Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akizungumza
na Afisa Mtendaji, Kata ya Kondoa Mjini Samson Mtui alipofika Ofisini kwake
kujitambulisha kabla ya kuanza ziara ya kukagua maendeleo na ubora wa kazi ya
kutenga maeneo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2022.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akitoa
maelekezo kwa timu ya warasimu ramani wanafanya kazi ya kutenga maeneo huko
wilayani Kondoa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2022
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa akisikiliza
maelezo kutoka kwa Mrasimu ramani Emmanuel Mahemba wakati wa ziara ya kukagua
kazi ya utengaji maeneo katika Mtaa wa Mnarani, Kata ya Kondoa Mjini mkoani
Dodoma. Kulia ni Mrasimu Ramani Galos
Mbedule.
Mkuu wa Kitengo cha Mfumo wa Taarifa za Kijiografia
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Benedict Mugambi akitoa maelezo namna maeneo ya
kuhesabia watu yanavyotengwa na taarifa za taarifa za kijiografia
zinavyokusanywa. Wengine ni warasimu ramani na kwa nyuma ni Meneja wa Takwimu
Mkoa wa Dodoama Iddi Mruke.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk. Albina Chuwa amesema
matumizi ya tekinolojia za kisasa zitaleta ufanisi mkubwa katika Sensa ya Watu
na Makazi ya Mwaka 2022 hivyo kuipatia nchi Takwimu za uhakika zaidi na kwa
wakati kuliko Sensa zilizopita.
Dk. Chuwa alieleza hayo jana wakati alipotembelea
wilaya ya Kondoa kukagua maendeleo na ubora wa kazi katika zoezi ya kutenga
maeneo katika mtaa wa Mnarani wilayani Kondoa ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
“Lengo letu ni kufanya Sensa ya Watu na Makazi ya
Mwaka 2022 kwa Ufanisi mkubwa na nimekuja hapa kukagua na kutathmini ubora wa
kazi ya kutenga maeneo katika wilaya yenu” Dk. Chuwa alimueleza Afisa Mtendaji,
Kata ya Kondoa Mjini Samson Mtui alipofika Ofisini kwake kujitambulisha.
Wakati wa ukaguzi huo Dk. Chuwa alioneshwa namna
maeneo hayo yanavyopimwa na kuwekewa mipaka pamoja na namna taarifa
zinavyohifadhiwa katika Kishikwabi (tablet) ambazo zitatumika wakati wa
kuhesabu watu tofauti na Sensa zilizopita ambapo Wadadisi walikuwa wakitumia
ramani zilizochorwa katika karatasi.
Mkuu wa Kitengo cha Mifumo ya Taarifa za Kijiografia
katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Benedict Mugambi alimueleza Mtakwimu
Mkuu kuwa kwa kutumia Kishikwambi Mdadisi atafanya kazi yake ya kuhesabu watu
katika eneo lake tu na hataweza kuingia eneo la mwenzake.
“Mdadisi akitoka nje ya eneo lake Kishikwambwi
kitamuonesha alama kuwa anaingia eneo silo lakini zaidi Dodoso halitaweza
kufunguka hivyo hataweza kufanya kazi” alieleza Mugambi.
Dk. Chuwa alibainisha kuwa matumizi hayo ya
tekinolojia yatapunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha watu wanaosahaulika kuhesabiwa
wakati wa zoezi la kuhesabu watu.Katika Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 kiwango
cha watu waliosahaulika kuhesabiwa kilikuwa asilimia 5 ambacho hata hivyo ni
cha chini ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.
Kwa mfano, katika Sensa iliyopita nchini Afrika Kusini
kiwango cha watu waliosahaulika kuhesabuwa kiliwa zaidi ya asilimia kumi.
“Tunataka kile
kiwango cha asilimia 5 cha waliosahauliwa kuhesabiwa mwaka 2012 kiondoke katika
Sensa ijayo ili tupate takwimu halisi na kuongeza ufanisi katika upangaji wa
mipango yetu ya maendeleo” Dk. Chuwa alisisitiza.
Awali, akitoa taarifa ya kazi, kiongozi wa timu hiyo
Mrasimu Ramani Jerve Gasto wa NBS alieleza kuwa hadi sasa vijiji vyote 84
katika Halmashauri ya Kondoa Vijijni tayari vimetengewa maeneo ya kuhesabia
watu na taarifa zote muhimu zimeshachukuliwa na kuweka katika ramani.
Kwa upande wa Halmashauri ya Kondoa Mjini, Gasto
alieleza kuwa kazi imeanza na wamekamilisha mtaa mmoja wa Mnarani kati ya mitaa
36 na kuongeza kuwa kazi hiyo inatarajiwa kumalizika baada ya siku kumi.
Kuhusu taarifa zilizokusanywa alieleza kuwa ni za
huduma za jamii kama elimu, maji na afya, shughuli za uzalishaji kama viwanda
na ofisi za serikali na huduma za kiroho.Gasto alieleza kuwa mwitikio wa wananchi ni mzuri na
wamekuwa wakiwapa ushirikiano wakati wote wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao
na kuwashukuru viongozi wa wilaya kwa kuwa nao bega kwa bega tangu walipoanza
kazi hiyo wilayani humo.
Hata hiyo alieleza kuna changamoto kadhaa
wanazopambana nazo wakiwa kazini ikiwemo baadhi ya wananchi kuingia katika
mapori ya hifadhi na utata wa mipaka katika baadhi ya vijiji.
Kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu wilayani
Kondoa ilianza tarehe 16 Septemba, 2019 na kushirikisha warasimu ramani kutoka
NBS, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS) na wataalamu wa mipango
miji kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Watalamu hao wamegawanyika katika timu tano zenye watu
watatu kila moja na kwa mujibu wa Gasto timu ya sita inatarajiwa kujiunga nao
sasa kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...