Na Moshy Kiyungi
Tasnia ya muziki wa rumba kwa mara nyingine tena imekumbwa na msiba mwingine wa nguli wa muziki wa rhumba, Mose Sengo Fan Fan.
Kifo chake kilitokea zikiwa ni siku mbili kabla maziko ya aliyekuwa mwanamuziki mkongwe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Lutumba Simaro Massiya aliyezikwa Mei 05, 2019 jijini Kinshasa.
Fan Fan ambaye alikuwa amefikisha umri wa miaka 75, alifariki kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mshtuko wa moyo, akiwa nyumbani kwake barabara ya Thika, jijini Nairobi, Kenya.
Kwa mujibu wa mke wake alisema mumewe alifariki kwa ugonjwa wa moyo kuwa kuvimba, na wanatajia kumzika Juni 08, 2019.
Enzi za uhai wake Fan Fan licha ya kucharaza gitaa, pia alikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo katika bendi mbalimbali zalizozipitia kupiga muziki.
Kuthibitisha hilo Mose Fa Fan alitunga wimbo wa ‘Papa Lolo’, uliokuwa maarufu na kuweza kutikisa anga za muziki barana Afrika kutokana na mipigo na ujumbe mzito kwa jamii.
Nguli huyo alikuwa Nairobi kwa ajili ya kurekodi nyimbo zake mpya kwa kushirikiana na wanamuziki Paddy Makani na Disco Longwa.
Tabu Osusa ambaye alikuwa rafiki na producer wa mwanamuziki huyo alisema kuwa Fan Fan alikuwa akipenda kutembelea Kenya kila mwaka.
Mose Sengo alikuwa akitokea London, Uingereza ambako ndiko yalikuwa makazi yake.
Kifo cha Fan Fan kilitokea huku wananchi wa DRC walikuwa wakijiandaa kumzika mwanamuziki nguli Lutumba Simaro Massiya aliyefariki dunia Machi 30, 2019, katika hospitali moja jijini Paris nchini Ufaransa akiwa na umri wa miaka 81.
Kama alivyokuwa Lutumba, Fan Fan naye alikuwa ni miongoni mwa wanamuziki wa mwanzo waliokuwa wakiunda kundi la T.P.OK Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luanzo Luambo Makiadi.
Kifo cha Mose Sengo Fan Fan kimemuweka kwenye orodha ya magwiji kadhaa waliofariki baada ya kufanya mambo makubwa katika tansinia ya muziki ulimwenguni.
Magwiji wengine wa muziki wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo waliotangulia mbele za haki ni akina Papa Wendo, John Bokelo, Joseph Kabasele ‘Grand Kale’, Dokta Nico Kasanda, Vicky Longomba, Franco Luambo Lwanzo Makiadi, Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’, Madillu System, Baba Gaston ‘Ilunga wa Ilunga Omer, Jimmy Monimambo, Fred Mayula Mayoni, Dindo Yogo na wengine wengi.
Enzi za uhai wa Mose Sengo Fan Fan, aliwahi kuishi nchini Tanzania na kupiga muziki katika bendi za Orchestra Makassy, Super Matimila na Tancut Orchestra ya Iringa.
Aliyekuwa kiongozi na mmiliki wa bendi ya Orchestra Makassy, Mzee Makassy, ambaye sasa amestaafu kupiga muziki, alisema kuwa kifo cha Fan Fan kimemstua na kumpa simanzi kubwa kwakuwa waliwahi kufanya kazi katika bendi yake.
“Nimesikitishwa sana kawa taarifa hizi.Tulifanya kazi pamoja kwa muda mrefu mchango wake ulikuwa mkubwa…”alisema Mzee Makassy.
Alisema kwamba alikuwa amewasiliana na Fan Fan kwa mara ya mwisho miaka mitatu iliyopita, katika mazungumzo yao, alimuahidi kwamba angelikunja nchiniTanzania katika ziku za karibuni.
Kwa upande wake Tshimanga Kalala Assosa, mwanamuziki aliyewahi kufanya kazi na Fan Fan katika bendi ya Orchestra Makassy, alionesha kuwa na majonzi zaidi kwa kuwa alikuwa na ahadi ya kurekodi nyimbo mpya za Fan Fan hivi karibuni.
