Mratibu wa Mbio za Rock City Marathon, Bw. Kasara Naftal akionyesha medali ambayo washiriki wote watakaomaliza mbio hizo watapatiwa.
  Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano ya mbio za Rock City Marathon, Bw. Samwel Gisayi (Wa pili kushoto) akizungumzia usajili wa washiriki wa mbio hizo, mapema leo katika mkutano na waandishi wa Habari.
Muwakilishi wa washiriki wa mbio za Rock City Marathon, Bw. Frank R. Mtweve akionyesha medali tofauti watakazopatiwa washindi wa mbio hizo.


Ikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya kufanyika kwa mbio za Rock City Marathon jijini Mwanza, wadau mbalimbali wanaotarajia kushiriki katika mbio hizo wameonyesha kufurahishwa na zawadi zitakazotolewa kwa washindi na washiriki ikiwemo medali na fedha taslimu zaidi ya Sh Mil 30.

Mbio hizo zilizojinyakulia umaarufu mkubwa ndani na nje ya nchi zinatarajiwa kufanyika Octoba 20 mwaka huu kwenye Viunga vya Jengo la Biashara la Rock City Mall huku wadau mbalimbali wakiwemo viongozi waandamizi serikalini akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella wakitarajia kushiriki katika mbio hizo. 

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mratibu wa mbio hizo kutoka kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Kasara Naftal amesema pamoja na medali washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 4 kila mmoja, sh.mil 2/- kwa washindi wa pili na sh. Mil 1/- kwa washindi wa tatu, huku washindi wanne hadi kumi na tano nao pia wakiibuka na zawadi za medali na pesa taslimu. 

Kwa upande wa mbio za Kilomita 21, Bw Kasara alisema pamoja na medali washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia sh. Mil 2/- kila mmoja, sh. Mil 1/- kwa washindi wa pili na sh. Laki 7/- kwa washindi wa tatu huku pia washindi wanne hadi wa kumi na tano wakiibuka na zawadi za pesa taslimu na medali kila mmoja. 

“Kuhusu mbio za kilomita tano ambazo zitahusisha washiriki kutoka mashirika na taasisi mbalimbali (corporates) tunatarajia kwamba zitaongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dk Philis Nyimbi sambamba na washiriki wenye ulemavu wa ngozi yaani albino ambapo zawadi za fedha taslimu zitatolewa kwa washindi watatu wenye ualbino pekee.” Alisema. 

Bw Kasara aliongeza kuwa kwa washindi wa mbio za kilomita mbili na nusu zitakazohusisha watoto wenye umri kati ya miaka 7 hadi 10 watapatiwa fedha taslimu. 

Mbio hizo zilizoanzishwa miaka kumi iliyopita zinatarajiwa kupambwa naburudani mbalimbali ikiwemo ngoma za asili sambamba na maonesho ya waadau mbalimbali wakiwemo wadhamini wa mbio hizo ambao ni pamoja na kampuni za TIPER, Pepsi, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). 

Wadhamini wengine ni pamoja na kampuni ya uwakili ya Lis Law Chambers & Consultants, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), CF Hospital, Metro FM, Mwanza Water, Pigeon Hotel, Cask Bar, Kampuni ya Usafi ya SDN na Kampuni ya Ulinzi ya Garda World. 

Akizungumzia usajili wa mbio hizo Bw. Samwel Gisayi kutoka idara ya mahusiano ya mbio hizo alitoa wito kwa washiriki kuendelea kujisajili kupitia vituo na mawakala wa mbio hizo katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma, Pwani na Arusha 

‘’Kwasasa usajili wa mbio hizo unaendelea kupitia vituo mbalimbali katika mikoa ya Mwanza (Rock City Mall, Pasiansi Afro Twist Gym), Dodoma (Shabiby Bus Terminal), Dar es Salaam (Shamo Tower, Imalaseko Super Market (Posta), Heleana Fashion – Dar Free Market), Arusha pamoja na Bagamoyo mkoani Pwani.’’ 

“Pia usajili unaweza kufanyika kwa njia ya mtandao kupitia website yetu ya Rock City Marathon ambayo ni www.rockcitymarathon.co.tz’’ 

Naye muwakilishi wa washiriki Bw. Frank R. Mtweve alielezea kufurahishwa kwake na zawadi zinazotolewa na waandaaji wa Rock City Marathon. 

“Rock City Marathon ndio mbio pekee hapa nchini ambazo zinatoa zawadi kubwa kuliko na washiriki wake wote watakaomaliza mbio kupata medali. Na pia ndizo pekee ambazo zinashirikisha watu wenye ulemavu wa ngozi (Albinism).” Alisema 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...