NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Simiyu
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), hivi karibuni uko mbioni, kuanzisha
mfumo wa waajiri na wafanyakazi kuwasilisha madai ya Fidia kwa njia ya mtandao,
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo Bw. Anselim Peter ameyasema hayo jana
kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika kitaifa kwenye viwanja
vya Nyakabindi nje kidogo ya mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Bw.Peter alisema lengo la kuanzisha mfumo huo ni kusogeza karibu
huduma za Mfuko kwa wateja wadau wake na hivyo kurahisisha upatikanaji wa
huduma.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unashiriki katika maonesho ya
Nanenane kwa lengo la kupata fursa ya kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi
kuhusu shughuli za Mfuko ambazo ni kulipa Fidia, utaratibu gani wa kufuata ili
kuwasilisha madai kabla ya kulipwa Fidia.
"Pia katika banda la WCF hapa Nyakabindi, wataalamu wetu
watatoa elimu kuhusu Mfuko, kusajiliwa, kuwafahamisha taratibu za michango,
kuwafahamisha taratibu za madai ya fidia na pia kupokea maoni ya wadau kuhusu
Mfuko. Lakini pia tunatoa huduma kwa vitendo jinsi wanavyoweza kufanya kazi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wafanyakazi wake kwenye orodha
iliyoko WCF, kuprinti cheti, na pia kulipa michango ofisini kwako.” Alifafanua
Bw. Peter.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka,
ameupongeza Mfuko huo kutokana na ushiriki wake katika mpango wa Mkoa kujenga
kiwanda cha kutengenza vifaa tiba Huu ni utekelezaji kwa vitendo azma ya
Serikali ya Awamu ya Tano katika kuanzisha na kuimarisha viwanda ambavyo
vitaipeleka nchi kafika uchumi wa Kati.
"Nishukuru na kutambua mchango mkubwa wa Mkurugenzi Mkuu wa
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi Bw. Masha Mshomba na WCF kwa ujumla kwa sababu
ni partner (Mshirika) Mkubwa kwenye mipango yetu ya ujenzi wa kiwanda cha Vifaa
tiba." Alisema Mhe. Mtaka.
Alisema uongozi wa Mkoa walishirikiana na WCF katika hatua
mbalimbali za kushirikiana katika ujenzi wa kiwanda hicho ambapo tayari site
clearance imeshafanyika na kwamba hivi sasa wizara iko katika nafasi
nzuri ya kutangaza zabuni ili kumpata mkandarasi atakayejenga kiwanda hicho.
"Kwetu sisi kama mkoa WCF imetoa ushirikiano mkubwa katika
mipango yetu ya kushiriki katika uchumi wa viwanda wametoa ushirikiano
mkubwa." Alisema Mkuu wa Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka (watatu kushoto), akizungumza jambo mbele ya Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Anselim Peter (katikati) na Mussa Mwambujule, Afisa Matekelezo Mwandamizi wa Mfuko, wakati alipotembelea banda la WCF kwenye maonesho ya Nanenane viwanja vya Nyakabindi Simiyu
Afisa Uhusiano Mwandamizi WCF, Bw. Sebera Fulgence (kulia) akitoa elimu ya Fidia kwa wafanyakazi
Mussa Mwambujule, Afisa Matekelezo Mwandamizi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), akitoa elimu hiyo.
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter, akisalimiana na mama huyu aliyefika banda la WCF kupata elimu ya Fidia kwa wafanyakazi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...