*Asema huu si wakati wa kubembelezana na kuambiana maneno matamu
*Awapa maagizo mazito Waziri Viwanda na Biashara , Kamishna TRA
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS Dk.John Magufuli amesema ataendelea
kutengua tu iwapo aliowapa nafasi watashindwa kufanya kazi ambayo anaitarajia
na kwamba huu si wakati wa kubembelezana na kuambiana maneno mazuri.
Amesema Watanzania wanahitaji kuona
matokeo mazuri kutoka serikalini na yeye atahakikisha anatimiza kiu hiyo, hivyo
ambaye atashindwa hatamuacha abaki huko. pia ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa
hata ambao amewaapisha leo wakishindwa kutimiza majukumu yao atawaondoa tu.
Rais Magufuli amesema hayo leo Ikulu
jijini Dar es Salaam wakati wa hafla za kuwaapisha Waziri wa Viwanda na
Biashara Innocent Bashungwa, Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Charles Kichere na
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).
"Ujue Watanzania wanataka kuona
matokeo. Kuambiana maneno mazuri hakusadii.Sisi tunataka matokeo. Mimi jukumu
langu ni kuteua ili kiu ya Watanzania ifanikiwe.
"Nimpongeze Kakunda(aliyekuwa Waziri
wa Viwanda na Biashara) amekuja hapa na huko ndiko kukomaa kisiasa. Hizi kazi
ni za muda, maisha yenyewe ni ya muda. Joseph Kakunda amejitoa, amesimama hapa
na hiyo ndio sawa.
"Mimi nataka matokeo na
Watanzania wanataka kuona utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambayo
tumeahidi inatekelezwa. Changamoto za wafanyabishara ni nyingi, kulikuwa na
ubaya gani, Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri na Katibu Mkuu kukutana
na wafanyabiashara na kuzungumza nao. Kuna ubaya gani? Nani aliwazuia?Amehoji
Rais Magufuli.
Ameongeza kitendo cha Waziri wa Viwanda na
Biashara kutokutana na wafanyabiashara na kutatua matatizo yao ndio maana
wanasema hawamjui. "Hata ningemsimamisha Stella Manyanya huenda wangesema
hawamjui".
Rais Magufuli ameongeza kuwa, kuna korosho
zimekaa tu kwenye maghala , tena wakati zinavunwa hakukua na nchi nyingine
iliyokuwa na korosho lakini Wizara ya Viwanda na Biashara ikasubiri hadi nchi
nyingine nazo zimevuna korosho na kuingiza sokoni.
"Waziri Bashungwa najua baada ya
kukuteau wapo ambao wamekupongeza lakini mimi nakupa pole, maana nikiona mambo
hayaendi natakutengua tu. Waziri Kabudi na Mpango wanashindwa kusema ukweli
lakini pumbavu nimeshawaambia mara nyingi, inakuja tu licha ya kunizidi umri.
"Tuko kwenye vita haiwezekani tuko
kwenye vita halafu tunabembelazana, lazima tuseme ukweli.Katika korosho Wizara
ya Kilimo imefanya kazi yake kwa kukusanya korosho tani 223, 000 ambazo
zipo kwenye maghala.
"Wametimiza wajibu wao lakini Viwanda
na Biashara wamebangua tani 2000, hizi zingine abangue nani? Wizara ya Viwanda
na Biashara ndio inayofanya biashara lakini wameshindwa na ilikuwa nitengue
kuanzia juu hadi chini.
"Waziri Bashungwa ukienda pale
Viwanda na Biashara nenda kafanye kazi.Usimchekee mtu , ni afadhali wakuchikie
lakini niliyekuteau ni kusifu.Yale ambayo yapo pale nenda katatue,"amesema
Rais Magufuli.
