Ni baada ya kumuomba msamaha, akiri alijifikiria sana lakini...
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
RAIS wa Serikali ya Awamu ya Tano Dk.John Magufuli ametangaza kumsamehe Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema William Ngeleja.
Siku za karibuni Januari Makamba na Ngeleja walisikika kupitia sauti zao wakiongea kwenye simu wakimteta Rais Magufuli na kutoa lugha zilizoonekana ni za dhihaka dhidi ya Rais.
Hata hivyo Rais Magufuli hakuwahi kuzungumza chochote kuhusu sauti za wabunge hao pamoja na vigogo wengine wa CCM ambao nao walisikika sauti zao wakimsema Rais.
Akizungumza leo Septemba 4,2019 jijini Dar es Salaam mbele ya Wakadiriaji Majengo, Wahandisi na Wakandarasi Rais Magufuli amesema kuna watu fulani walimtukana na akajiridhisha sauti hizo ni zao.
"Nikajiridhisha kwa asilimia zaidi ya 100 nikawa nafikiriaa...nikasema hawa wakipelekwa kenye kamati ya siasa ya kamati kuu adhabu itakuwa kubwa, nikaona ngoja ninyamaze.
"Nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha na kutoa kweli kutoka dhamira ya moyo wao ambao ni Mheshimiwa Januari Makamba na Ngeleja waliomba msamaha wakanigusa , nikaona ngoja na ni vijana acha niwasamehe.
Kabla ya kutangaza kuwasamehe wabunge hao, Rais Magufuli amesema kuwa kuna wakati inabidi usamehe ingawa kusamehe nako kunauma.
"Hivyo lazima kuwe na tabia ya kusamehe hata kama wakati mwingine ni ngumu nakumbuka siku za karibuni kuna watu fulani walinitukana tukana wee.
"Na sauti ambazo zilisikika ni za kwao kwa asilimia 100 lakini nimeamua kuwasamehe,"amesema Rais Magufuli na kisha akatumia nafasi hiyo kueleza namna ambavyo alitumia muda mwingi kuwafikiria hao walimtukana.
Kwa kukumbusha tu baada ya sauti za Januari Makamba na Ngeleja kusikika hadharani kupitia mitandao ya kijamii, baadhi ya wana CCM walicharuka na kutoa matamko ya kila aina kabla ya Katibu Mkuu wa CCM Dk.Bashiru Ally kutoa tamko la kuzuia watoa matamko.
Baada ya kutolewa katazo hilo na Katibu Mkuu wa CCM, Rais Magufuli alifanya mabadiliko kwenye baraza lake la mawaziri ambapo alimuondoa Januari Makamba aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais aneyeshughulikia Muungano na Mazingira.
Hata hivyo Rais alifafanua kuwa amemuondoa Janauri Makamba katka baraza lake la mawaziri kutokana na kutotekeleza maagizo aliyokuwa akipewa likiwemo la katazo la mifuko ya plastiki.
Baada ya kutoa ufafanuzi huo Rais Magufuli amekuwa kimya na hakuwataka kuzungumzia tena kuhusu sauti za wabunge hao lakini leo ameamua kuweka mambo hadharani na kutangaza kuwasamehe.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...