Na Said Mwishehe, Michuzi Tv
KUNA siku huwa najikuta nawaza ujinga tu, tena ujinga ambao hauna maana yoyote ile kwa yoyote.
Ndio! Sijui akili yangu ikoje? Nashindwa kuilewa kabisa na kwa nini mimi tu ndio niwaze ujinga? Nimekuwa nikijiuliza nakosa majibu.
Ipo siku Mungu wangu ambaye naamini kwa kila jambo atanipa utimamu wa akili. Nitakuwa na akili nambari moja, nitakuwa na akili ambayo itanifanya nichambue na kueleza mambo kwa kina. Hii akili ya kuwaza ujinga iko siku sitakuwa nayo. Najua nitaimisi lakini huenda Mungu anataka kunitoa nilipo na kuniweka kwenye daraja la wenye akili.
Bahati nzuri katika nchi yetu hii ya Tanzania, wajinga tunayo nafasi ya kusikilizwa. Hata kama tunapuuza lakini angalau ujinga wangu utapata nafasi ya kusikika au kuonekana hata kwa bahati mbaya.
Nikiri tu, ujinga wangu ndani yake umechanganyikana na baadhi ya mambo. Pata picha sina elimu halafu mjinga. Yaani kichwani huko nakujua mwenyewe tu.
Kwanza hata wewe ambaye umesoma hadi hapa nilipofika umenivumilia kweli. Najiuliza unaweza kusoma maneno yaliyoandikwa na mjinga mimi.
Kwa kuwa sina ambaye nimemlazimisha kusoma hapa haya twende. Fuatilia tu kusoma ujinga wangu. Hutapata dhambi lakini naamini utakuwa tu unafahamu mjinga nawaza nini.
Hata hivyo, najua changamoto ya msomi anapokutana na vitu vya kijinga. Nahisi anaweza kuwaza huyu mtu ni wa wapi? Ni wa dunia hii hii inayoishi binadamu. Ndio naishi duniani hapa hapa, unataka nikaishi wapi? Nani amekwambia mjinga hana nafasi duniani? Mjinga mimi nafasi ninayo na nitaendelea hadi hapo Muumba wa mbingu na ardhi atakapochukua pumzi yake.
Kwa ujinga wangu huu huu na akili yangu ndogo, jana nimepata nafasi ya kufuatilia mkutano kati ya Mkuu wa Mkoa (jina nimelisahau) ambao ameuitisha kwa ajili ya kuzungumza na watendaji wake na wakuu wa wilaya. Kwa ujinga wangu sikumbuki hata ilikuwa mkoa gani. Ila nilikuwa nasikiliza tu.
Ukweli ni kwamba licha ya ujinga wangu, kuna baadhi ya kauli ambazo zimenifurahisha kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huyo. Kwa mfano, wakati anazungumza na watendaji na wakuu wa wilaya ya mkoa wake huo akazungumzia ushirikiano ili kufanikisha miradi ya maendeleo.
Hongera, kauli za kushirikiana ni za msingi sana mahali popote iwe kazini, iwe nyumbani, iwe mtaani, iwe kwenye mambo ya familia na kokote kule lazima ushirikiano uwepo.
Kote ambako wamefanikiwa, msingi wake ni ushirikiano. Ndio maana hata katika ngazi ya familia tunaambiwa kwenye maendeleo ya mwanaume nyuma yake kuna mwanamke. Huo ndio ukweli na maana yake mume na mke wanashirikiana vema.
Hivyo, Mkuu wa Mkoa alipozungumzia ushirikiano kwanza ikanipa faraja, pili ikanipa matumaini sasa baada ya kikao hicho watendaji, wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa watakuwa wamoja na kushirikiana. Narudia tena hongera kwa kukumbusha ushirikiano.
Kwa ujinga wangu wakati naendelea kupongeza kauli ya ushirikiano, ghafla masikio yangu yakasikia tena kauli nyingine. Hii sasa inahusu kuhujumiwa. Mkuu wa Mkoa anasema anahujumiwa sana. Kuna watendaji na viongozi wa kisiasa ndani ya Mkoa wake wamekuwa sehemu ya kukwamisha mambo.
Nikawa nawaza nani anamhujumu Mkuu wa Mkoa? Kwanini anahujumiwa? Wanamhujumu wanataka kupata nini baada ya hujuma zao kufanikiwa? Kuna tatizo kati ya Mkuu wa Mkoa na watendaji wake au wakuu wa mikoa?
Kwa ujinga wangu nikawa naendelea kuwaza na kujiuliza mawali ya kijinga. Eti nawaza najiuliza kwa nini Mkuu wa Mkoa ahujumiwe na wanaomhujumu hawana wasiwasi. Hivi kukwama kwa miradi ya maendeleo katika Mkoa huo ni sababu za hujuma?
