Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akimkaribisha mwanachama mpya wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), Dkt. Khatibu Kazungu wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa chama hicho, jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akipokea hati kutoka kwa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Joseph Kamonga wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), jijini Dodoma.



Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akizindua hafla ya ugawaji hati za viwanja kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) jijini Dodoma ambapo aliziagiza Taasisi zote za Fedha nchini kuangalia namna bora ya ukokotoaji wa riba za mikopo.


Baadhi ya wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) (hayupo pichani) wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), Bw. Aliko Mwaiteleke wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa chama hicho, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) akionesha hati yake ya kiwanja baada ya kukabidhiwa hati hiyo katika hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), jijini Dodoma ambapo aliiagiza Benki Kuu ya Tanzania kufanya utafiti wa riba zinazotozwa na Taasisi za Fedha nchini.


Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatib Kazungu akipokea hati ya kiwanja kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye ni mlezi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), kutoka kwa mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Joseph Kamonga wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa chama hicho, jijini Dodoma.


Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isidor Mpango (Mb) (pili kushoto) akiwaongoza meza kuu katika picha ya pamoja na watendaji wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) wakati wa hafla ya ugawaji hati za viwanja vya Ihumwa Ngaloni kwa wanachama wa chama hicho, jijini Dodoma.



(Picha na Josephine Majura, WFM, Dodoma)

…………………….

Na. Josephine Majura na Farida Ramadhani

Serikali imeitaka Benki Kuu ya Tanzania- BOT kufanya utafiti wa Taasisi za kifedha hasa taasisi ndogo nchini kuona kama kweli riba wanazotoa kwa wateja wao zina sababu ya msingi au zinatolewa kwa riba kubwa kwa kujilimbikizia faida kubwa na kuwaumiza wateja, wakiwemo wajasiriamali na watumishi hasa wa kada ya chini.

Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua hafla ya kugawa Hati za viwanja kwa wanachama wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo- Hazina Saccos.

Dkt. Mpango amezitaka Benki na taasisi ndogo za fedha nchini kuangalia upya namna ya ukokotoaji wa riba kwa kuwa zinawaumiza wananchi wakiwemo wajasiriamali na watumishi ambao wanazitegemea katika kupata mitaji yao.

“Kuna Taasisi moja ambayo inakopesha fedha kwa watumishi wa Serikali akiwemo Walimu, kwa riba ya asilimia 32 ilihali wao wanachukua mikopo Benki kwa asilimia 20 ni hatari kweli, asilimia 32 ni riba kubwa mno”, alisisitiza Dkt. Mpango

Alisema kuwa mchango wa SACCOS unatambulika kama nyenzo muhimu ya kupunguza umasikini, ndio maana Serikali imetunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha kwa ajili ya kuzisimamia taasisi ndogo za fedha ili kuwapunguzia adha wafanyakazi na wajasiriamali wanaokopa fedha katika taasisi hizo kwa riba kubwa na masharti ya kinyonyaji.

Dkt. Mpango aliwasihi viongozi wa SACCOS zote nchini kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, weledi na kutumia maarifa ili kufanikisha ndoto za wanachama wao kwa kuwa SACCOS ndio kimbilio kwa watumishi wengi hasa wa kada za chini.

Alisema kuwa kunachangamoto ya ubadhilifu katika SACCOS nyingi nchini, jambo ambalo asingependa kulisikia kwa Hazina Saccos ambayo yeye pia ni mwanachama, hivyo ameitaka Saccos hiyo pamoja na nyingine kujitahidi kuweka mifumo imara ambayo itawezesha kutambua upotevu wa mali za Saccos ili kuweza kudhibiti mapema kabla ya madhara makubwa kujitokeza.

Waziri huyo amewataka wanachama wa Hazina Saccos kuchangamkia fursa za kiuchumi na zingine zilizopo katika Jiji la Dodoma kwa manufaa binafsi na taifa kwa ujumla.

Aidha ameitaka Saccos hiyo kuendelea kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wanachama na atafurahi iwapo Hazina Saccos itakuwa mfano kwa Saccos nyingine katika uadilifu na kujali masilahi mapana ya wanachama wake ili kuchochea shughuli za maendeleo zenye tija kwa taifa.

Amewataka Wanachama wa vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo kuacha tabia ya kutorudisha mikopo kwa wakati kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo ya Saccos.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS), Bw. Aliko Mwaiteleke, alimuomba Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) aweze kukisaidia chama hicho kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo suala la mipaka ya eneo walilonunua ambako miundombinu ya reli ya kati imepita.



Alisema katika eneo walilonunua kuna sehemu ambayo imeingia katika mradi wa reli ya kati lakini bado hawajaoneshwa mpaka wa wapi mradi huo unaishia ili kuwawezesha wamiliki wa eneo hilo kuanza kuliendeleza.



Pia Bw. Mwaiteleke alimuomba Dkt. Mpango, akiunganishe chama hicho na vyanzo vya fedha ili kiweze kupata mikopo nafuu kwa maendeleo ya chama na wanachama kwa ujumla.





Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina (Hazina SACCOS) kilianzishwa mwaka 1972 kikiwa na wanachama 100 na kusajiliwa kisheria mwaka 1973. Kwa sasa kina wanachama 5600 na kinaongozwa na Sheria ya Ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...