Na Moshy Kiyungi
Mwigizaji mkongwe wa filamu na vichekesho nchini Tanzania Amri Athuman maarufu King Majuto, alifariki dunia Agosti 8, 2018 saa mbili kamili usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Afisa habari wa Muhimbili Aminiel Eligaisha ambapo alisema Mzee Majuto alifariki akiwa anaendelea na matibabu ambayo yalianza Julai 31, 2018.

''Hali yake ilibadilika majira ya saa tisa alasiri ya leo hivyo kuhamishwa kutoka jengo la Sewahaji kwenda ICU. Ilipofika saa 1.30 jioni, hali yake ilibadilika zaidi na madaktari walijitahidi kuokoa maisha yale bila mafanikio. Ilipofika saa mbili alikata roho'', alisema Eligaisha. King Majuto alianza kuumwa muda mrefu akisumbuliwa na tatizo la nyonga ambapo mapema Mei 2018, alipelekwa nchini India kwaajili ya matibabu.

Safari hiyo iliwezeshwa na msamaria mmoja aliyejitolea tiketi za watu wawili za kwenda nchini humo. Alirejea toka India Juni 2018, ambapo alifikia katika hospitali ya Muhimbili lakini baadaye alipata nafuu, aliruhusiwa kurudi nyumbani. Mkongwe huyo alitangaza kustaafu kuigiza baada ya kutoka India.

King Majuto akiwa nyumbani kwake hali yake ilibadilika, akarudishwa tena Muhimbili. Aidha King Majuto aliwahi kutibiwa katika hospitali ya Tumaini jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa India kwa ajili ya matibabu zaidi. Atakumbukwa kwa kazi zake nyingi za vichekesho ambazo alizifanya kwa uhodari mkubwa na kuwa kivutio kwa mashabiki wengi.

King Majuto alisaidiwa kwakiasi kikubwa na mwigizaji mwenzake Sharo Millionea, kuingia mikataba na makampuni mengi yaliyokuwa yakimuingizia fedha. Milionea alifariki kwa ajali ya gari akielekea nyumbani kwa kwa wazazi wake mkoani Tanga.

Wasifu

Amri Athuman’ King Majuto’ alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga. Alisoma shule ya msingi Msambwini, mkoani Tanga ambapo alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka 9. Licha ya vichekesho, King Majuto alikuwa na talata za utunzi, uigizaji pia ni mwandishi wa miswada.

Nguli huyu Amri Athman ndiye aliyekuwa muigizaji wa kwanza kuandaa kazi zake katika mikanda na kuuza akiwa na Kampuni ya TFC (Tanzania Film Company). Kupia uigizaji wake King Majutoalijizolea mashabiki lukuki waliokuwa wakifuatilia vichekesho vyake kwenye maonesho mbalimbali.

Pamoja na umri kuonekana ulikuwa umemtupa mkono, mkongwe huyu wa sanaa ya Komedi, Amri Athuman ‘King Majuto’ aliwahi kutamka kuwa bado hakuna wa kumpiku katika tasnia hiyo. Aliwahi kutamka kwamba kumekuwapo na wachekeshaji wengi wanaoonekana kuja kwa kasi kutaka kumfunika, lakini hilo halitakuja kutokea kwasababu anaamini uwezo wake ni mkubwa katika fani hiyo.

Alinukuliwa akitamka kwa: “Uvumilivu, nidhamu na ubunifu niwapo kazini ndiyo siri pekee ya mafanikio niliyonayo kwenye Komedi na ndiyo inayosababisha niendelee kuwa bora siku hadi siku,” alisema King Majuto. Alijigamba kuwa fani hio ya uigizaji na vichekesho aliweza kuvuna mambo mengi, vikiwamo ubunifu na msimamo kutoka kwa aliyekuwa gwiji mwenzie, marehemu Said Ngamba ‘Mzee Small’.

King Majuto alimuelezea ‘Mzee Small’ walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 1973, mtaa wa Moshi uliopo Ilala, jijini Dar es Salaam. Akielezea namna alivyolipata jina la ‘King Majuto’, alisema alipokuwa kwenye kundi la DDC Kibisa, aliigiza michezo mingi ambayo mwisho ilimalizika kwa ‘kujuta’. Watu kuamua kumpachika jina hilo ambalo limedumu hadi alipofariki dunia,

King Majuto wakati wa uhai wake alikuwa akikerwa mno kwa uzembe, Wasanii wavivu katika kazi ya sanaa, waliokuwa na kawaida ya kujivutavuta kufika ‘Lokesheni’. Hakusita kutamka msanii analiyekuwa akimvutia katika sanaa ya uigizaji, aliwataja waigizaji Jacob Stephen ‘JB’ na Brother K. wa kipindi cha ‘Futuhi’.

“Faida niliyokwishaipata kwenye uigizaji ni kusomesha watoto wake, kujenga nyumba tatu, kununua magari matano, kumiliki shamba na mifugo,” alitamka enzi za uhai wake.

Aidha King Majuto alikuwa akijivunia kuwaibua wasanii wengi katika maigizo. Faida nyingine alizozipata kutokana na uigizaji kuwa ni kuanzisha kundi lake binafsi liitwalo King’s Entertainment. Kundi hilo lenye wasanii 75, ambalo maskani yake yapo CCM Hall, jijini Tanga.

King Majuto alikuwa baba wa familia yenye watoto 12 ambao takriban wote ni waigizaji kama alivyo yeye, isipokuwa mtoto wake wa kwanza aitwaye Athuman aliyeamua kuingia kwenye muziki akipiga gitaa.

King Majuto alikuwa msanii huru tangu 1983, baada ya kupitia vikundi mbalimbali vya sanaa vya JKT, JWTZ, Zimamoto na Bandari. Alipoulizwa juu ya kugombea nafasi za kisiasa, King Majuto alisema kuwa hana ndoto za kuwa mwanasiasa, na ameahidi kubakia kuwa mwigizaji sababu kwa kuwa vitu hivyo haviingiliani.

Licha ya kazi yake hiyo, Majuto pia ni mkulima bora mwenye shamba kubwa la mbogamboga linalomfaa kwa matumizi ya nyumbani. Aidha anashamba maeneo ya Kiruku, mkoani Tanga, lenye mazo ya Mananasi, Machungwa, Mihogo, Minazi na Miembe ambayo yameanza kumletea faida. Mwili wa Amri Athuman ‘King Majuto’ uliwekwa kwenye nyumba yake ya milele kijijini kwake huko mkoani Tanga.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0767331200, 0713331200, 0736331200 na 0784331200

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...