Na Veronica Kazimoto,Simiyu
Wafanyabiashara nchini
wameshauriwa kutunza kumbukumbu za biashara zao ili kulipa kodi stahiki na
hatimaye kupunguza kero ya madai yao kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
inawakadiria kodi kubwa isiyoendana na uhalisia wa biashara wanazofanya.
Akizungumza wakati wa
semina ya wafanyabiashara hao iliyofanyika Wilaya ya Busega mkoani Simiyu,
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka mamlaka hiyo Diana Masalla, amesema kuwa,
wafanyabiashara walio wengi hawana tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zao
suala linalosababisha malalamiko mengi baada ya kukadiriwa kodi na TRA.
“Ndugu zangu
wafanyabiashara sote tunajua kwamba, mali bila daftari hupotea bila habari
hivyo basi, niwaombe mjenge tabia ya kutunza kumbukumbu za biashara zenu siyo
tu kwa ajili ya TRA lakini pia kwa ajili yenu wenyewe kwani mtaweza kujua kama
biashara zenu zinakua au zinashuka lakini pia mtaweza kupanga bajeti za mauzo
na manunuzi yenu vizuri na mwisho wake mtalipa kodi stahiki na kuchangia
maendeleo ya nchi yetu,” amesema Masalla.
Masalla ameongeza kuwa,
kuna tofauti kubwa kati ya mfanyabiashara anayetunza kumbukumbu na yule
asiyetunza kumbukumbu kwani asiyetunza kumbukumbu kwa mauzo ya shilingi milioni
14 atalipa kodi shilingi 450,000 kwa mwaka wakati anayetunza kumbukumbu kwa
mauzo hayo atalipa shilingi 320,000 kwa mwaka.
“Tukichukulia mfano wa
wafanyabiashara wawili wenye mauzo ya shilingi milioni 14, lakini mmoja
anatunza kumbukumbu na mwingine hatunzi kumbukumbu tunaona kwamba, kuna tofauti
ya shilingi 130,000 kwa kuwa asiyetunza atalipa shilingi 450,000 na anayetunza
kumbukumbu atalipa shilingi 320,000. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kutunza kumbukumbu,”
amesisitiza Masalla.
Meneja huyo wa Elimu
kwa Mlipakodi amewaambia wafanyabiashara hao kuwa, nyenzo muhimu inayosaidia
utunzaji wa kumbukumbu ni pamoja na Mashine ya Kielektroniki ya Kutolea Risiti
(EFD) na kama mfanyabiashara hajafikia mauzo ya kutumia mashine ya EFD ambayo
ni chini ya shilingi milioni 14 anashauriwa kutumia kitabu cha risiti za
kuandika kwa mkono ambapo mfanyabiashara atakwenda na kumbukumbu hizo TRA kwa
ajili ya kukadiriwa kodi.
Kwa upande wake
mfanyabiashara wa mbao wilayani humo, Zakaria Manyilizu amesema kuwa, elimu
aliyoipata ya utunzaji kumbukumbu za biashara ni nzuri hata hivyo ameiomba TRA
kutoa elimu juu ya namna ya kutumia mashine za EFD kwani walio wengi hawana
utalaamu wa kutumia mashine hizo.
“Kwa kweli
tunaishukuru TRA kwa kutuletea elimu hii ya utunzaji wa kumbukumbu hapa
wilayani Busega lakini sisi tulio wengi hatujui kutumia vizuri mashine za EFD
hivyo ninaiomba TRA itufundishe namna ya kutumia mashine hizi ili na sisi
tunufaike na faida za utunzaji kumbukumbu alizozieleza meneja wa TRA,” alisema
Manyilizu.
Timu ya Maofisa wa
kodi wakiongozwa na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi Diana Masalla kutoka Mamlaka
ya Mapato Tanzania wako Mkoani Simiyu katika Wilaya ya Busega na Bariadi ambapo
wanakutana na wafanyabiashara mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya kodi ikiwa
ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla akitoa elimu ya kodi wakati wa semina ya
wafanyabishara wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu iliyofanyika mjini Nyashimo.
Meneja wa Elimu kwa
Mlipakodi kutoka mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Diana Masalla akiwafundisha
wafanyabishara wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu tofauti iliyopo kati ya
mfanyabishara anayetunza kumbukumbu na asiyetunza kumbukumbu katika semina ya
wafanyabishara hao iliyofanyika mjini nyashimo.
Mfanyabishara wa duka
katika Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu Paulina Hinda akichangia hoja wakati wa
semina ya wafanyabishara ambayo imeandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
na kufanyika Mjini Nyashimo Wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...