Katika maswali yooooote hayo nimekosa majibu ya moja kwa moja. Kwa bahati mbaya ujinga nilionao ninaweza kuuliza tu maswali lakini kupata majibu siwezi. Iko siku nitakuwa na akili timamu iliyochanganyika na elimu nitakuwa na majibu.
Hata hivyo, katika mazingira ya kawaida sikutaratajia watendaji (si wote) na wakuu wa wilaya (nao si wote) kufanya hujuma kwa Mkuu wa Mkoa. Ukweli maendeleo ya Mkoa wenu na kufanikisha kila lililo ndani ya mikakati yenu ni jukumu letu sote.
Natambua mamlaka ya Mkuu wa Mkoa, natambua mamlaka ya wakuu wa wilaya na wakati huo huo natambua nafasi ya watendaji kila mmoja kwa nafasi yake na majukumu yake. Ili mambo yaende lazima muwe wamoja.
Katika maisha ya dhana ya kuhujumiana ukweli nawaambia hamtafika. Mtakuwa na vikao vya kila mara kujadiliana nani anamhujumu nani. Hata hivyo, huu ni ujinga wangu tu.
Wakati naendelea kuwaza ujinga eti nimetamani na kikombe cha chai rangi ambacho ndani yake kuna harufu ya hiliki. Achana na habari ya kikombe cha chai.
Naomba nieleze kitu hapa kidogo. Tena weka akilini, kweli nawaza ujinga lakini kuna wakati akili inakaa sawa. Hapa naona angalau akili imetulia. Hivyo hiki ambacho nitaandika nacho weka akilini. Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nyote ni wateule wa rais, nyote mnajenga nchi moja na nyote ni Watanzania.
Msikubali kutenganishwa na hizo nafasi, kwamba nani mkubwa nani mdogo dhidi yangu. Unachotakiwa kuweka kichwani mmepata nafasi hiyo kwa lengo la kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo. Nchi yetu inapiga hatua.
Ndiyo maana halisi, tabia ya baadhi ya wakuu wa wilaya kuwadharau wakuu wa mikoa si sahihi hata kidogo. Mkuu wa Wilaya unayo nafasi ya kutambua nafasi yako na majukumu yako kimamlaka. Huo ndio ukweli. Mnayo nafasi ya kusikiliza na kupokea maagizo ya Mkuu wa Mkoa ilimradi yawe yanaheshimu Katiba, utu na utanzania wetu.
Vivyo hivyo kwa wakuu wa mikoa nanyi mnayo nafasi ya kuheshimu wakuu wa wilaya. Bila wao Mkuu wa Mkoa si chochote wala si lolote. Unakuwa Mkuu wa Mkoa kwa sababu kuna wakuu wa Wilaya ambazo kwa pamoja zinaunganisha Mkoa wenu.
Hivyo, wakuu wa mikoa mkijiona ninyi ni zaidi ya wakuu wa wilaya mtakosea.Tena mtakosea sana. Fuatilia kote ambako kuna kutoelewana kati ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya mambo hayaendi.
Ukitaka kuthibitisha hilo muulize Waziri Mkuu Kassim Majaliwa atakwambia.Tena hivi karibuni alikuwa Mkoa wa Morogoro. Amekuta na mauza mauza huko.
Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi picha haziendi. Kila mmoja anafanya mambo yake kwa namna anavyotoka.
Mkuu wa Mkoa ukijiona uko juu sana kuliko wengine kwenye mkoa wako, lazima kuna mahali mtatofautiana na hapo ndipo mtaanza kutafutana uchawi. Badilikeni, kuweni kitu kimoja kwa maslahi ya nchi yetu na wananchi wake.
Ngoja nirudi kwenye kuwaza ujinga, iko hivi kwa akili yangu hii ya kijinga nikiri nimekuwa nikifuatilia kwa karibu baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Nilichojifunza kuna wakati aidha wakuu wa wilaya au wakuu wa mikoa kila mmoja anatafuta sifa binafsi badala ya sifa ya pamoja katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Hili la kila mmoja kutafuta sifa ndipo changamoto inapoanzia. Ndio maana inakuwa rahisi miradi kukwama. Maana huyu anadhani hili likifanikiwa basi sifa itakwenda kwa fulani. Japo huu ni ujinga lakini nashauri jengeni tabia ya kutafuta sifa ya pamoja kama mnadhani sifa zina umuhimu katika maisha ya leo.
