Charles James, Michuzi TV

KATIKA kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kutoa elimu bure Chama cha Walimu Nchini (CWT) kimekabidhi mifuko 300 ya Saruji yenye thamani ya Shilingi Milioni Nne kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Makabidhiano ya mifuko hiyo yamefanyika baina ya Meya wa Jiji la Dodoma, Prof David Mwamfupe na Katibu Mkuu wa CWT, Deus Seif.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa mifuko hiyo, Prof Mwamfupe ameipongeza CWT kwa kuunga mkono juhudi za kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia Mapinduzi ya elimu huku akitoa wito kwa mashirika na taasisi nyingine kuiga mfano huo.

Amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imefanya kazi kubwa katika nyanja mbalimbali na haswa elimu hivyo ni jukumu la kila mmoja mwenye uchungu wa maendeleo kuhakikisha anatoa mchango wake katika kuboresha sekta ya elimu.

" Rais anafanya kazi kubwa sana. Watu wengi wanafikiri ni jukumu la Serikali kufanya kila kitu. Hayo ni mawazo hasi suala la ukuaji wa Nchi ni jukumu letu sote. CWT mmeonesha mwanga naamini kila mmoja ataiga mfano huu.

" Hakuna maendeleo kwenye sekta yoyote kama hatutotilia mkazo elimu. Mazingira bora kwa walimu na wanafunzi ndio yanayoleta matokeo chanya katika sekta hii muhimu. Tuungane katika kuboresha sekta hii ambayo kila mmoja wetu amekua akifaidika nayo," Amesema Prof Mwamfupe.

Mstahiki Meya huyo amesema Jiji la Dodoma limetenga bajeti ya Shilingi Bilioni Nane katika kuhakikisha linafanya Mapinduzi ya elimu ikiwa ni pamoja na kujenga vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.

" Tunafahamu changamoto ya uhaba wa walimu katika Jiji letu na kwa kujua umuhimu wa elimu sisi hatutosubiri walimu watakaoajiriwa na Serikali. Tumejinga kuajiri walimu kwa fedha zetu za ndani hasa katika masomo ya Sayansi. Lengo letu ni kukuza elimu katika Jiji la Dodoma na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wetu," Amesema Prof Mwamfupe.

Aidha Mstahiki Meya ameungana na CWT kwa kuahidi nae kutoa mifuko 10 ya saruji huku pia Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwinyi Kata ya Iyumbu, Elias Richard akitoa mifuko mitano.

Kwa upande wake Katibu wa CWT Taifa, Deus Seif amesema wao kama walimu wanafahamu changamoto iliyopo kwenye elimu hasa katika vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.Amesema wao kama CWT wataendelea kushirikiana na wadau wa elimu ili kukuza kiwango cha elimu nchini.

" Sisi tunaamini miundombinu ya vyumba vya madarasa, nyumba za walimu zilizo karibu na shule na vyoo vinachangia sana ukuaji wa elimu na kuongeza kiwango cha ufaulu.

" Kwa hiyo sisi Mhe Meya tunatoa hii mifuko 300 ili tuwe sehemu kidogo cha ukuaji wa elimu ya Dodoma. Tunafahamu kuna changamoto ya vyumba kwa asilimia 60 hivyo sisi tunahitaji angalau mchango wetu usaidie hata ujenzi wa msingi tu," Amesema Seif.

Pia amewataka wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali katika kutekeleza sera ya elimu bure na kuahidi wao kama CWT hawatochoka kutoa mchango yao.
 Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof David Mwamfupe (kulia) akipokea mifuko 300 ya Saruji kutoka kwa Katibu wa Chama cha Walimu Nchini (CWT), Deus Seif.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof David Mwamfupe akizungumza wakati akipokea mifuko 300 ya Saruji kutoka kwa Chama cha Walimu Nchini jijini Dodoma leo.

 Meya wa Jiji la Dodoma, Prof David Mwamfupe akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa CWT wakiongozwa na Katibu wa Chama hicho, Deus Seif.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...