Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge la 11 , Bungeni jijini Dodoma, Septemba 13, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akielekekea kenye eneo la kusomea hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge la 11, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 13, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wabunge, Bungeni jiini Dodoma, Septemba 13, 2019. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri , Ofisi ya Rais TAMISEMI na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara, Waziri wa Madini na Mbunge wa Bukombe, Doto Biteko, Mbunge wa Geita Vijijini Joseph Msukuma na wa pili kulia ni Waziri wa Nishati na Mbunge wa Chato, Dkt. Medard Kalemani
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Kuteuliwa, Janeth Masaburi kwenye jengo la utawala la Bunge jijini Dodoma, Septemba 13, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Viti Maalum, Bernadeta Mushashu, Bungeni jijini Dodoma, Septemba 13, 2019
Spika wa Bunge Job Ndugai akiongozwa kutoka kwenye ukumbi wa Bunge baada ya kuahirisha Mkutano wa 16 wa Bunge la 11, jijini Dodoma, Septemba 13, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

……………….
Shukrani
  • Mheshimiwa Spika, awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa kwenye mkutano huu wa 16 wa Bunge lako tukufu.
  • Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuendelea kuliongoza Bunge hili tukufu kwa umahiri mkubwa, ukisaidiwa na Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge. Aidha, niwashukuru sana Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kupokea na kuchambua taarifa, Maazimio na Miswada mbalimbali iliyowasilishwa kwenye Kamati hizo.
  • Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa michango mizuri mliyoitoa wakati wa mijadala ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali kwenye Mkutano huu ambayo ninaamini itasaidia sana kuboresha utekelezaji wa mipango ya Serikali. 
Salamu za Pole
  • Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapa pole Watanzania wenzangu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kupata ulemavu kutokana na ajali ya lori la mafuta iliyotokea tarehe 10 Agosti 2019 mjini Morogoro na kupoteza maisha ya watu 104. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za marehemu mahali pema peponi na awape nafuu majeruhi wapone haraka.
  • Mheshimiwa Spika, baada ya tukio hilo la kusikitisha tarehe 12 Agosti 2019 niliunda Kamati Maalumu kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Lengo lilikuwa kufahamu chanzo cha ajali, mazingira baada ya ajali na hatua gani zichukuliwe kuzuia matukio kama haya sambamba na kuwawajibisha wale wote ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo kabla na baada ya ajali kutokea. Tayari kamati hiyo imekamilisha majukumu yake na mamlaka husika zimeelekezwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa wale wote ambao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo.
  • Mheshimiwa Spika, niwashukuru madaktari na wahudumu wa Hospitali ya Rufaa ya Morogoro na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wadu wote ambao walishiriki katika kuokoa maisha ya wahanga wa ajali hiyo tangu ilipotokea. Nawasihi Watanzania wenzangu kujifunza kutokana na ajali hiyo iliyotokea Morogoro na hivyo kuepuka mikusanyiko ya aina hiyo katika maeneo ya ajali. Aidha, tujenge nyoyo za huruma na kuwa wepesi wa kutoa msaada kwa wahanga wa ajali badala ya kutumia ajali hizo kama fursa za kujinufaisha isivyo halali. 
  • Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Mohammed Dahman, mwanahabari nguli wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) aliyekuwa Balozi mzuri wa lugha ya Kiswahili ambaye alifariki tarehe 02 Agosti 2019 huko Ujerumani. Aidha, natoa pole kwa familia ya marehemu Ibrahimu Kaduma aliyefariki tarehe 31 Agosti 2019 huko nchini India alikokwenda kwa ajili ya matibabu. Marehemu Kaduma aliyekuwa mfuasi mkubwa wa falsafa za Mwalimu Julius Nyerere hasa za ujamaa na kujitegemea, atakumbukwa pia kwa kuitumikia nchi yetu katika nyadhifa mbalimbali ikiwemo uwaziri wa Mambo ya Nje. 
  • Mheshimiwa Spika, nitoe pole pia kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kutokana na kifo cha Dkt. Omary Nundu, aliyewahi kuwa Waziri wa Uchukuzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel, kilichotokea tarehe 11 Septemba 2019. Kadhalika, nitoe pole kwa wadau wa michezo kwa kuondokewa na Bw. Ramadhan Nasib, aliyewahi kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) tarehe 29 Agosti 2019 na pia kwa kuondokewa na shabiki wa Taifa Stars Bw. Christopher Rupia, ambaye alipoteza uhai wakati alipokwenda kuishuhudia na kuiunga mkono Taifa Stars ikicheza dhidi ya Burundi tarehe 8 Septemba 2019. Mungu aziweke roho za marehemu mahala pema. Amina!
  • Mheshimiwa Spika, tarehe 6 Septemba 2019, Tanzania ilipokea kwa mshtuko mkubwa kifo cha Rais Mstaafu na Baba wa Taifa la Zimbabwe Mheshimiwa Robert Gabriel Mugabe kilichotokea huko Singapore alikokwenda kwa ajili ya matibabu. Nami niungane na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa salamu za pole kwa Mheshimiwa Emmerson Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe, Familia ya Mzee Robert Gabriel Mugabe, Wananchi wa Zimbabwe, Waafrika na wale wote walioguswa na msiba huu.
  • Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa Mzee Robert Gabriel Mugabe, alikuwa ni miongoni mwa viongozi jasiri, shupavu na mwanamajumui wa Afrika (yaani Pan Africanist) aliyekataa ukoloni kwa vitendo. Tanzania tutaendelea kumkumbuka sana Mzee Mugabe kwa mchango wake mkubwa katika kuhakikisha Mwalimu Nyerere anaenziwa ipasavyo na Umoja wa Afrika, kutokana na mchango wake kwenye harakati za ukombozi na kujenga mtangamano wa Waafrika.
  • Mheshimiwa Spika, itoshe tu kusema kwamba Mzee Mugabe alimheshimu sana Mwalimu Nyerere hata kufikia hatua ya kuandika kitabu mwaka 2015 kiitwacho “Julius Nyerere, Ahsante sana, Thank You Mwalimu”. Kitabu hicho kimebeba simulizi nyingi kuhusu Mwalimu Nyerere na Tanzania. Tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahala pema. Amina!
Pongezi
  • Mheshimiwa Spika, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo hilo kufuatia uchaguzi mdogo uliofanyika hivi karibuni ambapo alipita bila kupingwa, karibu sana sisi Wabunge tunakuhakikishia kukupa ushirikiano katika kuwatumikia Watanzania wenzetu. 
SHUGHULI ZA BUNGE
Maswali na Majibu
  • Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kuuliza maswali ya msingi 123 na maswali 217 ya nyongeza ambayo yalijibiwa na Serikali. Pia, maswali 6 ya Papo kwa Papo yaliulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu.
Miswada ya Sheria
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili na kupitisha Miswada minne iliyowasilishwa na Serikali katika Mkutano huu. Miswada ya Sheria iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu katika Mkutano huu ni kama ifuatavyo:
  1. Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019;
  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019;
  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019; na
  1. Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.6) wa Mwaka 2019.
Maazimio ya Bunge
  • Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu, Bunge lako tukufu lilijadili na kuridhia maazimio nane kama ifuatavyo:
  1. Azimio la Kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania;
  1. Azimio la Kuridhia Mkataba wa Minamata Kuhusu Kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo Matumizi ya Zebaki ifikapo Mwaka 2030;
  1. Azimio la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika kutekeleza Itifaki ya Cartagena;
  1. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Hakimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea;
  1. Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere;
  1. Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Kigosi kuwa Hifadhi ya Taifa ya Kigosi; 
  1. Azimio la kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Ugalla kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla; na
  1. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Marrakesh inayowezesha Upatikanaji wa Kazi zilizochapishwa kwa Watu Wasioona, Wenye Uoni Hafifu au Ulemavu Unaofanya Mtu Kushindwa Kusoma ya Mwaka 2013.
  • Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri ya kuwasilisha Miswada na Maazimio yaliyojadiliwa katika Mkutano huu pamoja na kutoa ufafanuzi kuhusu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Kadhalika, nimpongeze Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wataalamu wake kwa kazi nzuri ya kuandaa miswada hiyo. 
DIPLOMASIA YA UCHUMI
  • Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha Mkutano huu, ningependa kutumia fursa hii japo kwa uchache kuzungumzia na kutoa ufafanuzi kuhusu baadhi ya masuala muhimu yaliyojiri katika kipindi hiki hususan utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.
  • Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika Kimataifa. Ukweli wa hili unajidhihirisha katika matokeo ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC); Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7) na juhudi za Serikali katika kujenga miundombinu wezeshi ya kiuchumi kwa lengo la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara na hivyo, kurahisisha utekelezaji wa dhana ya diplomasia ya uchumi. 
Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC
  • Mheshimiwa Spika, kama itakavyokumbukwa, tarehe 3 Septemba, 2019 Bunge lako tukufu lilipitisha Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa SADC na kuendesha vyema Mkutano wa 39 wa Jumuiya hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam, tarehe 17 na 18 Agosti, 2019.
  • Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio ya Uenyekiti wa Tanzania kwenye Mkutano huo ni kitendo cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kupitisha matumizi ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya nne katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini wa Afrika sambamba na lugha ya Kiingereza, Kifaransa na Kireno. Kwa kuanzia lugha ya Kiswahili itatumika katika mikutano ya Wakuu wa Nchi na Serikali na Baraza la Mawaziri.
  • Mheshimiwa Spika, Tanzania inaendelea kujivunia historia ya lugha ya Kiswahili hususan matumizi yake wakati wa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika na pia kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Umoja wa Afrika. Nitoe wito kwa wadau wote wa Kiswahili nchini, watumie vyema fursa hii kutengeneza ajira kupitia huduma za ukalimani, ufundishaji na masuala mengine yenye kuhusisha matumizi ya lugha hii adhimu yenye kuakisi utamaduni wa Mwafrika. Naiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kujipanga vizuri ili kuchangamkia fursa hiyo muhimu.
  • Mheshimiwa Spika, katika hotuba yake ya kupokea Uenyekiti wa SADC, Mheshimiwa Rais pamoja na mambo mengine alisisitiza umuhimu wa kuimarisha umoja na kuongeza biashara ndani ya Jumuiya sambamba na kukuza viwanda kwa kushiriki katika mnyororo wa thamani ndani ya ukanda wa SADC. 
  • Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, nitoe wito kwa Bunge lako tukufu, wadau wa sekta binafsi na Watanzania kwa ujumla wamuunge mkono Mheshimiwa Rais akiwa Mwenyekiti wa SADC ili aweze kutimiza malengo ya kujenga Mazingira Wezeshi kwa ajili ya Maendeleo Endelevu na Jumuishi ya Viwanda, Kukuza Biashara na Ajira ndani ya SADC.
  • Mheshimiwa Spika, taarifa kuhusu hali ya usalama wa chakula katika ukanda wa SADC, imeonesha kutetereka kutokana na athari mbalimbali ikiwemo ukame katika upande wa magharibi wa ukanda, mvua zilizokithiri, mafuriko na vimbunga vya IDAI na Kenneth pamoja na wadudu waharibifu wa mazao na magonjwa. 
  • Mheshimiwa Spika, athari hizo zimesababisha uzalishaji wa nafaka kama mahindi, mtama, mpunga, ngano na ulezi ndani ya SADC kupungua kwa asilimia 14 kutoka tani milioni 42.6 mwaka 2018 hadi tani milioni 36.8 mwaka 2019 sambamba na kupanda kwa bei. Hata hivyo, Tanzania na Afrika Kusini kwa kipindi hicho zilizalisha ziada ya mazao hayo ambayo yanakadiriwa kukidhi mahitaji kwa mwaka 2019/2020.
  • Mheshimiwa Spika, natambua pia kuwa tarehe 29 na 30 Agosti 2019, Wizara ya Kilimo iliratibu Mkutano na Wadau mbalimbali wenye kujihusisha na uzalishaji na biashara ya nafaka. Aidha, pamoja na kupongeza juhudi hizo zenye lengo la kujadili fursa zilizopo katika mazao ya nafaka, changamoto pamoja na utatuzi wake, nitumie fursa hii kuelekeza Wizara husika ihakikishe inashirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kutumia vema fursa ya uwepo wa masoko ya nafaka kwenye ukanda huu wa SADC na hivyo, kukidhi mahitaji katika ukanda sambamba na kuboresha biashara na maisha ya wananchi wa vijijini. Aidha, ni muhimu kuendelea kuhamasisha uzalishaji wa mazao hayo kwa wingi ili tuweze kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada.
Mkutano wa TICAD 7
  • Mheshimiwa Spika, katika mwendelezo wa utekelezaji wa diplomasia yetu ya kiuchumi, tarehe 28 hadi 30 Agosti 2019, nilimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo Kuhusu Maendeleo ya Afrika. Serikali imeendelea kutumia majukwaa na mikutano ya namna hii kusukuma ajenda mbalimbali za maendeleo kwa lengo la kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa maslahi ya Watanzania.
  • Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano wa saba wa TICAD, Serikali ya Japan imetenga kiasi cha Dola za Marekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu kwa nchi za Bara la Afrika. Lengo ni kuziwezesha nchi hizo kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi. Kiasi hicho kitatolewa ili kuendeleza miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, kilimo, maji, nishati, ujenzi wa maeneo maalumu ya viwanda na miundombinu ya usafiri na usafirishaji. 
  • Mheshimiwa Spika, ninaielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ishirikiane kwa karibu na Wizara zenye dhamana kuratibu vema utekelezaji wa miradi nane ya maendeleo ambayo tayari imewasilishwa kupitia TICAD 7 kwa ajili ya kujadiliwa na kupatiwa fedha za ufadhili. Lengo ni kuhakikisha nchi yetu inanufaika na fedha zilizotengwa na Serikali ya Japan kwa ajili ya nchi za Afrika katika kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. 
  • Mheshimiwa Spika, sambamba na Mkutano wa saba wa TICAD, ujumbe wa Tanzania ulitumia vema fursa ya Mkutano huo kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi mbalimbali, wakuu wa mashirika ya kimataifa na kitaifa, taasisi na makampuni mbalimbali. Mazungumzo na viongozi na wadau hao wa maendeleo yamekuwa na tija katika kusukuma ajenda za kuendeleza biashara na uwekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii. Baadhi ya maeneo yaliyopewa kipaumbele ni uwekezaji kwenye viwanda vya nguo na nyuzi, sukari, sekta ya uvuvi, elimu, nishati pamoja na uboreshaji wa sekta ya afya ikiwemo kuimarisha huduma za uchunguzi wa kisasa wa magonjwa na matengenezo ya vifaa tiba.
  • Mheshimiwa Spika, Serikali ya Japan na wadau wengine wa maendeleo wameridhishwa na kusifu namna Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, anavyosimamia mwenendo wa uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan ile inayotekelezwa kwa kushirikiana na nchi hiyo. Aidha, Tanzania na Japan zinaendelea na mashauriano kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kipaumbele ikiwemo kuendeleza Jiji la Dodoma pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kuboresha barabara; ukarabati wa bandari ya Kigoma na mradi wa maji Zanzibar.
