelekea Dodoma itakayoruka saa 1:40 Asubuhi na kuwasili Dodoma saa 3:25 Asubuhi kila siku za Jumatatu, na kila siku za Ijumaa kutakuwa na ndege kutoka Dodoma itakayo anza safari saa 11:50 Jioni na kuwasili  Jijini Mwanza saa 1:35 jioni.”

 “Tunajivunia na tunafuraha kuwa mstari wa mbele katika kuboresha na kuunganisha miundo mbinu kwenye sekta ya usafiri wa anga, jukumu ambalo tumelitekeleza tangu kuanzishwa kwa kampuni hii. Lengo letu ni kuunganisha Tanzania katika pande zote za mashariki, magharibi, kusini na kaskazini na zaidi kupitia usafiri wa anga wenye uhakika,” alisema Mremi.

Aliendelea kufafanua zaidi kuwa mtazamo huu siyo wa shirika hili pekee, lakini pia ni mtazamo unaoafikiwa na wananchi na serikali kwa pamoja.

“Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuendeleza viwanda nchini hivyo, maboresho ya usafiri wa anga wenye uhakika ndiyo njia pekee katika kutekeleza dhamira hiyo.”

Hali kadhalika, mapema mwaka huu, umma ulishuhudia ufunguzi wa safari mpya kadha za anga kwenda na kutoka Dodoma uliofanywa na Precision Air, jambo ambalo lilipokelewa kwa furaha na wengi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...