*Pia yaeleza inavyoshirikiana na nchi za jumuiya hiyo kukomesha dawa za kulevya

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imempongeza Rais Dk.John Magufuli kwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Mbali ya kumpongeza Rais Magufuli, pia Mamlaka hiyo imefafanua kwa kina inavyoshirikiana na nchi za SADC kukomesha biashara ya dawa za kulevya na wanavyosaidiana katika kutoa kinga na tiba kwa walioathirika na dawa hizo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Michuzi Blog na Michuzi TV, Kamishina wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti  Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Dkt. Peter Mfisi ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa SADC.

"Kabla ya haya mahojiano yetu,sote tunatambua nchi yetu imetoka kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 39 wa SADC.Hivyo nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wetu kuwa Mwenyekiti wa SADC.

"Rais wetu ni kiongozi makini na ukweli usio na mashaka nchi za jumuiya ya SADC zitakwenda kule ambako wakuu wa nchi hizo wanataka iende kwa manufaa ya wananchi wote,"amesema Dkt.Mfisi.

Kuhusu ushirikiano kwa nchi za SADC , amesema Tanzania kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekuwa ikishirikiana kwa karibu na nchi za jumuiya hiyo kukomesha biashara ya dawa za kulevya.

"Tumekuwa na ushirikiano mzuri na nchi nyingine za SADC katika kukabiliana na dawa za kulevya, hivyo tumekuwa tukipeana taarifa za kiintelijensia na kuzifanyia kazi,"amesema Dkt.Mfisi.

Akifafanua zaidi katika eneo hilo la ushirikiano na nchi nyingine za SADC, amesema baada ya Mamlaka hiyo kufanikiwa kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa dawa za kulevya na kuwepo kwa sheria kali, wanaojihusisha na biashara hiyo wameona kwa Tanzania biashara imekuwa ngumu, hivyo wanatumia nchi nyingine kupitisha dawa hizo.

Amesema baada ya Mamlaka hiyo kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa dawa hizo nchini katika viwanja vya ndege na Bahari ya Hindi, wanaojihusisha nayo wanatumia nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Malawi na Zambia kuingiza dawa nchini Tanzania.

"Baada ya kuanzishwa mamlaka hii kumekuwa na sheria kali za kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya, hivyo wachache wanaojihusisha nayo wamekimbia nchini na hata wanaoendelea kuifanya wanatumia nchi za Msumbiji na Afrika Kusini.

"Zikishaingia kwenye nchi hizo sasa ndio wanajaribu kutaka kuziingiza nchini kwa kutumia mipaka ya Msumbiji, Zambia na Malawi ambako nako tumeweka mfumo mzuri wa kudhibiti,"amesema Dk.Mfisi.

Kamishna huyo wa Kinga na Tiba amesema katika kuhakikisha wanashirikiana kukabiliana na dawa za kulevya kwa nchi za jumuiya hiyo tayari Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini kupitia mawaziri husika wameweka mkakati kuanzisha chombo maalumu cha kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya.

"Ofisi za chombo hicho zitakuwa Msumbiji na 

kila nchi itahusika kuchangia gharama za kukiendesha na wenzetu wa UN-ODC, Umoja wa Ulaya na DA ambacho ni chombo cha kupambana na dawa za kulevya nchini Marekani wameahidi kutusaidia,"amesema Dk.Mfisi.

Kuhusu eneo la tiba na kinga , amesema wamekuwa wakishirikiana vizuri."Tunashirikiana vizuri kwenye eneo la tiba na kinga na mamlaka yetu imekuwa ya mfano kwa nchi nyingine za jumuiya hiyo.Pia tumekuwa tukishirikiana na nchi za Kenya na Uganda ambazo hazipo SADC".

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...