Na Moshy Kiyungi
Siku hazigandi ilikuwa wiki, miezi, miaka hadi zaidi ya miongo miwili imepita tangu Pepe Kalle alipofariki dunia!. Maradhi ya moyo ndiyo yaliyokatisha maisha ya nguli huyo Novemba 28, 1998 akiwa na umri wa miaka 47, itatimia miaka 21 tangu aiage dunia itakaofika Novemba 28, 2019.

Wasifu wa Pepe Kalle unaonesha kuwa alizaliwa Novemba 30, 1951 katika Jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, akapewa jina la Kabasele Yampanya. Ukiangalia mwezi aliozaliwa na ule aliofariki dunia ni uleule Novemba!

Sifa za mwanamuziki huyo ni kwamba wakati wa uhai wake alikuwa mtunzi, mwimbaji wa muziki wa soukous, pia aliongoza kundi la wanamuziki wa bendi ya Empire Bakuba, iliyokuwa maarufu nchini humo. Pepe Kalle lilikuwa na umbo kubwa lililokuwa na uzito wa Kilo 136 na urefu wake ulikuwa Sentimeta 190 ambazo ni sawa na futi sita na inchi tatu. Alijulikana kama ‘Tembo wa Afrika’

Sauti yake ilikuwa nyembamba na nyororo, mwenye uwezo mkubwa wa kughani, alikuwa mwepesi kunengua jukwaani licha ya umbo lake hilo. Watanzania wengi tutaendelea kumkumbuka mwanamuziki huyo hususan wakati alipokuja nchini mwetu, akatikisa majiji ya Arusha, Dar es Saalam na Mbeya.

Kwenye ziara hiyo Pepe Kalle alifuatana na wanamuziki akiwemo mipiga wa gitaa la besi Gode Lofombo na waimbaji akina Papy Tax na Dilu Dilumona. Aidha alifuatana na rapa wake mahiri na kiongozi wa wanenguaji Djouna Mombafu ‘Bileku Mpasi’ na mbilikimo wawili Emoro na Jolly Bebbe.

Kwa pamoja walitoa burudani za kutosha kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam mwaka 1991. Mwaka uliofuatia wa 1992, Emoro alifariki dunia akiwa na bendi yake nje ya nchi kwa safari za kikazi ya muziki. Historia yake katika muziki inaeleza kwamba alianza muziki rasmi kutunga na kuimba akiwa katika bendi ya African Jazz, iliyokuwa ikiongozwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’.

Grand Kalle, ndiye aliyemtengeneza vilivyo Pepe Kalle kimuziki, kuafuatia uzoefu wake mkubwa katika muziki. Baadhi ya watu wamekuwa wakichangaya majina yao, kwamba Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’ alikuwa baba wa Kabasele Yampanya Pepe Kalle’ Hao wote walikuwa ni wanamuziki mahiri wenye kupishana kwa mbali sana kwa umri.

Joseph Kabasele ‘Grand Kalle’ alizaliwa Desemba 16, 1930 mjini Matadi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kabasele Yampanya ‘Pepe Kalle’ alizaliwa Novemba 28, 1951 jijini Kinshasa. Baada ya kujiona kuwa amekomaa, akatimka na kwenda kujiunga na bendi ya Orchestra Lipua Lipua iliyokuwa ikifadhiliwa na Kiamunagana Mateta Wanzela Mbonga ‘Verckys’.

Verckys alikuwa akimiliki bendi ya Orchestra Veve, bendi za Lipua Lipua na Orchestra Kiam, alikuwa akizifadhili. Pepe Kalle akiwa na bendi hiyo hakuchukua kipindi kirefu akafanywa kuwa mwimbaji kiongozi, akishirikiana na mwimbaji mwingine Nyboma Mwandido. Pepe Kalla safari yake katika muziki haikuishia katika bendi ya Lipua Lipua, mwaka 1973 akiwa na Dilu Dilumona na Papy Tax waliondoka katika bendi hiyo wakaenda kuunda bendi yao iliyopewa jina la Empire Bakuba.

