Charles James, Michuzi TV

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU wilayani humo kufanya uchunguzi kwenye miradi miwili ya Soko la Mazao lililopo Kata ya Mkoka na Mnada wa Mifugo uliopo Kijiji cha Mbande.

DC Ndejembi ametoa maagizo hayo wakati alipofanya ziara ya kutembelea miradi hiyo akiambatana na Wawakilishi kutoka Ubalozi wa Denmark ambao wanashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kupitia mradi wa 'Local Investment Climate' kujenga miradi hiyo.

Amesema muonekano wa miradi hiyo haiendani na kiasi kilichotumika kuijenga hivyo ni vema TAKUKURU wafanye uchunguzi ili kuweza kujiridhisha.

" Tumefanya ziara kwenye hii miradi ambayo tunaijenga kwa kushirikiana na LIC ambayo iko chini ya Ubalozi wa Denmark lakini sijaridhishwa hata kidogo na thamani ya fedha kwenye haya majengo, ukiangalia muonekano wa hii miradi na kiasi kilichotumika unaona kabisa kuna walakini hapa.

" Huu mnada tumeambiwa thamani yake ni Shilingi Milioni 56, Hapa Soko hili mpaka sasa wameshatumia zaidi ya Milioni 200 lakini kinachoonekana hakiendani na thamani ya fedha hata kidogo. Hivyo niwatake TAKUKURU kuchunguza mara moja miradi hii na waniletee ripoti ili tuweze kuchukua hatua.

DC Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya tano haiwezi kukubali kufumbia macho kasoro zozote ambazo wataziona kwenye miradi ambayo inatekelezwa na wao kama wasaidizi wa Rais Magufuli watahakikisha wanasimamia kwa nguvu uadilifu katika kazi bila kumuonea mtu.

Aidha katika ziara hiyo DC Ndejembi pia ameiomba Taasisi ya LIC kutoa sapoti yao kwenye mradi wa Kiwanda cha Maziwa ambacho kinajengwa wilayani hapo ili kiweze kukamilika ambapo anaamini kitatoa ajira nyingi kwa vijana pamoja na kuongeza mapato lakini pia kitaitangaza Wilaya hiyo.

" Niwashukuru ndugu zetu wa LIC mmekua mkishirikiana sisi kwenye miradi ya maendeleo, niwaombe pia muweze kutusaidia kukamilisha kiwanda hiki ambacho naamini kitaongeza mapato kwenye Wilaya yetu, kitapunguza changamoto ya ajira lakini tutakua tumemuunga mkono Rais Dk John Magufuli katika kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia Sera yake ya viwanda," Amesema DC Ndejembi.

Kwa upande wake Mkuu wa Maendeleo ya Biashara kutoka Ubalozi wa Denmark, Jema Ngwale amempongeza DC Ndejembi kwa hatua aliyoichukua ya kuagiza TAKUKURU kuchunguza miradi hiyo ili kuweza kujiridhisha na kiasi kilichotumika.

" Sisi tutaendelea kushirikiana na Wilaya ya Kongwa katika kuwaletea miradi wananchi, Kuhusu sapoti yetu kwenye kiwanda cha maziwa jambo hilo tumelichukua na tukuahidi Mhe DC tutalifanyia kazi," Amesema Jema.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi akizungumza na Wawakilishi wa Balozi wa Denmark waliofika ofisini kwake ambapo walifanya mazungumzo na kukagua miradi inayojengwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa na Ubalozi huo.
 Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi akizungumza na watumishi kutoka Halmashauri ya Wilaya hiyo pamoja na Wawakilishi kutoka Ubalozi wa Denmark wakati wa ziara ya kukagua miradi inayojengwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Kongwa na Ubalozi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe Deo Ndejembi akikagua ujenzi wa Mradi wa Soko la Mazao lililopo katika Kata ya Mkoka wilayani humo

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...