Uimarishaji wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji
  • Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Tanzania imeanza kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara nchini (Blueprint on Regulatory Reforms For Improved Business Environment) na Mpango Kazi wa Utekelezaji wake tangu Julai mosi, 2019. Aidha, sote tunatambua kuwa lengo la blueprint ni kujenga mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji ambapo kupitia Mkutano wa 15 wa Bunge la 11 jumla ya kodi na tozo 54 ziliondolewa.
  • Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, Serikali imeunda Timu ya Wataalamu ambayo inafanya uchambuzi wa changamoto zilizobainishwa kwenye taarifa mbalimbali na kuandaa mapendekezo ya marekebisho ya sheria husika. Aidha, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu ya bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu inakamilisha mapitio na uandaaji wa Sera mpya ya Uwekezaji nchini. Hivyo, nitoe rai kwa wadau wote kutoa maoni yao kuhusu mapitio ya Sera ya Uwekezaji hasa kupitia tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya www.pmo.go.tz na ile ya Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) ya www.tpsftz.org.  
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, nitumie fursa hii kumpongeza tena Mheshimiwa Rais kwa hatua za makusudi anazochukua kuhakikisha anaimarisha shughuli za biashara na uwekezaji kupitia ziara za kitaifa za viongozi rafiki kutoka mataifa mbalimbali sambamba na makongamano ya kibiashara na uwekezaji.
  • Mheshimiwa Spika, kati ya Agosti na Septemba 2019, Mheshimiwa Matalema Cyril Ramaphosa, Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini na Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda walifanya ziara rasmi za Kiserikali nchini Tanzania. Vilevile, ziara hizo muhimu ziliambatana na makongamano ya biashara na uwekezaji kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na nchi hizo.
  • Mheshimiwa Spika, niungane na Mheshimiwa Rais kusisitiza kuwa makongamano ya namna hiyo yamekuwa na mchango mkubwa katika kubaini na kutumia fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini lakini pia kushughulikia changamoto za kibiashara na uwekezaji zinazokabili pande husika.
  • Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine ya kuimarisha biashara na uwekezaji Mheshimiwa Rais wetu mpendwa tarehe 22 Agosti 2019, jijini Dar es Salaam, alikutana na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje. Kupitia mkutano huo, Mheshimiwa Rais aliwafahamisha Mabalozi kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini na wajibu wa Mabalozi katika kuvutia uwekezaji nchini, kutafuta masoko ya bidhaa na mazao yetu na kutangaza utalii. Nami niungane tena na Mheshimiwa Rais kusisitiza kuwa utendaji wa wawakilishi wetu nje, utaendelea kupimwa kwa idadi na matokeo ya uwekezaji na biashara walizovutia nchini.
  • Mheshimiwa Spika, mwaka 2001 Robert Kiyosaki, mwandishi maarufu wa vitabu aliwahi kuandika nami ninamnukuu: “The size of your success is measured by the strength of your desire; the size of your dream; and how you handle disappointment along the way.” Mwisho wa kunukuu. Kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, mwandishi huyu anajaribu kueleza kuwa ukubwa wa mafanikio yako hupimwa kwa kiwango cha utashi, ndoto zako na namna unavyokabiliana ama kukatishwa tamaa wakati ukitekeleza malengo yako.
  • Mheshimiwa Spika, nukuu hii kwa kiasi kikubwa inaakisi dhamira ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha anajenga misingi ya uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea pamoja na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi bila kutetereka kutokana na kauli za kubeza zinazotolewa na baadhi ya watu wachache wasioitakia mema nchi hii.
Ujenzi wa Miundombinu Wezeshi
  • Mheshimiwa Spika, juhudi hizo za Mheshimiwa Rais zinakwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu wezeshi ikiwemo ya usafiri na usafirishaji, nishati pamoja na maendeleo ya Jamii. Napenda kutumia fursa hii kutaja japo kwa uchache baadhi ya miradi inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Rais kwa lengo la kuchochea uwekezaji, kujenga uchumi imara, shindani na wenye kujitegemea. 