Jina la Empire Bakuba lilitokana na mashujaa wapiganaji wa makabila ya Kongo. Katika miaka hiyo ya 1970, Empire Bakuba na Zaiko Langa Langa ndizo zilikuwa zakiwika katika jiji la Kinshasa na kujizolea umaarufu mkubwa kwa wapenzi wa muziki wa rhumba. Vibao vya Dadou cha Pepe Kalle na Sango ya Mwa ya Papy Tex, iliiweka Empire Bakuba kwenye chati na ikaanzisha mtindo wa Kwasa kwasa.

Yalipofanyika maadhimisho ya miaka kumi ya bendi yao ya Empire Bakuba mwaka 1982, ilipigiwa kura na ikashinda kuwa bendi bora huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire). Miaka ya 1980 Bakuba ilijizolea wapenzi na washabiki lukuki. Pepe Kalle alikishirikiana na Nyboma Mwandido kurekodi wimbo wa Moyibi mwaka 1988. Wimbo huo uliiongezea bendi hiyo umaarufu katika nchi zinazozungumza lugha ya Kifaransa huko Afrika ya Kati na Magharibi.

Album ya Roger Milla iliyokuwa ikimuenzi na kumsifia mchezaji wa mpira wa miguu Roger Milla ambaye alichezea timu yake ya Taifa ya Cameroon, akiwa na umri mkubwa kuliko wote mwaka 1990. Miaka ya 1990 Pepe Kale alitoa album zingine za Gigant Afrique Larger than Life na Cocktail.

Nyimbo zingine zilikuwa za Hidaya, Sintia, Reovisie, Guy guy na Yanga Afrika. Aliachia vibao vya La- rhumba, Don’t Cry, Yaja, Zouke Zouke Nakutuna na Pon moun Paka Buoge. Bendi ya Empire Bakuba iliwahi kufanya ziara sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi yao. Kama wanamuziki wengine, Pepe Kalle naye ailiwashirikisha wanamuziki wengine wakongwe katika tasnia ya muziki akiwemo Simaro Lutumba na Nyoka Longo.

Watanzania tutaendelea kumukumbuka Pepe Kalle ambaye alipotua Tanzania, ilitunga nyimbo kupitia lugha ya Kiswahili, za Yanga Afrika, akisifia Klabu ya Yanga iliyokuwa ikimtaja mfadhili wa klabu hiyo Abbas Gulamali, Hidaya, wimbo alioimba akilalamika kupoteza mkanda wake wa kiuno na mpenzi Bupe, aliutunga alipotoka jijini la Mbeya kufanya onyesho.

Wakati wa uhai wake Pepe Kalle alirekodi nyimbo zaidi wa 300 na kufyautua album 20 katika miongo miwili ya muziki wake. Bendi ya Empire Bakuba baada ya kifo cha kiongoizi wake Pepe Kalle kufariki dunia, haisikiki tene licha ya wanamuziki wake kuwapo.

Djouna Mombafu ‘Bileku Mpasi’ ndiye pekee aliyejikwamua kwa kuunda bendi yake ya Orchestra Big One. Hivi sasa ni gumzo katika jiji la Kinshasa, wakitamba na albamu ya Tonnerre de Brest yenye kibao kikali cha ‘6600 Volts’. Bileku Mpasi akiwa na kundi hilo, amefanikiwa kufyatua albam nyingi kwa kipindi kifupi zilizopelekea kupata mialiko lukuki nje ya nchi yao hususan za Ulaya.

Amekuwa kivutio akionekana kwenye video zake nyingi kwa kuimba na kucheza akishirikiana na wanenguaji mbirikimo, Djuma Fatembo na mwanadada Jolly Bebe. Baadhi ya album alizoachia mwanamuziki huyo ni pamoja na Moun Baka Bouger, Karachiga, Tatou, Djouna Big One 6600Volts, Cupidon Brise , Tonnere de Best Onze na nyingine nyingi.

Ikumbukwe kwamba hapa nchini msanii aliyejulikana kwa jina la Kokoriko, aliweza kuiga miondoko ya uchezaji na uvaaji wa Bileku Mpasi, akapachikwa jina la Bileku Mpasi wa Tanzania.

Mungu aiweke roho yake pahala pema peponi, Amina.

Mwandishi wa makal hii anapatikana kwa namba: 0784331200, 0767331200, 07361331200 na 0713331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...