Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Zoezi la uthamini kulipa fidia kwa wananchi wa Nyamongo wilaya ya
Tarime mkoa wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu North Mara kwa
ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Taka limekumbwa na changamoto
kufuatia baadhi ya wananchi kujenga nyumba ama kuongeza sehemu za
nyumba zao maarufu kama ‘Tegesha’ ili kujipatia faida kupitia thamani
ya fidia.
Wathamni katika zoezi hilo walibaini tofauti kubwa katika uthamini
walioufanya awali na pale walipoenda kwa mara ya pili kwa ajili ya
uhakiki ambapo ilibainika baadhi ya vyumba katika nyumba zilizofanyiwa
uthamini kuwa wazi baada ya waliokuwa wakiishi kuondoka baada ya
kuthaminiwa.
Imeelezwa kuwa lengo wananchi wanaofanya ujanja wa ‘Tegesha’ ni
kujipatia posho ya makazi ambayo kwa kawaida hutolewa kama fidia kwa
wamiliki kulingana na idadi ya vyumba kwenye nyumba ya mmiliki.
Kwa mujibu wa Wathamini wa zoezi hilo, mbali na wamiliki walioathirika
na zoezi hilo kulipwa gharama nyingine kama vile nyumba na mazao pia
hulipwa posho ya makazi kwa kipindi cha miezi 36 lengo kumuwezesha
mpangaji kupata mahali pa kuishi kabla ya kuanza zoezi la kuondolewa.
Mwandishi wa Gazeti hili alishuhudi moja ya nyumba iliyopo kitongoji
cha Kigonga A katika kijiji cha Matongo ikiwa na vyumba ishirini na
moja wakati nyumba hiyo ilistahili kuwa na vyumba vitatu na baadhi ya
vyumba havina hata madirisha.
Mthamni Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha ambaye alitembelea baadhi ya
nyumba hizo kukagua maendeleo ya kazi ya uthamini katika eneo hilo
aliweka wazi kuwa Ofisi yake inafanya kazi kwa kufuata sheria ya
Uthamini na hatua kali zitachukuliwa kwa mtu atakayeonekana kufanya
udanganyifu kwa kwa lengo la kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Mugasha, zoezi la uthamini katika eneo la Nyamongo
linalohusisha vitongoji vitatu katika kijiji cha Matongo limekuwa
likifanyika kwa uwazi na kushirikisha pande zote wakati wa kuorodhesha
mali na kufafanua kuwa hata mwananchi asiyeridhika na uthamini katika
eneo lake hupewa fomu maalum ya kujaza lengo likiwa kutoa haki.
‘’Tumeona watu walihamisha magodoro, vitanda na mizigo mingine lengo
ni kupata posho ya makazi ili kujipatia faida na cha kushangaza baadhi
ya wapangaji hawajui hata choo cha nyumba wanayoishi kilipo, ofisi
yangu haitavumilia vitendo hivyo kila mtu atalipwa anachostahili’’
alisema Mugasha.
Mthamini kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Lazaro Magumba
alieleza kuwa wakati zoezi la uthamini kumekuwa na changamoto hasa
wakati wa kukagua mali za wananchi kutokana na baadhi yao kuwa na
dhana ya kujipatia utajiri kupitia mradi huo ambapo hufanya maendelezo
ya kuegesha maarufu kama ‘tegesha’ ili kulipwa fedha nyingi.
‘’ Wananchi wanajenga nyumba zilizopangana na hakuna hata nafasi na
wakati wa uthamni usiku kucha watu wanahamisha vyombo, magodoro na
wengine hata wanyama ili ionekane ni makazi halali’’ alisema Lazaro.
Alisema wanachokifanya wao ni kukagua kwa awamu kwa lengo la
kujiridhisha kama kweli walionekana wakati wa uthamini kama ni wakazi
halali ama walienda kutegesha.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Matongo wilayani Tarime mkoa wa Mara
ambao hawakupenda majina yao yawekwe wazi kutokana na sababu za
kiusalama walikiri kuwepo mchezo huo wa Tegesha lakini walidai
hufanywa na watu wasio wakazi wa muda mrefu katika kijiji hicho bali
walienda kwa lengo la kujipatia faida kupitia zoezi hilo.
Kwa mujibu wa wakazi hao, baadhi ya wananchi kutoka nje ya kijiji
hicho walinunua nyumba ama maeneo kwa wenyeji na kuongeza vyumba na
kuwakodisha watu kuishi ili kuvizia zoezi la uthamini wa fidia wapate
faida.
Kwa muda mrefu wananchi wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa
wale wanaoishi vitongoji vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
wamekuwa wakilalamikia uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja
kutoka Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri afya zao jambo
lililomlazimu Rais John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake katika
eneo hilo kuagiza kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akiwa katika chumba kilichojengwa maarufu kama Tegesha katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akionesha moja ya chumba kilichojengwa maarufu kama Tegesha katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa Dhahabu wa North Mara ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi.
Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha (Wa pili kushoto)
akiongozana na timu ya uthamini katika kijiji cha Matongo wilaya ya
Tarime mkoa wa Mara wakati akikagua kazi ya uthamini wa fidia
inayofanywa na Ofisi yake katika eneo la Nyamongo kupanua mgodi wa
Dhahabu wa North Mara ili kupisha ujenzi wa bwawa la maji taka juzi.
(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...