Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akikabidhi cheti cha ufanyakazi bora kwa mmoja wa wafanyakazi bora wa Wizara ya Madini, Bi. Asteria Muhozya baada ya ufunguzi wa mafunzo kwa viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma. Wanaoshuhudia ni Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (Mb) (kushoto), Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila (wa pili kutoka kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Madini Bw. Issa Nchasi (kulia).
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) akifungua mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) na Waziri wa Madini, Mhe. Doto Biteko (Mb) wakifurahia jambo baada ya ufunguzi mafunzo kwa viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu Wizara ya Madini Bw. Issa Nchasi.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George H. Mkuchika (Mb) (hayupopichani) katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika (Mb) amewataka
viongozi na watumishi wa Wizara ya Madini kuwa waadilifu katika utendaji
kazi wao ili Tanzania iweze kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Mhe. Mkuchika ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo kwa
viongozi wa Wizara ya Madini katika ukumbi wa St. Gaspar jijini Dodoma.
Mhe. Mkuchika amesema kuwa, katika kulenga dira ya pamoja ya kufikia
uchumi wa kati ifikapo 2025 ni lazima viongozi na watumishi wa Wizara ya
Madini kufuata misingi ya maadili kama inavyoelezwa katika Kanuni za
Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2005.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, kutozingatia viapo vya maadili ni kosa
kwa mujibu wa sheria.
Mhe. Mkuchika amewataka viongozi wa Wizara ya Madini kuwa mfano wa
kuigwa katika kutekeleza kiapo cha uadillifu.
“Kiongozi unapaswa kuwa mfano katika kutekeleza kiapo chako cha
uadilifu, na kama utakuwa umesahau kiapo chako, si vibaya ukaichukua
nakala ya kiapo ofisini kwako na kujikumbusha mara kwa mara,” Mhe.
Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika amesema kuwa ni vema watumishi wa Wizara ya Madini
hasa wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya uchimbaji madini wawe
waadilifu pia ili kuongeza tija na utendaji kazi mzuri.
“Watumishi mlioko kwenye maeneo yenye shughuli za uchimbaji, muwe
waadilifu na mtangulize uzalendo wa nchi mnapotekeleza majukumu yenu”
Mhe. Mkuchika amesema.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewataka viongozi na watumishi wa Wizara ya
Madini kuepuka vitendo vya rushwa huku akinukuu maneno ya aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Hayati Koffi Annan.
“Rushwa ni ugonjwa ambao unatafuna taratibu na wenye kuleta madhara
katika jamii. Unadhoofisha demokrasia na utawala wa sheria, unaleta
uvunjifu wa haki za binadamu, unaharibu hali ya maisha, na kusababisha
kuwepo kwa mauaji na mambo mengine yanayotishia usalama wa
binadamu” Mhe. Mkuchika amesema.
Katika tukio la ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhe. Mkuchika amekabidhi vyeti
vya ufanyakazi bora kwa watumishi 12 wa Wizara ya Madini.
Mafunzo ya viongozi wa Wizara ya Madini yamefanyika lengo ikiwa ni
kukumbushana stadi muhimu za kazi, kuwajengea uwezo wa utendaji kazi
na kuongeza ari ya utekelezaji wa majukumu yao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...