Mosi:    Kuongeza Bajeti kwa ajili ya mikopo ya Elimu ya Juu kutoka Shilingi bilioni 186.48 mwaka 2010 hadi Shilingi bilioni 424 mwaka 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 44.1 sambamba na ongezeko la wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya Elimu ya Juu kutoka wanafunzi 72,035 mwaka 2009/2010 hadi kufikia 122,754 mwaka, 2018/2019 sawa na ongezeko la asilimia 58.7;
Pili:    Kuendelea na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma na kisha kufikisha kwenye mipaka ya nchi za Burundi na Rwanda, kwa fedha zetu wenyewe. Ujenzi wa Kilometa 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro upo katika hatua nzuri na kilometa 412 kutoka Morogoro hadi Makutupora nao unaendelea vizuri. Gharama za ujenzi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma zitafikia shilingi trilioni 7.062;
Tatu:    Kuendelea na upanuzi wa bandari zetu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga ambao utagharimu shilingi Trilioni 1.2;
Nne:    Kukamilika kwa ujenzi wa meli mbili za Mv. Iringa na Mv. Ruvuma, ambazo zinatoa huduma katika Ziwa Nyasa. Kuendelea na ukarabati wa meli mbili za Mv. Victoria na Mv. Butiama pamoja na ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya Ziwa Victoria kwa zaidi ya shilingi bilioni 172.3;
Tano:    Kuendelea na ujenzi wa Ubungo Interchange kwa shilingi bilioni 247 na barabara ya njia nane kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze kwa gharama ya shilingi bilioni 140;
Sita:    Ujenzi wa Daraja la Kigongo – Busisi unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 699.2;
Saba:    Kuendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme, ikiwemo kutumia gesi yetu asilia na ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa maji wa Megawati 2,115 (Nyerere Hydro Power Project) kwa shilingi trilioni 6.5 katika maporomoko ya mto Rufiji; na
Nane:    Kukamilika kwa ujenzi wa Jengo la Tatu la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa gharama ya shilingi bilioni 722, na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kilimajaro kwa thamani ya shilingi bilioni 91. Aidha, tunaendelea na ukarabati wa viwanja takriban 11 vya ndege sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Mwanza (bilioni 90); Mtwara (shilingi bilioni 46); Shinyanga (shilingi bilioni 49.2); Sumbawanga (shilingi bilioni 55.9); Musoma (shilingi bilioni 21), Songea (shilingi bilioni 21) na Iringa (shilingi bilioni 39);
  • Mheshimiwa Spika, maboresho katika sekta ya usafiri wa anga na mengine yanayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano yamekuwa na matokeo makubwa katika kuitangaza na kuimarisha heshima ya Tanzania kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kwa mfano, tumeendelea kupokea fursa ya kuwa wenyeji wa matamasha ya kimataifa ya utamaduni, wachezaji na wasanii maarufu akiwemo muigizaji wa sinema wa Marekani, Will Smith ambaye amekuja nchini zaidi ya mara mbili. 
  • Mheshimiwa Spika, Watanzania wote wanatambua tukio lililotokea hivi karibuni la kushikiliwa kwa Ndege yetu aina ya Airbus 220-300 huko Afrika Kusini. Napenda kutumia nafasi hii kulipongeza jopo la Wanasheria wazalendo wa Kitanzania wakiongozwa na Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Songea Manispaa kwa jitihada zao za kupigania kurejeshwa kwa Ndege yetu hapa nchini, bila kuwasahau Watanzania walioonesha kukerwa kwa tukio lile. TANZANIA ITAJENGWA KWANZA NA WATANZANIA WENYEWE.
  • Mheshimiwa Spika, tarehe 21 hadi 28 Septemba 2019, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Tamasha la Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki lijulikanalo kama Jumuiya ya Afrika Mashariki Utamaduni Festival (JAMAFEST). Rai yangu kwa waandaaji na wadau wa tasnia ya ubunifu na ujasiriamali ni kutumia vema fursa ya uwepo wa Tamasha hilo lenye kukutanisha viongozi, wabunifu, wajasiriliamali na wasanii kuhamasisha masoko ya bidhaa za wabunifu na wajasiriamali kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu ya masoko ya bidhaa hizo.
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine nitumie pia fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hamis Kigwangalla (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii, Ubalozi wa Tanzania nchini China, Watendaji wa Wizara na Bodi ya Utalii nchini kwa kufanikisha Makubaliano na Mtandao maarufu nchini China (BAIDU). Lengo la makubaliano hayo ni kuongeza idadi ya Wachina wanaotembelea vivutio vyetu vya utalii kutoka 32,773 msimu uliopita hadi 100,000. 
  • Mheshimiwa Spika, Tanzania ndiyo nchi pekee kutoka Afrika iliyofanikiwa kuingia katika mpango wa BAIDU ujulikanao kama “Wonder Planet”. Vilevile, ndiyo nchi ya kwanza kutembelewa na timu inayoandaa mpango huo. Mpango wa Wonder Planet, una lengo la kutembelea nchi saba ili kuona vivutio vilivyopo kwenye nchi hizo na kuvitangaza kwa wateja wa mtandao huo wasiopungua milioni 700.
  • Mheshimiwa Spika, tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi hiki. Waswahili husema “huwezi kuwasha taa, halafu ukaifunika”. Hivyo basi, tunaeleza mafanikio haya ili wananchi watambue kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha inashirikiana nao katika kujenga Taifa lenye uchumi imara, shindani na wenye kujitegemea. Kwa lugha nyingine, mipango endelevu tuliyojiwekea, sera maridhawa na usimamizi makini vinatupa matumaini kuwa lengo tulilojiwekea linatimia pasi na shaka.
  • Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia muktadha huo, niwaombe Watanzania wenzangu kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awajalie viongozi wetu hekima na busara ili waendelee kuliongoza Taifa letu kwa haki, kuondoa uovu, kujenga umoja na mshikamano, kudumisha amani katika nchi yetu pamoja na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
  • Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa wito kwa wawekezaji kutumia fursa ya uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara, miundombinu wezeshi, upatikanaji wa malighafi na rasilimali watu kwa ajili ya kujenga viwanda mbalimbali hususan vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na malighafi nyinginezo zinazopatikana nchini.
