Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
IMEELEZWA kuwa watu wapatao laki nane duniani hupoteza maisha kwa kujiua kunakosababishwa na matatizo mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo, matumizi ya pombe na dawa za kulevya pamoja na kukaa na magonjwa sugu kwa muda mrefu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Daktari bingwa wa afya ya magonjwa akili kutoka hospitali ya taifa Muhimbili Praxeda Swai amesema kuwa shirika la afya duniani (WHO) limekuja na kauli mbiu ya kuzuia matukio ya kujiua na hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo kote duniani.
"Kila mwaka duniani kote watu laki nane hupoteza maisha kwa kujiua wakitumia njia hatarishi na kufanya kati ya vifo laki moja vifo kumi na mbili hutokana na kujiua kwa mwaka" ameeleza Praxeda.
Aidha amesema kuwa kwa sekunde 40 mtu mmoja hupoteza maisha kwa kujiua na kwa saa moja pekee watu 90 hupoteza maisha kwa kujiua wakiwa wamedhamiria licha ya wengine kuokolewa.
Akieleza sababu ya watu kujiua Dkt. Praxeda amesema kuwa matatizo msongo wa mawazo, kuishi na magonjwa sugu, matumizi ya pombe na dawa za kulevya huweza kumpelekea mtu kujiua huku akitolea mfano kuwa mtu akiwa amelewa hakuna kitu kinachomzuia kufanya chochote.
Kuhusiana na wimbi la watoto wenye umri mdogo kujiua amesema kuwa;
" Wimbi la watoto wadogo kujiua husababishwa na kutekelezwa, kunyanyasika kingono, kiakili, kimwili, kutosikilizwa katika familia pamoja na kunyanyaswa na watoto wenzao hali inayowapelekea kushindwa kuhimili misongo hiyo na kuamua kujiua" ameeleza.
Ameeleza kuwa viashiria vya mtu kutaka kujiua ni pamoja na kufanya majaribio ya kutaka kujiua kama vile kujikata kwa wembe, vyupa na kisu na hata kutuma jumbe za kukata tamaa, kuaga watu wake wa karibu, kugawa mali au vitu anavyomiliki pamoja na kuandika wosia na amewashauri wanajamii kushiriki kukomesha suala hilo kwa kuongea na watu wenye viashiria hivyo pamoja na kuonesha upendo kwao.
Kwa upande wake Msaikolojia tiba na mwenyekiti wa chama Cha wataalamu wa afya ya akili (MEHATA) Dkt. Isaack Lema amesema kuwa wameendelea kuhamasisha wanajamii kuhusiana afya ya akili ili kujenga ustawi wa kutambua na kukabiliana na msongo wa mawazo, kufanya maamuzi na kufurahia maisha.
"Kati ya watu wanne mmoja ana tatizo la akili na kama kunafanyika mawasiliano baina yao hayatafanikiwa kwa kuwa mmoja ana tatizo la akili, na pia katika wafanyakazi watano mmoja ana tatizo la akili hivyo lazima jamii itambue kuwa suala la afya ya akili ni la watu wote." Ameeleza.
Vilevile amesema kuwa vifo vya vijana wa kati ya miaka 15 hadi 29 sababu ya kujiua hushika nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikiwa ni ajali huku sababu vifo kwa wazee wa miaka 75 na kuendelea sababu ya kujiua imeendelea kuwa juu.
Amesema kuwa afya ya akili ni kwa watu wote na mpango wa kuzuia kutokea kwa matukio ya kujiua unaofanywa na hospitali ya taifa Muhimbili, Chama cha wataalamu wa afya ya akili (MEHATA) na sekta nyingine utafanikiwa kwa kushirikiana na wanajamii hasa kwa kuwaunganisha na huduma watu wenye viashiria vya kutaka kujiua.
Msaikolojia tiba na mwenyekiti wa chama Cha wataalamu wa afya ya akili
Dkt. Isaack Lema akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mpango
wa kupambana na vitendo kujiua ambapo amesema kuwa jamii ishiriki
kuwasaidia watu wenye viashiria vya kutaka kujiua kwa kuwaunganisha na
huduma katika hospitali kote nchini, leo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa afya ya magonjwa ya akili Praxeda Swai akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na wimbi la watu kujiua kunakosababishwa na matatizo mbalimbali ikiwemo msongo wa mawazo ambapo amewashauri wanajamii kushiriki kuwasaidia watu wenye viashiria vinavyopelekea kujiua, leo jijini Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...