Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
IDADI ya watu waliofariki kutokana na janga la moto lililotokea mkoani Morogoro Agosti 10, 2019 baada ya roli la mafuta kulipuka wamefikia 101 huku wengine wakiendelea kupata matibabu pamoja na kufanya mazoezi ya kusimama na kutembea.
Akizungumza leo Agosti 23,2019 jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha amesema kuwa majeruhi mmoja katika ajali hiyo ya moto amefariki dunia alfajiri ya leo.
" Hospitali ya Taifa Muhimbili tulikuwa tumebaki na majeruhi 15, kwa bahati mbaya leo alfajiri ya saa 12:30 majeruhi mmoja mwanaume, Sadick Ismail Mganga amefariki dunia na kufanya idadi ya majeruhi waliobaki hospitalini hapo kufikia 14," ameeleza Aminiel.
Aidha amesema kuwa kati ya majeruhi 14, majeruhi 11 bado wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na wagonjwa watatu wapo wodi namba 22 Sewahaji na wanaendelea na vizuri na matibabu pamoja na mazoezi ya kusimama na kutembea.
Pia amesema kuwa maiti zote zimesafirishwa mkoani Morogoro kwa mujibu wa taratibu zilizopangwa na kuongeza kuwa vifaa na wataalamu wapo wanaendelea kupigania maisha ya wagonjwa hao.
Tunaomba pia tuishukuru Serikali na wadau mbalimbali kwa kushirikiana na hospitali ya Taifa Muhimbili katika kuhakikisha wagonjwa wetu hawa na wengine waliopo hospitalini hapo wanapata huduma stahiki,"amesema.
Ikumbukwe kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipokea majeruhi 47 kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro na kwa bahati mbaya majeruhi 33 wamefariki dunia hadi sasa na kufanya idadi ya majeruhi waliobaki kuwa 14.
Ofisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Aminiel Aligaesha
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...