KILIMO
Hali ya Chakula
  • Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini imeendelea kuwa toshelevu. Kwa mfano, katika msimu wa kilimo wa 2018/2019 uzalishaji ulifikia takriban tani milioni 16.41 ikilinganishwa na mahitaji ya tani milioni 13.84. 
  • Mheshimiwa Spika, hivi sasa wafanyabiashara wa mazao ya chakula wanaendelea kusafirisha na kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi. Serikali inawahimiza wananchi wote kuhifadhi chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya nyumbani hususan wakati huu tunapoingia kwenye msimu mpya wa kilimo kwa mwaka 2019/2020.
Maandalizi ya Msimu wa Kilimo
  • Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha kuanzia Septemba 2019 maeneo mengi ya nchi yetu huanza kupata mvua za vuli ambazo ni ishara ya kuanza kwa msimu mpya wa kilimo. Serikali inahakikisha pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu bora, mbolea na viuatilifu kwa ajili ya msimu huu mpya wa kilimo zinapatikana.
  • Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuiagiza Wizara ya Kilimo ihakikishe inasimamia ipasavyo mawakala waliopewa jukumu la kusambaza pembejeo kwa wakulima ili ziwafikie kwa wakati na kwa bei inayohimilika na ubora unaohitajika.
Upatikanaji wa Masoko ya Mazao
  • Mheshimiwa Spika, nawapongeza wakulima kwa kuitikia wito wa Serikali katika kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya kilimo hasa yale ya biashara kama vile pamba, tumbaku, kahawa na korosho. 
Pamba
  • Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya bei ya pamba katika soko la dunia yaliyosababishwa na mgogoro wa kibiashara kati ya mataifa makubwa yameporomosha bei ya pamba katika soko la dunia kinyume na matarajio kuwa bei ingeongezeka. Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua zifuatazo:
Mosi:    Kusimamia makubaliano kati ya Benki Kuu na Benki zilizotoa mikopo kwa kampuni zinazonunua pamba kulingana na mahitaji yao ya mitaji ya kununua pamba ili pamba yote inunuliwe kwa wakati;
Pili:    Kuhamasisha makampuni kupeleka fedha kwa ajili ya malipo ya wakulima na kulipia pamba iliyopimwa ghalani na iliyobaki mikononi mwa wakulima.
Tatu:    Kudhibiti udanganyifu kupitia mizani, malipo ya wakulima na makato ya pembejeo katika maeneo yaliyobainika kutokea kwa vitendo hivyo.
  • Mheshimiwa Spika, hivi sasa, wanunuzi wote wamepewa maeneo yote yenye Pamba na tayari wameshapewa fedha kwa ajili ya kulipia pamba yote. Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wasimamie manunuzi haya ili wakulima walipwe malipo yao stahiki.
Tumbaku
  • Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 31 Agosti, 2019 mauzo ya tumbaku za mkataba yalikuwa yamekamilika. Jumla ya kilo milioni 60.59 zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 92.79 zilinunuliwa. Kiasi hicho, ni sawa na asilimia 105.7 ya lengo la kuzalisha kilo milioni 57.31 za tumbaku ya mkataba. 
  • Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tathmini ya masoko imeonesha uwepo wa tumbaku ya ziada kiasi cha kilo milioni 12.22 ambazo zilizalishwa nje ya mkataba katika maeneo mbalimbali. Serikali inaendelea na majadiliano na makampuni ya ununuzi kwa lengo la kuhakikisha tumbaku yote inanunuliwa.
Korosho
  • Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2018/2019 jumla ya tani 224,964 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi bilioni 729.90 zilikusanywa. Kati ya hizo, tani 222,825 zilikusanywa na Serikali. Aidha, korosho zilizolipwa ni tani 197,547 na Serikali inakamilisha malipo ya kiasi kilichobaki cha tani 25,278. Hivi sasa, korosho yote imenunuliwa na inasafirishwa. Aidha, baada ya zoezi hilo Bodi ya Mazao Mchanganyiko itarudi kulipa madeni yaliyobaki kwa wakulima na wenye maghala.
  • Mheshimiwa Spika, kuelekea msimu ujao wa ununuzi wa korosho, Serikali imeandaa mikakati ya kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika. Jitihada zinazofanywa na Serikali hivi sasa ni:-
Moja:    Kuvutia uwekezaji katika viwanda vya kubangua korosho nchini;
Mbili:    Kupanua soko la korosho kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine zitokanazo na korosho zikiwemo siagi, maziwa, mvinyo na sharubati;
Tatu:    Kuendelea kujenga maghala ya mfano na yenye viwango kwa ajili ya kuhifadhia korosho katika maeneo ya kimkakati;
Nne:    Kusimamia uuzwaji wa korosho inayozalishwa nchini kwa wakati ili kutumia fursa ya korosho ya Tanzania ambayo inazalishwa kipindi ambacho hakuna korosho nyingine katika soko la dunia; na
Tano:    Kuimarisha mifumo ya ununuzi wa korosho kwa lengo la kuvutia wanunuzi wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi;
  • Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, msimu wa korosho utaanza na wakulima wataarifiwa kuhusu utaratibu mzima wa uuzaji. Aidha, Serikali itatoa nafasi ya kwanza ya ununuzi kwa wenye viwanda nchini. Hivyo, ni vema sasa waandae mahitaji yao kwa msimu huu na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika ili kuwahakikishia malighafi ya kutosheleza mahitaji ya viwanda vyao.
