Na Said Mwishehe,Michuzi TV
KESHO ndio kesho kwa wanaotuhumiwa kwa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha!Ndivyo unavyoweza kuelezea kwani kesho ndio zinamalizika siku saba ambazo Rais Dk.Joh Magufuli amezitoa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) kushughulikia kesi za watuhumiwa hao ili watakaokiri na kukubali kurudisha fedha waachiwe huru.
Rais Dk.Magufuli Septemba 23,mwaka 2019 wakati wa kuwaapisha viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Ikulu jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine alishauri iwapo itawezekana wale ambao wapo mahabusu kwa kesi za tuhuma za uhujumi uchumi na utakatishaji fedha, wakiri makosa yao na baada ya hapo wapewe msamaha ili warudi uraiani.
Baada ya ushauri huo wa Rais , DPP Biswalo Mganga siku iliyofuata alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwa kutoa utaratibu ambao utatumika kwa watuhumiwa hao ambapo alieleza wazi
jambo hilo linawezekana endapo mshtakiwa mwenyewe ataiandikia ofisi yake barua kupitia kwa Mkuu wa Gereza na kusisitiza barua hiyo inapaswa kuandikwa na mtuhumiwa mwenyewe aliye gerezani na siyo Wakili. .
Tangu kutolewa kwa ushauri wa Rais kuhusu watuhumiwa hao na kisha DPP kutoa maelekezo ambayo yanapaswa kufuatwa imeelezwa kuwa idadi kubwa ya mahabusu wa kesi hizo wamejisalimisha ofisi za DPP kwa ajili ya kuomba msamaha ili waachiwe.
Hata hivyo hadi sasa haijafahamika idadi rasmi ya watuhumiwa ambao wameandika barua kwa DPP kupata msamaha huo ingawa inaelezwa kuwa wengi wanaotuhumiwa wamejitokeza kutumia nafasi hiyo kukiri makosa yao na kuomba msamaha.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na vyombo vya habari DPP Biswalo Mganga amenukuliwa akieleza ni vema akaachwa afanye kazi yake , hata hivyo alikiri ofisini kwake ameendelea kupokea watuhumiwa hao. Katika kuhakikisha watanzania wanafahamu kinachoendelea , Michuzi TV na Michuzi Blogu itaendelea kukujuza kuhusu watuhumiwa hao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...