Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika halmashauri ya Mji Geita.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara mkoani Geita ambapo amesema fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu nchini.

Ole Nasha amesema serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwajengea fursa na mazingira mazuri ya kusoma watoto wenye mahitaji maalum na ndio maana imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vitabu ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.

“Kwa miaka mingi jamii nyingi zimekuwa zikiwatenga watoto wenye mahitaji maalim, lakini kwa sasa nashukuru tumeendelea kuwawezesha kupata haki yao ya Elimu kama walivyo watoto wengine na kwamba wanaweza kuwa na changamoto za kimaumbile lakini ubinadamu wao upo palepale amesema Waziri Ole Nasha.

Amewataka wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kutokatishwa tamaa na changamoto walizonazo za kimaumbile kwani serikali imewawekea mazingira ya kuwawezesha kufika mbali zaidi katika Elimu na kuwataka kuendelea kutumia fursa hizo za kielimu ili kutengeneza maisha yao ya baadaye.

"Wanafunzi, mtu hawezi kujua kipaji chako ni kipi lakini serikali inakupa fursa ya kuonyesha kipaji chako, Mhe Rais ametambua uwezo mkubwa wa watu wenye mahitaji maalum na ndio maana siku hizi tunae Naibu Waziri anayeshughulika na watu wenye mahitaji maalum ambaye naye ana changmoto ya ulemavu," amesema Naibu Waziri.

Awali Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Mbugani Edwicka Ndunguru amemweleza Naibu Waziri kuwa kituo hicho kilijengwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata haki ya kielimu katika mazingira wezeshi na kuwapa fursa wengi zaidi wenye mahitaji maalum wanaoishi mbali na shule zinazotoa elimu maalum kupata elimu.

Amesema mafanikio ya kuwepo kwa vituo vya watoto wenye mahitaji maalum mbali na kuwawezesha kupata haki yao ya kielimu, pia imewasaidia kujifunza ujuzi mbalimbali, jamii imetambua nakuthamini umuhimu wa wanafunzi wenye mahitaji maaluma kupata Elimu na wengine kufanikiwa kupata kazi katika maeneo mbalimbali.

Wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapomaliza hapa wanakua na ujuzi katika fani za ushonaji, ufumaji na useremala, fani hizi zimewezesha baadhi kuajiriwa katika maeneo mbalimbali na wengine kujiajiri amesemu mwalimu Ndunguru. 

Kituo hicho chenye vitengo vinne vyenye jumla ya wanafunzi 143 ambavyo ni vitengo vya ulemavu wa akili, Viziwi, ulemavu wa viungo na ulemavu wa macho, mbali ya kuhudumia wanafunzi hao wenye uwezo wa kufika shuleni lakini pia vinahudumia watoto 38 wenye ulemavu wa kiwango cha juu ambao hawawezi kufika shuleni.
 Sehemu ya bweni lilojengwa na serikali katika Kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita Mkoani Geita
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa bweni la watoto wenye mahitaji maalum katika kituo Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.
Baadhi ya wanafunzi wa kituo cha Elimu Maalum katika shule ya msingi Mbugani wakicheza ngoma mbele ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha aliyefanya ziara katika kituo hicho kukagua maendeleo ya ujenzi wa bweni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na watoto wenye mahitaji maalum (Hawapo Pichani)  baada ya kukagua ujenzi wa bweni la Kituo cha Watoto wenye mahitaji Maalum cha Shule ya msingi Mbugani iliyopo mkoani Geita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...