  • Mheshimiwa Spika, kama mtakavyoona, Serikali inafanya kazi kubwa ya kuimarisha masoko ya mazao ndani na nje. Kwa msingi huo, naielekeza Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa masoko mapya ya mazao mbalimbali. 
  • Mheshimiwa Spika, wizara hizo, zinapaswa kuzingatia maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipokutana na Mabalozi wanaoiwakilisha nchi yetu. Aidha, taasisi zinazohusika na utafutaji wa masoko ikiwemo Soko la Bidhaa (TMX), TanTrade na Bodi zote za Mazao zijikite katika kutafuta masoko ya mazao yanayozalishwa nchini. 
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
  • Mheshimiwa Spika, tarehe 24 Novemba 2019, nchi yetu itafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano. Lengo la uchaguzi huo ni kukidhi matakwa ya Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inayoelekeza kuwa Mamlaka na Madaraka ya Serikali yanatokana na wananchi. 
  • Mheshimiwa Spika, wakati tukielekea kwenye uchaguzi huu, napenda kusisitiza mambo yafuatayo:
Moja:    Kuwasihi Waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuhamasisha wananchi watumie haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa. Natoa rai kwenu kuhakikisha mnashiriki kikamilifu katika shughuli zote za uchaguzi huo;
Pili:    Kuwahimiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya waratibu shughuli za uchaguzi katika maeneo yao na kuhakikisha uwepo wa ulinzi na usalama wakati wote wa uchaguzi hasa kipindi cha Kampeni na wakati wa kupiga kura. Vyombo vya ulinzi na usalama vishiriki kikamilifu kuhakikisha wananchi wanafanya uchaguzi katika mazingira ya amani na utulivu bila kubughudhiwa; na
Tatu:    Kuwahimiza Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhakikisha wanazielewa Kanuni na miongozo ilitoyotolewa ili waweze kutoa tafsiri sahihi wakati wa kusimamia uchaguzi huo na kuhakikisha unafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa mujibu wa Sheria.
  • Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Watanzania wote wenye sifa wajiandikishe katika orodha ya wapiga kura, wachukue fomu za kugombea nafasi mbalimbali na kushiriki kupiga kura kwani hiyo ni haki yao ya kikatiba kwa kuzingatia misingi ya demokrasia. 
  • Mheshimiwa Spika, pia, nitoe rai kwa wadau mbalimbali watakaoshiriki katika uchaguzi wakiwemo Vyama vya Siasa, Taasisi za Serikali na Zisizo za Serikali na Wananchi kusoma na kuzielewa Kanuni na miongozo ya uchaguzi kwa kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vyovyote vya rushwa na uvunjifu wa amani. Serikali haitasita kuchukua hatua pale itakapothibitika vitendo hivyo kufanyika kinyume cha Kanuni na Sheria nyingine za nchi. 
UBORESHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura, tarehe 18 Julai 2019 Serikali ilizindua zoezi hilo mkoani Kilimanjaro. Uboreshaji huo, unahusisha Wapiga Kura waliotimiza umri wa miaka 18 na wale watakaotimiza umri huo wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
  • Mheshimiwa Spika, makundi mengine yatakayohusika ni wapiga kura waliohamia katika kata au jimbo jingine la uchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao zimeharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao; mfano majina ambayo hapo awali yalikuwa yamekosewa pamoja na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza sifa kama vile kufariki.
  • Mheshimiwa Spika, kwa sasa zoezi hilo tayari limekamilika katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Simiyu, Mara na Mwanza (isipokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba). Zoezi hilo linaendelea kutekelezwa chini ya kaulimbiu isemayo Kadi Yako, Kura Yako, Nenda Kajiandikishe.
  • Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wote wanaoendelea kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Aidha, nitoe rai kwa wananchi ambao bado hawajajiandikisha, wafanye hivyo ili watimize haki yao ya Kikatiba. Kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, nirudie maelekezo niliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo kwa waandikishaji kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu ikiwemo wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu ili wasikae kwenye foleni kwa muda mrefu.
MICHEZO
  • Mheshimiwa Spika, katika nyanja ya michezo naomba nitoe pongezi za dhati kwa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Umri wa Miaka 20 (maarufu kama Tanzanite) kwa kutwaa kombe la mpira wa Miguu kwa Nchi za COSAFA huko Port Elizabeth, Afrika ya Kusini. Aidha, naipongeza timu ya kandanda ya Taifa Stars kwa kufanikiwa kuiondoa Harambee Stars katika mashindano ya CHAN 2020. Kadhalika, kwa kuiondoa Burundi na kufanikiwa kuingia hatua ya makundi ya kufuzu Kombe la Dunia huko Doha, Qatar 2022. Hatua hii ni nzuri na muhimu kwani inaiweka timu yetu katika nafasi nzuri kushiriki fainali za mashindano hayo. Timu ya Taifa itarudi dimbani kupambana na Sudan tarehe 22 Septemba, 2019 kwenye Uwanja wa Taifa. Kama kawaida yetu twenda tukaujaze Uwanja wetu na kuishangilia kwa nguvu timu yetu ya Taifa.
