TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema
inawashikilia viongozi 99 wa vyama 10 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) pamoja na
kurejesha milioni 255,598,194.00 ikiwa ni utekelezaji wa agizo walilopewa na
Rais Dkt. John Pombe Joseph alilolitoa akiwa katika ziara ya kikazi katika Mkutano
wa Hadhara na Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa Mjini, mkoani Lindi.
Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi Rais Dkt Magufuli aliiagiza
TAKUKURU pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo na Ushiriki, Hussein Bashe, kuhakikisha
kuwa Vyama 10 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vinavyodaiwa na Wakulima
vinawalipa wakulima husika kabla ya msimu wa Korosho kuanza, vinginevyo
wahusika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa Sheria.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari leo
Oktoba 19, 2019, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John
Mbungo amesema ofisi yake imeshatekeleza agizo hilo la Rais kwa kuwakamata
Viongozi 99 wa Vyama 31 vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) vilivyowadhulumu
Wakulima wa Ufuta kiasi cha Sh. 1,236,364,075.00.
Amesema kiwango hicho
cha fedha wanachodaiwa kukidhulumu viongozi hao ni takribani mara tatu (3) ya
kiwango kilichobainika awali ambapo baada ya Viongozi hao kuhojiwa wamekubali
kulipa deni lote wanalodaiwa kabla ya kuisha kwa Mwaka 2019.
Brigedia Mbungo
amesema zoezi hilo litakuwa endelevu na halitokoma mpaka wahakikishe wakulima
wote wamelipwa stahili zao kwa mujibu wa Sheria na kwamba fedha zote
zilizorejeshwa kiasi cha Sh. 255,598,194.00 zimeshaanza kugawiwa kwa walengwa
ambao ni wakulima wa Ufuta kupitia kwa Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Lindi, Robert
Nsunza chini ya Usimamizi na uangalizi wa TAKUKURU.
Pia amesema katika zoezi la kurejesha fedha za wakulima,
Takukuru imekuwa ikitambua mali za watuhumiwa, kuzipiga picha na kuzikamata
mali za viongozi hao wa AMCOS ambazo zimekuwa zikidaiwa kama dhamana ya madeni
wanayodaiwa kwa wakati kama walivyoahidi ili kuziuza endapo watashindwa
kutimiza ahadi zao.
“Ili kuwathibitishia kuwa TAKUKURU haina utani katika zoezi
hili tunaendelea na zoezi la kutambua, kuzipiga picha na kukamata mali za
viongozi wa AMCOS zinazodaiwa kama dhamana ya madeni wanayodaiwa, na endapo
viongozi hao watashindwa kukamilisha malipo ya madeni wanayodaiwa kwa wakati
kama walivyoahidi kwa maandishi wao wenyewe kwa hiari yao basi mali husika
zitataifishwa kwa mujibu wa Sheria ili wakulima wa Ufuta wapewe fedha zao.
Aidha Brigedia Mbogo amewataka Viongozi wote wa Vyama vya
Ushirika nchini vinavyodaiwa na Wakulima viwalipe wakulima wao haraka
iwezekanavyo kabla TAKUKURU haijawafikia na kwamba katika zoezi hilo hakuna
chama cha ushirika kinachodaiwa ambacho kitabaki salama.
Amesema zoezi la ufuaitliaji wa malipo ya Wakulima kwa Vyama
vya Ushirika ni endelevu na pindi litakapokamilika Takukuru itatoa taarifa
kamili.
Amewataka wananchi wenye ushahidi wa dhuluma iliyofanywa kwa
wakulima wa ufuta ama kwa yeye mwenyewe kudhulumiwa au kuhujumiwa kwa namna
yoyote ile katika biashara ya Ufuta, wafike katika ofisi za TAKUKURU
zinazopatika katika Mikoa na Wilaya zote nchi nzima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...