Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (mwenye miwani) na Ujumbe wake, akizungumza na mwakilishi wa Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoani Kagera, Justin Mrenga (kulia), alipotembelea Taasisi hiyo kukagua uunganishwaji wa umeme, akiwa katika ziara ya kazi, Julai 17, 2019.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia), akimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti lengo la ziara yake mkoani humo, Julai 17, 2019.
********************
Na Veronica Simba – Kagera.
Serikali imetoa agizo kwa mameneja
wote wa mikoa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha
viwanda vyote nchini vinafungiwa Transfoma mahsusi kwa matumizi ya
viwanda pekee pasipo kuchanganya na matumizi ya wananchi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alitoa agizo hilo jana, Julai 17, 2019 akiwa katika ziara ya kazi mkoani Kagera.Akizungumza na Uongozi wa Shirika
la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), mkoani humo, mara baada ya kukagua
Transfoma mpya iliyofungwa maalumu kwa matumizi ya Shirika hilo; Dkt.
Kalemani alisema hatua hiyo itasaidia kuboresha upatikanaji wa umeme wa
uhakika kwa viwanda hivyo kuviwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Wenye viwanda wawe na Transfoma
zao, wasichangie matumizi na wananchi. Mwananchi akiunguza kwake
anaathiri Kiwanda pia maana umeme utakosekana kote hivyo uzalishaji
unasimama. Haifai.”Vilevile, Waziri aliwaagiza
mameneja hao nchi nzima kuhakikisha wanabadilisha miundombinu yote ya
umeme ambayo ni mibovu katika maeneo yao mathalani Transfoma, Nguzo,
Nyaya na Mita ili kuwaondolea wananchi kero za kukatika kwa umeme mara
kwa mara.
“Meneja yeyote ambaye eneo lake
litabainika kuwa na Transfoma iliyoungua au kuharibika kwa kipindi cha
zaidi ya mwezi mmoja na hajafanya jitihada yoyote kutatua, Mkurugenzi
Mtendaji mchukulie hatua maana ni hasara kwa Shirika,” aliagiza Waziri.
Akifafanua zaidi, alisema
miundombinu iliyoharibika isiporekebishwa kwa wakati, husababisha
Shirika kupoteza mapato hivyo kuitia hasara Serikali.
Akisisitiza kuhusu agizo hilo,
Waziri Kalemani alibainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati,
imetenga fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo na urekebishaji wa
miundombinu mbalimbali ya umeme kwa maeneo yote nchini, hivyo hakuna
sababu ya kusuasua katika kutekeleza zoezi hilo.
“Mathalani, kwa Mkoa huu wa
Kagera, tumetenga jumla ya shilingi bilioni 9.2 kwa mwaka huu kwa ajili
ya matengenezo ya miundombinu ya umeme,” alibainisha.
Katika ziara hiyo, Waziri
alitembelea na kukagua uunganishwaji umeme katika Taasisi ya SIDO eneo
la Rwamishenye na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) Tawi la
Bulugo wilayani Bukoba, ambapo alikiri kufurahishwa na utekelezaji wa
maagizo aliyoyatoa awali kwa uongozi wa TANESCO, kuzifungia Taasisi hizo
Transfoma.Waziri aliambatana na viongozi pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Wizarani, TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...