  • Mheshimiwa Spika, vilevile, navipongeza vilabu vya Azam, Malindi na Yanga kwa kufanikiwa kusonga mbele kuingia hatua ya pili katika michuano ya vilabu ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF). Aidha, kwa vilabu vya KMC, KMKM na Simba, ambavyo vimeondolewa katika hatua ya mwanzo kabisa, vichukulie hali hiyo kama changamoto ya kujitathmini na kujiandaa kwa ajili ya michezo ya ndani na mashindano yajayo ya kimataifa badala ya kutumia muda mrefu kujadili kuhusu kutolewa kwao mapema.
  • Mheshimiwa Spika, kwa upande wa masumbwi, bendera ya Tanzania imeendelea kupeperushwa vyema kufuatia wana masumbwi wengine wawili wa Kitanzania kufanya vizuri katika medani za kimataifa. Nitumie nafasi hii kuwapongeza mwanamasumbwi Abdallah Shaaban Pazi maarufu Dulla Mbabe kwa kufanikiwa kutwaa ubingwa wa dunia wa WBO baada ya kumpiga kwa KO kwenye raundi ya tatu mpinzani wake Mchina anayejulikana kwa jina la Zulipikaer Maimaitiali. 
  • Mheshimiwa Spika, nampongeza pia mwanamasumbwi mwingine wa kitanzania Bruno Tarimo maarufu vifua viwili kwa kumnyoosha mpinzani wake Mserbia, Scheka Gurdijeljac kwenye pambano la ubingwa wa dunia lililofanyika mwanzoni mwa mwezi huu huko Serbia. Hongereni sana wanamichezo wetu na endeleeni na moyo huo wa kizalendo mliouonesha katika kuipeperusha vema bendera ya Taifa letu. 
  • Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mrembo wetu Miss Tanzania 2019, Miss Sylvia Sebastian Bebwa pamoja na Queen Anthony Magese na Greatness Amos Nkuba walioshika nafasi ya pili na ya tatu. Tunamtakia matayarisho mema Miss Tanzania ili akapeperushe vema Bendera ya Taifa letu nchini Uingereza kwenye mashindano ya Mrembo wa Dunia (Miss World) ambako pia ataitangaza nchi yetu na vivutio vya utalii tulivyonavyo. Aidha, naitaka Wizara kuendelea kuratibu vizuri shughuli za michezo, utamaduni na sanaa ili zilete ufanisi wa hali ya juu na pia kuweka msisitizo sambamba na kuwa na mikakati ya kuendeleza michezo ikiwemo shuleni, vituo maalumu vya michezo sambamba na kuwa na mifumo mizuri ya upatikanaji wa fedha za kuendesha vilabu nchini.
HITIMISHO
  • Mheshimiwa Spika, wakati nikielekea kuhitimisha hotuba yangu napenda kukupongeza pamoja na Bunge lako tukufu kwa heshima kubwa tuliyoipata kama nchi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 50 wa Chama cha Mabunge cha Jumuiya ya Madola, Kanda ya Afrika (CPA) uliofanyika huko Zanzibar tarehe 2 Septemba 2019.
  • Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa mkutano huo ni ishara tosha ya utekelezaji mzuri wa diplomasia yetu ya mabunge yaani parliamentary diplomacy ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kusaidia kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania, kuingiza fedha za kigeni na kutoa fursa kwa wanyabiashara nchini kufanya biashara zao hususan zile za utoaji huduma (service delivery).
  • Mheshimiwa Spika, nami niungane nawe kutoa rai kwa wafanyabiashara na Watanzania wenzangu kwa ujumla kuchangamkia fursa hizi adhimu tunazozipata kwa kuaminiwa na mataifa mbalimbali kwani licha ya kuja kwetu, mataifa mengine pia yangetamani kuzipata kutokana na mchango wake katika kuinua kipato cha wananchi kupitia biashara za huduma.
  • Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kumshukuru Katibu wa Bunge na watendaji wa Ofisi ya Bunge kwa kazi kubwa ya kuratibu vikao vya mkutano huu. Aidha, niwashukuru watendaji wa Serikali kwa kufanikisha shughuli zilizopangwa na Bunge lako tukufu kwa weledi na ufanisi mkubwa. 
  • Mheshimiwa Spika, kipekee, niwashukuru wanahabari kwa kufikisha habari kuhusu mkutano huu kwa wananchi. Nivishukuru pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa huduma wanazozitoa kwa washiriki wa Bunge hili bila kuwasahau madereva waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa Bungeni. 
  • Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwatakia safari njema Waheshimiwa Wabunge, niwaombe mnaporejea majimboni kwenu muendelee kuwahamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kushiriki ipasavyo kwenye uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa. Aidha, waendelee kuiunga mkono Serikali kwenye jitihada zake za kujenga uchumi imara, wenye ushindani na kujitegemea.
  • Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 05 Novemba, 2019 siku ya Jumanne saa tatu kamili asubuhi litakapokutana tena katika ukumbi huu Jijini Dodoma.
  • Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...