Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa Dickson Mkasanga akizungumza na wanafunzi wa kozi ya ufundi wa simu za mkononi wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo katika chuo cha VETA Kipawa.
Mratibu wa kozi ya Ufundi wa Simu za Mkononi Ricky Sambo akitoa maelezo kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa kozi hiyo.


Picha ya pamoja.

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA Kipawa imeanza kutoa mafunzo ya Ufundi wa Simu za Mkononi kwa lengo la kuandaa mafundi bora wa simu za mkononi nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo Agosti 26, 2019, Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Kipawa Dickson Mkasanga alisema mafunzo hayo yanalenga kuandaa mafundi wa simu za mkononi wenye ujuzi na  weledi watakaofanya kazi zao kwa mujibu wa sheria na kutoa huduma zenye viwango na ubora.

Alisema mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambapo wahitimu wa kozi hiyo watapatiwa vyeti vitakavyowawezesha kusajiliwa na kupewa leseni ya kufanya kazi za ufundi wa simu za mkononi inayotolewa na TCRA.

Alisema chuo chake pamoja na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) zilishirikishwa na TCRA kubaini uhitaji wa kozi hiyo, umahiri wa mafundi wanaohitajika sokoni na kutengeneza mtaala kwa ushirikiano na wadau mbalimbali na kwamba chuo chake kimejipanga kutoa mafunzo hayo kwa kiwango cha juu.

“Chuo hiki kitatumia rasilimali zake za kisasa na utaalamu wa walimu wake ili kuhakikisha mafunzo haya yanatolewa kwa umahiri na weledi wa hali ya juu”.Alisema

Aliwasihi wanafunzi wa kozi hiyo kuonesha ushirikiano na kufuata taratibu za mafunzo katika hatua zote ili kuwawezesha kupata ujuzi uliokusudiwa na kuwa mahiri katika kutoa huduma za ufundi wa simu za Mkononi.

Naye Mratibu wa kozi hiyo Ricky Sambo alisema mafunzo hayo yamepangwa kutolewa kwa ngazi tatu ambazo ni kozi ya ufundi simu ngazi ya awali,ngazi ya kati na ngazi ya juu.

Kwa mujibu wa Sambo, TCRA imetoa ufadhili wa ada kwa wanafunzi 60  kusoma kozi ya awali huku VETA ikitoa waalimu na vifaa vya kuendesha kozi hiyo.

Desemba 2018, Serikali iliagiza kusajiliwa na kupatiwa leseni kwa mafundi wanaotoa huduma za matengenezo ya simu za mkononi ili kuhakikisha huduma wanazozitoa kwa wananchi zinakuwa na viwango stahiki.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...