AFISA Tarafa Itiso  Wilayani Chamwino  Remidius Emmanuel ameahidi kutumia njia ya mazungumzo kama hatua ya kwanza kukabiliana na uharibifu wa Mazingira unaofanywa baadhi ya wananchi wachache kukata na kuchoma miti kwa ajili ya mkaa katika msitu wa hifadhi ya Chenene Mashariki /Magharibi (Mtungutu) katika eneo la Tarafa hiyo.

Hayo ameyasema leo alipotembelea na kuona uharibifu unaoendelea kufanyika katika hifadhi ya nsitu huo na kueleza kusikitishwa na kiwango kikubwa cha  ukataji wa miti na uchomaji wa mkaa unaoendelea kufanywa na wahalifu wa Mazingira.

" Natambua kazi kubwa  inayofanywa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, kwa kipindi kirefu wameendelea kukabiliana na wahalifu wote wa mazingira katika misitu hii.Nimeamua kushirikiana nao kwa nguvu zote kukomesha hali hii." Amesema.

"Nimeingia ndani ya msitu huu nimepata uchungu mkubwa kwa jinsi hali ilivyo, nimefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wananchi wanaokata miti na kuchoma mikaa licha ya wengine kukimbia, lakini nimewataka tufanye mazungumzo ya pamoja ili kuachana na shughuli hii, nimewaeleza nia yetu kushirikiana na TFS ya kuwapatia mizinga ya Nyuki ili wawe mabalozi wema kuhifadhi misitu hii na kuongeza kipato kwa shughuli halali tofauti na hiki kinachoendelea sasa. Ameeleza Remidius.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wanaojishughulisha na ukataji wa miti na kuchoma mkaa katika msitu huo, wamesema wamepata ujasiri wa kuzungumza na Afisa Tarafa huyo wakiwa na nia ya kuacha uharibifu huo na wanaiomba Serikali iwasaidie wapate hiyo mizinga ya Nyuki na shughuli mbalimbali zitakazowasaidia kupata kipato halali.

"Tunakiri kabisa kwamba sisi tumekuwa tukifanya uharibifu, wengine wamekimbia walipokuona, lakini ujumbe utawafikia wote, tuko tayari kufanya kikao na mazungumzo ya pamoja kuacha uharibifu huu lakini tunaomba mtusaidie tupate mahala pa kujipatia riziki" Alisema moja ya wananchi hao.

Afisa Tarafa Remidius amewataka wananchi hao kuacha uharibifu huo, na kwa pamoja wamekubali kufanya kikao na mazungumzo  wiki ijayo yatakayohusisha pia Meneja wa TFS Wilaya ya Chamwino, amesema mazungumzo hayo yatakuwa ya kirafiki na kwa hatua ya kwanza hakuna atakayekamatwa, wao wajitokeze kwa wingi ili Serikali ione njia mbadala ya kuwasaidia kiuchumi.

Kiongozi huyo aliyembatana na baadhi ya Wataalamu na Watendaji was vijiji vya  kata ya Haneti, amesema Kipaumbele cha Serikali ni kutaka jamii yenyewe kwanza ichukizwe na Uharibifu huo na kuelewa umuhimu wa Misitu hiyo na kueleza kuwa Serikali haijalala juu ya hilo na TFS  kwenye bajeti yake 2019/2020 imetenga fedha kwa ajili ya kujenga ranger Posts kuzunguka misitu hiyo na mipango ipo ya kushirikiana na SUMA JKT katika ulinzi wa Misitu hiyo.
 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akitizama mti uliokatwa na wahalifu wa Mazingira  ndani kabisa ya msitu wa Mtungutu (Chenene Mashariki)
 fisa Tarafa Itiso akiwa na uwakilishi wa baadhi ya wananchi wanaojishughulisha na uharibifu wa mazingira katika msitu wa Mtungutu (Chenene Mashariki), Wananchi hao wamekubali kufikisha ujumbe kwa wenzao ili yafanyike mazungumzo ya pamoja na Serikali kwa lengo la kuachana na uharibifu huo na Serikali kupitia TFS itaona namna ya kuwawezesha mizinga ya nyuki ili wapate kipato kwa shughuli halali.
 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akitizama eneo ambalo shughuli za Uchomaji wa Mkaa zimefanyika ndani kabisa ya msitu wa Mtungutu (Chenene Mashariki)
 Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel akiendelea kujionea uharibifu wa Mazingira  ndani  msitu wa Mtungutu (Chenene Mashariki)
Moja ya Wananchi waliombatana na Afisa Tarafa  ndugu Shabani  Temaunji mkazi wa Kijiji cha Chenene (Tarafa ya Itiso) akionyesha eneo ambalo limeharibiwa kutokana na uharibifu wa Mazingira katika Msitu wa Mtungutu. 
 Maeneo ambayo shughuli za uchomaji wa mkaa zimefanyika ndani ya Msitu wa Hifadhi ya Chenene Mashariki (Mtungutu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...