“Kifo chake kimenipa mshtuko mkubwa sana kwa sababu nilizungumza naye saa chache kabla ya kifo chake kumfika” alisema Assosa.
Aliongeza “Katika mazungumzo yetu, alinieleza kuwa amekwishalipia gharama zote katika moja ya studio za jijini Arusha. Tulikuwa na mpango wa kuingia studio jijini humo kwa ajili ya kurekodi baadhi ya nyimbo zake mpya…” alisema Assosa.
Mose Sengo Fan Fan aliyezaliwa Oktoba 16, 1945, huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alianza kujihusisha na muziki mwanzoni mwa miaka ya 1960.
Alijifunza muziki tangu akiwa mwanafunzi kwenye shule moja ya kanisa Katoliki nchini humo DRC.
Baadaye alikwenda kupiga muziki katika bendi za Somo Somo, Orchestra Revulution na kisha akachukuliwa kujiunga katika kikosi cha T.P.OK Jazz, ambako alikabidhiwa gitaa la pili la solo.
Fan Fan alidumu katika bendi hiyo kwa kipindi kirefu cha miaka 27, tangia mwaka 1967 hadi 1994.
Akiwa na bendi hiyo alitoa mchango mkuwa kwa kutunga baadhi ya nyimbo na kulicharaza gitaa.
Fan Fan ndiye aliyecharaza gitaa la solo katika vibao vya Djemelasi na Testament vya bendi ya T.P.OK Jazz, ambazo zilitamba sana wakati huo.
Upigaji wake wa gitaa hilo kwenye vibao hivyo umefanana kwa kiasi kikubwa na upigaji wa Franco, kiasi kwamba mashabiki na wapenzi wa muziki huo, waliamini kuwa Franco ndiye aliyecharaza gitaa hilo.
Baada ya kujigundua kwamba anaweza kufanya vizuri zaidi akiwa kwenye bendi nyingine, Fan Fan akaamua kwenda nchini Zambia na baadaye akaingia nchini Tanzania.
Akiwa nchini humu, alijiunga kwa mara ya kwanza katika bendi ya Orchestra Makassy, ambako alishiriki kurekodi nyimbo mbalimbali zikiwemo za Morema na Muungano.
Mwaka 1979, Fan Fan akawa mmoja wa waanzilishi wa kundi la Super Matimila akiwa pamoja na marehemu Ramadhani Mtoro ‘Dk. Remmy Ongara’.
Nguli huyo kwa kipindi kifupi alipiga muziki katika bendi ya Tancut Alimasi ya mjini Iringa.
Mose Sengo Fan Fan baadaye aliondoka nchini kwenda Uingereza ambako alifanya makazi ya kudumu hadi mauti nyalipomfika.
Akiwa nchini humo, alikuwa akishirikiana na baadhi ya wanamuziki wenzake kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Jamhuri ya Kongo Brazzaville kurekodi nyimbo nyingi.
Fana Fan mwaka 1993 aliondoka Uingereza akaenda nchini Ubelgiji, ambako alianzisha kundi la Bana OK. Kundi hilo liliwashirikisha wanamuziki kadhaa wa zamani wa bendi ya T.P.OK Jazz kiwemo Papa Noel, wakarekodi albamu moja.
Mwaka 1995, alirekodi albamu nyingine akiwashirikisha wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi la Somo Somo.
Alirekodi albamu nyingine iliyokuwa na jina la Bayekeleye, ikiwa na nyimbo saba za miondoko ya rhumba mwaka 2005.
Hadi mauti yanamfika, Fan Fan alikuwa anatamba na kwa kibao chake Papa Lolo, alichokirekodi nchini Kenya, ambacho kinaelezea kukithiri kwa matukio ya ushirikina katika jamii.
Wakati wa enzi za uhai wake alishiriki katika matamasha mbalimbali ya muziki katika jiji la London, Uingereza, Ubelgiji na Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, amina.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0784331200 na 0767331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...