Na Moshy Kiyungi, Tabora

Hauwezi kuamini bendi iliyoanzishwa zaidi ya miongo minne iliyopita, bado ipo inapiga muziki. Bendi hiyo ni ya Orchestra Super Mazembe iliyojipatia umaarufu mkubwa katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati, ikiwa na  makao yake makuu Nairobi, Kenya.

Historia inaeleza kuwa kabla ya kuitwa Super Mazembe, ilikuwa na mizizi katika kundi la Super Vox, iliyoundwa mwaka 1967, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikiongozwa na Mutonkole Longwa Didos.

Mwaka 1974 Super Vox ikahamishia makazi yake katika jiji la Nairobi nchini Kenya, ambako ndiko walikobadili jina la bendi kuwa Orchestra Super Mazembe. Kwa mujibu wa Mutokole, alisema kuwa bendi yao ilikuwa ikitoa burudani za muziki wa Soukous katika kumbi mbalimbali za jijini humo, kibao chao kikubwa walichoanza nacho wakakiimba kwa lugha adhim ya Kiswahili ni wa Shauri yako.

Vibao vingine maarufu vilivyotamba wakati huo ni pamoja na Loboko, Kayembe, Nabimakate, Atia Joe, Samba, Bwana Nipe Pesa na Kasongo. Super Mazembe ilihesabiwa kama moja ya bendi za Kikongo wakati wa ‘dhahabu’ nchini Kenya.

Ikiwa nchini humo bendi hiyo ilikumbana na bendi zingine zilizokuwepo jijini humo za Les Mangelepa, Baba Gaston, Orchestra Virunga, Orchestra Moja One, Les Knoirs na zingine nyingi, ambazo nazo zilikuwa na wanamuziki wengi waliokuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire).

Kama makundi mengi ya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yaliyojikita katika nchi za  ya Afrika Mashariki, Super Mazembe ilikuwa tishio kwa jinsi ilivyokuwa imeenea wanamuziki waliokuwa mahiri kila idara.

Baadhi ya wanamuziki wa bendi hiyo ambao kila mara walikuwa wakiingia na kutoka, ni pamoja na Mutonkole Longwa Didos, Lovy Longomba, Kasongo wa Kanema, Kilambe na Katele Aley waliokuwa watunzi na waimbaji.

Lovy aliacha bendi hiyo mwaka 1981, alianzisha vikundi vya Super Lovy na baadae Bana Likasi. Lovy alikuwa ni mwana wa Vicky Longomba, aliyekuwa mwanamuziki mkongwe katika bendi ya T.P.OK.Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luambo Makiadi.

Familia ya mzee huyo takriban wote wamepitia mambo ya muziki akiwemo Awilo Longomba, Watoto wa Lovy Longomba wakiongozwa na Christian Lovy, ambao waliunda kikundi chao  cha Longombas, ambacho ni maarufu nchini Kenya.

Kasongo wa Kanema naye aliondoka katika bendi hiyo mapema miaka ya 1980, akaenda kujiunga katika bendi ya Orchestra Virunga, iliyokuwa ikiongozwa na Samba Mapangala. Kwa upande wa washika ala za muziki alikuwepo Bukasa wa Bukasa ‘Bukalos’ aliyekuwa kiongozi wa wapiga magitaa. Bukalos alitangulia mbele za haki mwaka 1989.

Aidha alikuwepo mcharazaji wa mwingine wa gitaa Kayembe Miketo, ambaye alifariki dunia mwaka 1991. Muungurumishaji wa gitaa zito la besi alikuwa Mwanza wa Mwanza Mulunguluke ‘Atia Jo’, aliyefariki dunia mwaka 2006. Komba Kasongo Songoley aliyekuwa ikilicharaza gitaa, yeye alifariki mwaka 1990.

Drums zilikuwa zikicharazwa na Kitenge Ngoi wa Kitombole na Musa Olokwiso Mangala. Orchestra Super Mazembe ilitamba kwa nyimbo zao zingine za Mwana Mazembe, Longwa Mukala Musi, Ouma ya mwaka 1980, Banamama ya mwaka 1983, Samba ya mwaka 1978, Okova, Mbanda ya Mobange na Mwana Nyau.

Kama zilivyo wahi kuanguka bendi zingine, halikadhalika Super Mazembe aliondoka kwenye sura ya muziki mwaka 1985 baada ya baadhi ya wanamuziki wake kuokoka na wengine kufariki dunia. Lakini habari zilizopatikana hivi karibuni toka Nairobi, zimeeleza kwa Super Mazembe imerejea tena ulingoni, baada ya baadhi ya wanamuziki wake walio hai, kuizindua upya.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa mitandao mbalimbali.
Mwandaaji anapatikana kwa namba: 0713331200, 0736331200, 0784331200 na 0767331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...