Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
LEO Oktoba mosi taasisi isiyo ya kiserikali ya Bright Jamii Iniatives kwa kushirikiana  na taasisi ya Plan International wamezindua na kupitia ripoti ya ulinzi wa mtoto wa kike katika kazi za sanaa ikiwa ni katika kuelekea maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike inayofanyika Oktoba 11 kila mwaka.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi wa taasisi ya Bright Jamii Iniatives Irene Fugara amesema kuwa, mtoto anapaswa kulindwa kwenye  kazi za sanaa na hiyo ni kwa kupitia kazi  mbalimbali ambazo wasanii wa muziki na filamu huzitengeneza kwa kuangalia maudhui kwa jamii lengwa.

" Maadili ni muhimu sana katika kujenga kizazi bora cha baadaye, ni vyema kazi zetu za sanaa zikazingatia maadili na utamaduni kama wanavyofanya nchi za wenzetu" ameeleza.

Vilevile amesema kuwa sanaa lazima  iepushe ukatili dhidi ya watoto pindi wanaposhiriki shughuli mbalimbali za kisanaa;

"Kumekuwa na matamasha mbalimbali ambayo huwakutanisha watoto lakini kwa namna wanavyochezeshwa nyimbo ni kinyume na maadili ya kitanzania kabisa hivyo ni vyema wazazi, walezi na jamii kwa ujumla tukashiriki katika kuhakikisha utu wa mtoto unalindwa" ameeleza.

Aidha amewashauri wasanii kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili bila kuyumbishwa na teknolojia kutoa nje;

"Ukiwa unamkimbiza mtu ni vyema ukafahamu anapoelekea tusiyumbishwe na tamaduni za nje na kuzikimbilia tudumishe maadili yetu kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa miradi kutoka taasisi ya Plan International Dkt.Benatus Sambili amesema kuwa ripoti hizo mbili zilizozinduliwa leo zimefanyika kimataifa na nchini zimefanyika katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam na zimeonesha hali ya mtoto wa kike na mwanamke katika nyanja mbalimbali.

Sambili amesema kuwa kati ya ripoti hizo mbili, ripoti moja ilifanyika kimataifa kwa kuangalia hali ya wanawake pamoja na nafasi yao katika sanaa na vyombo vya habari na ripoti nyingine ilifanyika nchini na kuangalia ulinzi wa mtoto katika sanaa ya muziki na filamu.

Amesema kuwa taasisi hizo mbili zitaendelea kushirikiana katika kutetea haki za watoto katika njanja mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kisiasa na utamaduni.

 Mkurugenzi wa miradi wa taasisi ya Bright Jamii Iniatives Godwin Mongi amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na kasi ya  mmomonyoko wa maadili kunakochangiwa na maendeleo ya teknolojia ambayo kwa kiasi kikubwa maudhui yatokanayo huwaathiri watoto kwa kiasi kikubwa.

Amesema kuwa baadhi ya wazazi wameshindwa kuwaandaa vyema watoto pindi wanapoingia kwenye kazi za sanaa kwa kufuata miiko ya maadili na tamaduni hivyo wakaona ni vyema kuwakutanisha wadau wa filamu,  muziki watayarishaji wa filamu na muziki, vyombo vya habari na watoto ili kuweza kutoka na sauti moja inayoipa thamani sanaa na yenye mlengo wa kuipeleka mbele zaidi na kuweza kuajiri vijana wengi zaidi.

"Kupitia kikao hiki tunategemea kuokoa vijana wengi kupitia sanaa na kuwokoa vijana wengi ambapo wanajiingiza kwenye tabia hatarishi ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya, na tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa sanaa, serikali na vyombo vya habari ili kuweza kufikia azma" ameeleza.

Vilevile amesema kuwa kazi nyingi sanaa zimetengeneza mtazamo hasi ambayo mara nyingi huwaathiri watoto kimwelekeo;

"Katika tafiti tulizozifanya katika Mikoa ya Mwanza na Arusha baadhi ya watoto wamekuwa wakiamini ukiwa msanii unapata mafanikio ya haraka na kwa muda mfupi na hiyo ni kutokana na maudhui yanayotawala kazi nyingi za sanaa jambo ambalo sisi kama wadau lazima tutoe elimu zaidi kuhusiana na mwenendo wa sanaa nchini" amesema.

Mwakilishi wa wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo Habibu Msami amezipongeza taasisi hizo kwa kufanya jambo hilo muhimu na kueleza kuwa kuna watu wanapotosha maudhui na kuleta mmomonyoko wa maadili jambo ambalo si jema na serikali haziwezi kulivumilia.

Amesema kuwa msanii yeyote atakayejaribu kulibadilisha taifa katika mfumo ambao ni kinyume na maadili, mila na tamaduni atafungiwa kufanya kazi za sanaa.

"Sanaa ichukuliwe ni chombo cha kuelimisha licha ya mambo kubadilika lazima wasanii wafahamu ni nini wanataka kufanya kwa jamii, wasiingie kichwa kichwa na kuharibu mfumo wa jamii" ameeleza.
 Mkurugenzi wa taasisi ya Bright Jamii Iniatives Irene Fugara akizungumza katika kikao kazi na  kupitia ripoti ya ulinzi wa mtoto wa kike katika kazi za sanaa kilichowashirikisha wadau mbalimbali ambapo ameeleza kuwa maadili ni nyenzo muhimu katika kujenga kizazi bora, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa miradi wa taasisi ya Bright Jamii Iniatives Godwin Mongi akizungumza wakati wa mkutano huo na kueleza kuwa kumekuwa na kasi ya mmomonyoko wa maadili yanayochagizwa na utandawazi, leo jijini Dar es Salaam.
 Mkurugenzi wa miradi wa Taasisi ya Plan International Benatus Sambili akizungumza katika mkutano huo ambapo amesema kuwa sanaa iheshimiwe na kuelimisha jamii, leo jijini Dar es Salaam.
 Msanii wa kizazi kipya kipya Kala Jeremiah akiwasilisha mapendekezo katika mkutano huo ambapo amesema kuwa jamii nzima lazima iendelee kudumisha mila, desturi na utamaduni, leo jijini Dar es Salaam. 
 Mkurugenzi wa taasisi ya Bright Jamii Iniatives Irene Fugara akizungumza akichangia mada  katika kikao kazi na kupitia ripoti ya ulinzi wa mtoto wa kike katika kazi za sanaa kilichowashirikisha wadau mbalimbali uliofanyika katika hoteli ya Serena  leo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mjadala.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...