Na Moshy Kiyungi
Wimbo wa ‘Arua’ aliouimba kwa ujasiri mkubwa Zahir Alli Zorro, ulimuongezea sifa nyingi mno Afrika ya Mashariki.
Katika wimbo huo Arua ulikuwa ukiwakaribisha mashujaa wetu waliokwenda mstari wa mbele kupigana vita na nduli Idd Amin wa Uganda.
Zahir wakati huo alikuwa mtunzi, mwimbaji mahiri na mwenye uwezo mkubwa wa kulicharaza gitaa la solo katika bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Wana ‘Kimulimuli’ iliyokuwa jijini Dar es Salaam.
Mwaka 1978 nchi yetu ilivamiwa na majeshi ya Uganda, nchi iliyokuwa ikiongozwa na Rais Idd Amin Dada.
Kitendo hicho kimfanya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Tanzania, ambaye pia alikuwa Rais, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuyaamrisha majeshi yetu kupigana vita, ambavyo hatimaye vilimuondoa madarakani Idd Amin.
Baadhi ya bendi za muziki humu nchini zilitunga nyimbo za kuyahamasisha nakupongeza majeshi yetu kwa ushindi.
Baada ya ushindi huo, mkoa wa Ziwa Magharibi au West Lake Region (kwa lugha ya Kiingereza) wakati huo, ukabadilishwa jina ukaitwa mkoa wa Kagera.
Historia ya Zahir Alli Zorro katika muziki inaonesha kuwa amechangia katika kunyanyua tasnia ya muziki wa Tanzania.
Zahir ni mmoja kati ya wanamuziki wakongwe aliyeingia kwenye gemu la muziki mwaka 1968 na hadi sasa anaendelea ‘kupeta’ kwenye tasnia hiyo.
Ni baba wa familiya ya mke na watoto wawili ambao nao ni wasanii Banana na dada yake Maunda Zorro.
Watoto hao wamedhihirisha usemi wa “mtoto wa nyoka ni nyoka”, hivi sasa wanatamba katika muziki wa kizazi kipya ‘Bongo Flava’.
Wasifu wake katika muziki alisema kuwa awali alijiunga na bendi ya muziki ya Super Vea chini ya Maestro Musama Andrew, baadaye akajiunga na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) na aliajiriwa katika kitengo cha OP TANU M19 mwaka 1973 hadi 1989.
Zorro alibainisha baadaye alijiunga na bendi ya Sambuluma, iliyokuwa ikiongozwa na Mbangu Nguza ‘Vicking’, ambako alitunga wimbo uliovuma sana kwa jina la Cleopatra mwaka 1991.
Safari ya muziki ya Zahir alimfikisha kupiga hodi katika bendi ya Washirika iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Watunjatanjata' mwaka 1992 hadi 1996.
Mkongwe huyo aliunda bendi yake ya Mass Media, ambayo haikudumu kwa kipindi kirefu, licha ya kuachia nyimbo kadhaa ambazo zilikuwa simulizi mitaani.
Zahir Ally Zorro alizaliwa Aprili 24, 1954 katika hospitali ya Ocean road jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa elimu, alisema kuwa alipata elimu ya awali katika shule ya Wazazi iliyokuwa inayoitwa TAPA mwaka 1959, iliyokuwa katika jengo la Taasisi, karibu kabisa na mnara wa Mwalimu Nyerere mjini Tabora.
Zahir alianza elimu ya msingi mjini humo ambako alihitimu masomo hayo mwaka 1968.
Baada ya masomo yake ya elimu ya msingi aliingia kwenye tasinia ya muziki, ambayo amedumu nayo hadi sasa.
Nguli huyo anao mpango wa kuwamwagia ujuzi wa muziki kwa vijana wa Tanzania, ambao watakuwa na ari ya kujifunza.
Zahir alisema mikakati yake kwa ujumla ni pamoja na kuirudisha bendi ya Mass media ambayo awali aliwahi kufanya nayo kazi kabla ya kuvunjika.
Lengo lake kubwa la kuirejesha bendi hiyo ni pamoja na kuanzisha kituo ili aweze kutoa elimu ya muziki aliyonayo kwa wanamuziki chipukizi wanaopenda kujifunza kazi hiyo.
Vilevile mkongwe huyo anakusudia kutunga nyimbo zake binafsi kwa kwa ajili ya kutoa albamu yake.
Zahir Alli alitamka kuwa licha ya mkakati huo, pia anatarajia kutoa kitabu kitakachoitwa SHADOUX ambacho kitachapichwa na Kampuni ya magazeti ya Global Publishers.
"Kazi ya kutunga nimekamilisha na kilichobakia kazi ya kuchapa ambapo kampuni ya Global ndio itafanya kazi hiyo," alisema Zorro.
Pamoja na mikakati hiyo alibainisha kuwa changamoto zinazowakabili ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kununulia vyombo vya muziki.
Zorro alisema kuwa kwa sasa vyombo vya muziki vipo vingi sana madukani hapa nchini lakini ukosefu wa fedha kwa ajili ya kununulia ndiyo tatizo kubwa.
Aidha alisema kuwa kuna utofauti kidogo na zamani ambapo fedha zilikuwepo lakini hakukuwa na vyombo vya muziki.
Zahir Alli Zorro nyimbo zake kamwe hazitachuja masikioni mwa wasikilizaji kwa kuwa zilikuwa na ujumbe madhubuti kwa jamii.
Baadhi ya nyimbo hizo za Tikisa, Cleopatra, Haifai Kabwe na Arua uliokuwa ukiwakaribisha mashujaa wetu waliokwenda mstari wa mbele kupigana vita na nduli Idd Amin wa Uganda.
Zahir bado yupo na wakati mwingine hushirikiana na mwanawe Banana anayemiliki bendi iitwayo B.Band.
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200, 0736331200 na 0713331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...