Kama kuna mradi wa maendeleo wote muwe wamoja, zungumzeni kauli moja ambayo mtaona ndio chachu ya mafanikio yenu. Kinyume na hapo mtabaki mkinyoosheana vidole. Kuna mikoa inaleta raha. Watu hawana maneno zaidi ya kuchapa kazi kwa uadilifu na uaminifu. Hongereni mlioko kwenye mikoa hiyo.
Wale wanaobaki kujibizana na kurushiana maneno wasiwape tabu. Iko siku tena si nyingi watakuwa wamoja tu na kuchapa kazi. Maana angalau wanaweza kuitana na kuambiana ukweli.
Pamoja na yote hayo bado naamini kuwa rais wangu mpenda Dk. John Magufuli amewapa nafasi hizo kwa kuamini mtatekeleza yale yote ambayo amewaagiza. Mtatekeleza ambayo mnakubaliana katika Mkoa au Wilaya zenu.
Nimekumbuka kitu. Wakuu wa Wilaya (si wote) acheni dharau na kiburi. Kuna mambo mengi yanakwama na mnashindwa kufanikisha kwa sababu tu ya dharau mlizonazo kisha mnachanganya na kiburi.
Sijui kiburi kinatokana na nini au ndio cheo tena. Yetu macho tu. Mjifunze kama unataka kuheshimiwa lazima uheshimu waliopo au wanaokuzunguka. Kama unataka kufanikisha shirikiana na wenzako kufanikisha. Kama unataka usilete kiburi basi nawe acha kiburi.
Na kwa wakuu wa mikoa, nanyi naomba niwaambie hivi mamlaka mliyonayo ni makubwa katika ngazi ya mkoa. Tumieni mamlaka hayo vizuri. Mamlaka hayo yasiwe fimbo kwa walio chini yenu.
Mamlaka mliyonayo yasiwatie kiburi na kujenga dharau. Mamlaka mliyonayo yasiwe sehemu ya kujiona mnaweza kufanya chochote na kwa yoyote.
Pamoja na mamlaka yenu jitahidi kuheshimu wengine. waheshimu mliowakuta kwenye utumishi, wahehimu waliowakuta ofisini.
Waheshimu wananchi wenu na kubwa zaidi heshimu mawazo ya wengine. Unaweza kuwa kwenye nafasi lakini baadhi ya maamuzi yako yakawa si sahihi. Ukipingwa kubali, rekebisha kisha songa mbele.
Ukweli nawaambieni kuna wakuu wa mikoa ni hazina kwa taifa letu na wakuu wa mikoa hao lazima washikiliwe kwa mikono miwili. Najua pia wakuu wa mikoa hao ambao ni hazina kwa nchi wana kasoro ndogo ndogo ambazo zikifanyiwa kazi hakika sina shaka kabisa na utumishi wao. Waache sifa, waache dharau. waache kujiona wao ndio kila kitu na hakuna zaidi yao.
Nihitimishe kwa kueleza tu, yooote hayo ambayo nimeandika ni ujinga.Tena ujinga ambao unapaswa kupuuzwa na hauna sababu ya kuweka akilini. Iko siku nikiwa na akili nitaandika mambo ya msingi kwa ajili ya nchi yangu kama ambavyo wanafanya wengine.
Angalizo; ujinga wangu una nia njema, isitafsiriwe vibaya. Sina ugomvi na mtu. Najua mamlaka ya Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa. Ndio wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, aidha ya Wilaya au ya Mkoa. Nitafurahi nikibaki kuwa rafiki badala ya kuwa adui. Nitaishi wapi mie maisha yenyewe ndio haya pangu pakavu tia mchuzi.
Mie ambaye nimepewa akili tu za kuvukia barabara naomba mniache, maana si amri yangu. Naamini nitakuwa sawa. Hata hivyo, kwa kumaliza jambo linalonipa faraja nchi yangu iko kwenye mikono salama ya Rais wangu Dk. John Magufuli.
Hapa sasa kwa akili zangu timamu naomba niseme hivi mwakani ni Uchaguzi Mkuu, na kupiga kura ni siri ya mpiga kura. Hata hivyo kura yangu sitaki iwe siri tena.
Kwanini iwe siri wakati yanayofanywa na Rais Magufuli nayaona tena kwa macho. Kura yangu katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 inakwenda kwa Rais Magufuli.
Iko siku nitaeleza kwa nini kura yangu kwa Rais Magufuli. Kubwa tuombe uzima tu. Nakukumbusha ujinga ambao nimeuandika achana nao kabisa. Tubaki kujadili mambo ya maana.
Mwisho kabisa kabisa maandiko ya vitabu vitakatifu yanasema; Neno lililooza lisitoke kinywani mwenu, bali neno lolote ambalo ni jema kwa ajili ya kujenga -Kitabu cha WAEFESO 4:29
Simu 0713833822.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...