"Viwanda ambavyo vimeshindwa
kufanya kazi sio tu kuviorodhesha bali kavichukue.Kwa mfano kiwanda cha nguo
pale Mbeya kinakwenda kubadilishwa kuwa cha Pipi, haiwezekani hii nchi iwe ya
kula mapipi."
Kwa upande wa TRA, Rais Magufuli amesema
kuwa Dk.Philipo Mpango akiwa Kaimu Kamishna pale TRA alifanikiwa
kukusanya kodi kutoka Sh.bilioni 850 hadi Sh.trilioni 1.3 na ndipo
alipoamua kumteua kuwa Waziri wa Fedha.
"Wengine wote mkienda pale mnabaki
kuwa tu hapo hapo mtadhani mmekariri.Aliyekuwa Kamishna wa TRA nimemtumia sms
zaidi ya 30 za malalamiko lakini ukifuatilia hakuna matokeo.Dhambi ambayo
ninayo siwezi kusahau jambo lazima nifuatilie.
"Haiwezekani Kamishna kukadiri kodi,
anakadiria vibata halafu Kamishna wa TRA upo kimya tu unamuangalia. Haiwezekani
kodi ya ndani inashuka halafu unakaa kimya.
"Kuna wafanyabiashara wanapakia
mizigo wakidai inakwenda nje lakini wakifika mpakani wanagonga mhuri na kurudi
nchini na TRA iko kila mahali, Kamishna yupo.TRA mnashikilia vifaa vya kuchimba
dhahabu, vifaa vimekaa zaidi ya mwaka mzima.
"Alikuwa anadaiwa sijui Sh.milioni
moja wakamuongezea nyingine,Wanashindwa kufahamu kuwa muwekezaji anaweza
kuongeza ajira, Siku ile ya wafanyabiashara nakuuliza na wewe(Kichere) halafu
na wewe unaangalia mwingine,"amesema Rais Magufuli.
Amesema ameamua kumteua kuwa Katibu Tawala
na huko nako akishindwa nako anamuondoa na huo ndio ukweli.
"Niliyekuteau kwenda TRA nenda
kafanye kazi, najua watasema wamepita wengi na wewe utapita na kuna watu wako
TRA wanajifanya hawagusiki, nenda kawaguse., nchi hii bila kodi
haiende,"amesema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa wanajeshi
wanahitaji mshahara na asipowalipa atawakuta pale Ikulu, atawajibu nini.
"Kwa hiyo usicheke na mtu, kuna uwezekano usiende mbinguni lakini
Watanzania milioni 50 tutakusuma tu uende mbinguni, nenda kakusanye kodi kwa
ajili ya Watanzania, bila kodi hakuna nchi.
"Kuna wafanyabishara wazuri sana na
ukienda watakupa ushirikiano, kuna wafanyabiashara walikuwa wanafoji na
mazingira yalikuwa yanaruhusu kufanya hivyo, kaa nao waulize wanaweza kulipa
ngapi.
"Kuna watumishi wanafanya mambo ya
hivyo na kusema wametumwa kutoka juu, usikubali kuendelea nao wakifanya mambo
ya hovyo timua tu, hakuna ubaya kama unao watumishi 1000 halafu 200 ukawatimua
kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao,"amesema Rais Magufuli.
Amemwambia Kamishna mpya wa TRA kuwa
anajua siku atapoingia kazini watampelekea maua na hata ambao hawastahili
kumuita bosi, watamuita bosi.
"Kwanza jana kuna ujumbe nimekutumia
wa malalamiko nadhani umeupata au bado? kuna mipaka ambayo inafanya vizuri,
Tunduma na Sirali hawafanyi vizuri , wale makamishna wa vituo hivyo fukuza.
"Tena mnaowahamisha wengi mnawapeleka
kodi , hawa ambao mtakuwa mnawaondoa peleka kwenye Wizara nyingine huko,wapeni
hata umesenja wabebe mafaili na hata ofisi yangu ikiwezekana waleteni tu
niwabebeshe mafaili,"amesema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...