TAMASHA la 11 la muziki wa Cigogo linaanza kurindima leo kwenye
viwanja vya Chamwino Ikulu jijini Dodoma ikiwa ni muendelezo wa kukuza
na kuendeleza sanaa ya Tanzania.
Tamasha hilo linaanza leo kwa makundi mbalimbali ya ngoma za asili
yakitoa elimu kwa jamii kupitia nyimbo zao huku kesho ndio uzinduzi
rasmi ambao, mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye ulemavu
Anthony Mavunde.
Mavunde katika tamasha hilo ataongozana na watendaji wengine wa ofisi
za serikali wanaotumikia Sanaa, lengo likiwa ni kufikisha ujumbe wa
jamii kupitia wasanii.
Kwa kuwa tamasha la Cigogo ni mojawapo ya sehemu ambayo inabeba urithi
wa utamaduni wa mtanzania kwa sababu ya kukusanya idadi kubwa ya wadau
wa sanaa, watanzania wanakaribishwa kwa wingi kujipatia ujumbe ambao
ni sehemu ya elimu.
Ingawa hivi sasa Tanzania kuna utitiri wa matamasha lakini umuhimu wa
tamasha hilo ni wa kupigiwa mfano kutokana na shughuli zinazofanyika
kwenye wiki ya tukio hilo.
Kwani mshindo wa tamasha hilo umefika mbali zaidi ambao umevuka mipaka
ya nchi na kutokomea katika mabara ya Ulaya, Amerika na Asia ambayo
huchota busara na urithi wa sanaa za Tanzania.
Yaliyomo ndani ya tamasha hilo ni kiota ambacho kimebeba dhamira na
taratibu nzima za sanaa kwa sababu anayelisimamia tamasha hilo ni
mwanazuoni mbobevu anayefanya kazi hizo na kuzifundisha ikiwa ni eneo
la elimu, burudani na taratibu nyingine ambazo ni sehemu ya jamii.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa tamasha hilo Dk Kedmon Mapana vumbi
limeanza kufuka leo katika viwanja vya Chamwino lilipo lango la
kuingilia Ikulu ambalo litafikia tamati Jumapili.
Anasema tamasha hilo lililoasisiwa mwaka 2005 kijijini hapo na Kituo
cha Sanaa cha Chamwino (CAC) kwa lengo la kuenzi na kuuendeleza muziki
wa asili ya Kigogo.
Dk Mapana anasema ubora wake umezidi kukua kwa sababu ya matukio
ambayo yanaendana na kasi ya maendeleo ya sanaa duniani.
Mapana anasema kadri siku zinavyokwenda mbele ndivyo linavyozidi
kupiga hatua kwa matukio ambayo ni sehemu ya maendeleo ya sanaa.
“Kwa kuwa sanaa ni eneo ambalo ninaishi, kila mwaka matukio
yanabadilika kuendana na wakati, hivyo ni nafasi ya mashabiki wa sanaa
na utamaduni kujitokeza kwa wingi kujionea jinsi makundi ya sanaa
yanavyoendeleza utamaduni wa mtanzania,” alisema Dk Mapana.
Dk Mapana ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Sanaa za Ubunifu Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam (UDSM) anasema kutakuwa na matukio mbalimbali ambayo
ni njia ya kufikia malengo yanayokusudiwa.
Anasema katika makundi shiriki huwa wanapewa nafasi ya kuibua vionjo
vya asili kama vile aina ya ngoma, uchezaji wake na hata maleba.
Makundi shiriki
Anasema tamasha la mwaka huu linatarajia kushirikisha makundi 31 ya
hapa nchini ambayo yatabadilishana utamaduni.
Ingawa kutakuwa na wadau zaidi ya 20 kutoka nje ya Tanzania ambao
wanakuja kujifunza na kushuhudia utamaduni wa Mtanzania kupitia
tamasha hilo.
Anaweka bayana wadau hao kutoka nje ya Tanzania ni Afrika Kusini (4),
Bulgaria (4) Amerika (4), Argentina (2) na Thailand (15) na Uganda
(1).
Dk. Mapana anasema wafadhili wakubwa wa tamasha la Muziki wa Cigogo ni
wasanii wenyewe ambao huwa wanajitoa kwa asilimia kubwa. Tamasha hilo
limejijenga kutokuwa tegemezi, yaani hatusubiri wafadhili kuuenzi
utamaduni wetu kwani hatusubiri tulipwe pesa.
“Sasa ukionyesha ulichonacho huwezi jua nani atakipenda na atakinunua
kwa gharama gani, lakini pia Tamasha hili limejikika katika kufundisha
watoto na vijana kuendelea kutambua mila na desturi zao,” alisema.
Kazi kubwa ya Kituo cha Utamaduni Chamwino ni kutafuta fedha ya
kuhakikisha wasanii wanakula vizuri.
Anaweka bayana wafadhili wengine wa tamasha hilo ni serikali ya kijiji
cha Chamwino ambacho kinatoa maeneo ya kufanyia tamasha hilo bila
gharama yoyote pamoja na Shirika lisilo la Kiserikali la Chamwino
Connect lililoko Marekani.
Anasema katika makundi shiriki huwa wanapewa nafasi ya kuibua vionjo
vya asili kama vile aina ya ngoma, uchezaji wake,na hata maleba.
Kutolewa semina mbalimbali
Mojawapo ya matukio yatakayofanikisha tamasha la 11 ni semina
mbalimbali zitakazotolewa na serikali kwa maeneo kama Baraza la Sanaa
la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu, Chama cha Hakimiliki Tanzania
(COSOTA), Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Dk Mapana anasema semina hizo si mara ya kwanza kufanyika tangu
kuasisiwa kwa tamasha hilo ambalo linazidi kukua kadri siku
zinavyokwenda mbele.
Msanii Dito ndani ya nyumba
Anasema kama ilivyokuwa mwaka jana, msanii wa muziki wa kizazi kipya,
Lameck Dito ni mmoja wa wasanii washereheshaji wa tamasha la 11.
Ditto kwenye tamasha hilo akiiwakilisha taasisi ya Tulia Trust ukiwa
ni ushirikiano kati ya CAC na taasisi ya Tulia.
Wanafunzi UDSM kujifunza zaidi
Dk Mapana anasema kama ilivyo ada ya tamasha hilo, wanafunzi wa sanaa
wa UDSM hupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo uandaaji wa Filamu
(Film Documentary), namna ya kuandaa matamasha na matukio mengine ya
sanaa.
“Huwa tunalitumia tamasha la Chamwino kama sehemu ya wanafunzi wetu
kujifunza kwa vitendo yale ambayo tunayowafundisha darasani,” alisema
Dk Mapana.
Kubwa zaidi katika tamasha
Dk Mapana anasema katika tamasha la mwaka huu kutakuwa na mchezo wa
kuigiza ulioongozwa na wataalam kutoka Bulgaria ambao utachezwa na
wanafunzi wa Shule ya Msingi Chamwino.
Anasema malengo makubwa ya mchezo huo ni kuibua na kuendeleza vipaji
kwa watoto ukiwa ni mpango wa CAC.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Suzan Mlawi akiwasilisha neno kwenye tamasha la kwa jana, kulia kwake ni Dk MapanaKatibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Suzan Mlawi akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa sanaa wa kada mbalimbali.
Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza na Dk Mapana wakicheza ngoma na kikundi cha watoto cha Ndagwa
Katibu wa Basata Godfrey Mngereza akipigamarimba kwenye tamasha la Cigogo 2018
Kundi la Iman Membe likitoa burudani kwenye tamasha la mwaka jana
Wakiserebuka tamashani
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...