Na: Kiyungi Moshy.Tabora.

Novemba, 2019

Asha Baraka ni mwanamke wa mfano wa kuingwa kwa ujasiri wa kuthubutu kufanya jambo, akafanikiwa.

Amejaaliwa kuwa na talanta lukuki ambazo kwa kauli yake anasema zingine bado hajazionesha.

Baadhi ya vipaji vyake hivyo vilianza kujitokeza akiwa katika shule ya sekondari ya Wasichana Tabora, alipokuwa katika mchezo mpira wa Pete na kikapu, iliyomfikisha kuchaguliwa timu ya shule.

Umahiri wake katika michezo hiyo, Asha alichaguliwa kuwa mmoja kati ya wanafunzi waliounda timu ya UMISETA mkoani Tabora.

Akiieleza historia ya maisha yake, Asha alisema kuwa alizaliwa katika kijiji cha Mwandiga, kilichopo katika Wilaya Kigoma Vijijini, Mkoani Kigoma.

Masomo yake ya msingi aliyapata katika shule mbili tofauti. Darasa la kwanza hadi la tatu alisoma katika shule ya msingi Kipampa iliyopo Ujiji, mjini Kigoma.

Baba yake Mzee Ramadhani Baraka alikuwa Daktari hivyo alihamishwa kwenda kufanya kazi katika hospitali nyingine ya Nguruka, mkoani humo.

Asha alilazimika kuandamana na wazazi wake kwenda Nguruka, akiwemo mama yake mzazi, maliyemtaja kwa jina maarufu la Mama Ali Baraka.

Alisoma katika shule ya msingi Nguruka darasa la nne hadi alipofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi.

Asha Baraka alikuwa ‘Kichwa’ kweli kweli darasani, alifaulu mtihani wa darasa la saba, akachaguliwa kwenda kusoma katika shule ya sekondari ya vipaji maalum ya Tabora Girls, iliyopo mjini Tabora.

Akiwa shuleni hapo alicheza mpira wa pete na kikapu hatimaye alichaguliwa kuwakilisha mkoa huo, akiwa katika timu ya mpira wa Pete.

Licha ya kucheza mchezo wa Pete na kikapu, Asha Baraka alikuwa mwanariadha mashuhuri akikimbia mbio za mita 100, na kuwa kati ya mwanamichezo bora shuleni hapo.

Alipomaliza masomo ya sekondari mwanzoni mwa miaka ya 1980, aliajirawa katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) la jijini Dar es Salaam katika Idara ya mauzo na masoko.

Asha ni mama mwenye familia ya mume na watoto wawili wa kiume. Aliwataja kwa majina kuwa ni Mope mwenye umri wa miaka 25 sasa, ambaye alisema amefuata nyayo zake za uhezaji wa mpira wa kikapu.

Aliwahi kuchaguliwa katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 18. Mwingine ni Imani mwenye umri wa miaka 20.

Asha licha ya majukumu yake ya kazi, pia alikuwa akijishughulisha na uongozi wa kundi la vijana waisopungua 45, katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’

Miaka ya nyuma kulikuwa na mipango mzuri ambapo baadhi ya mashirika ya umma yalikuwa na vikundi vya burudani za ngoma za asili, dansi na michezo.

Shirika la Bima la Taifa lilikuwa mojawapo ambalo lilikuwa na timu ya mpira wa pete halakadharika ilikuwa na bendi ya Bima Lee Orchestra.

Asha Baraka alicheza mpira wa pete na kikapu katika timu ya Bima, pia alichaguliwa katika timu ya wilaya hadi ya mkoa wa Dar es Salaam.

Kipaji kigine cha mama huyo ni kile cha kuchaguliwa katika timu ya ya taifa ya riadha. Enzi zake alikuwa akikimbia mbio za mita 100.

Wakiwa kambini mjini Arusha wakati huo, kulifanyika mchujo, naye akawa miongozi walioondolewa katika timu hiyo.

“ Siwezi kumshau Juma Ikangaa ambaye aliniletea viatu mahsusi kwa ajili ya kukimbilia (Sparks) toa Japan. Kabla ya hapo, nilikuwa ninakimbia nikiwa na viatu vya raba” alisema Asha Baraka.

Alitolea mfano wa mwanariadha wa zamani ambaye aliyepata mafanikio makubwa licha ya kutokuwa na zana, Mwinga Mwanjala.Mwanjala alishinda mashindano ya kitaifa ikikimbia bila viatu ‘Pekupeku’

Asha alibaisha kwamba hata kuchaguliwa kwake kukimbiza mwenge wa Olympic, haukufanyika kwa upendeleo, anasema yeye ni mwanariadha wa siku nyingi mwenye rekodi kitaifa.

Kama nilivyokueleza hapo awali kuwa Asha ana vipaji vingi mno, alionyesha maajabu baada ya kuendesha gari akiwa na umri mdogo wa miaka 14, wakati huo alikuwa kidato cha pili hapo Tabora Girls.

Alieleza kwamba hata alipoanza kazi Shirika la Bima, watu wengi wakiwemo wafanyakazi wenzake, walikuwa wakimshangaa kumuona binti mdogo wakati huo akiendesha ‘mkoko’ kuja kazini.

Mama Asha kupitia uzoefu wake wa muda mrefu wa kuendesha magari, aliwahi kupatwa na shauku ya kushindana katika mbio za magari hapa Tanzania.

Asha alikosa gari maalumu la mashindano hayo, licha ya kufanya mazoezi makali kupitia maeneo mbalimbali hadi Chalinze.

“Nilikuwa napenda sana kuendesha magari, nilifanya mazoezi ya kushindana nikapitia maeneo mengi hadi Chalinze. Anajisifu Asha Baraka.

Analisema kwamba Pamoja na kukosa gari, alijichomeka katika katika gari la wasindikizaji na kuweza kuzunguka toka mwanzo wa safari hadi mwisho wa mashindano hayo.

Ujasiri wa mama Asha ulionekana mwaka 2010, baada ya kuacha kazi yake nzuri katika Shirika la Bima la Taifa (NIC) na kuamua kujikita katika Biashara na Siasa.

Shirika la Bima la Taifa mwaka 2000, liliwataka waajiriwa wote kuomba kazi upya. Japo yeye alikuwa nje ya mji kikazi wakati huo, lakini aliporejea hakutaka kuendelea na kazi, hivyo akaamua kutoandika barua ya maombi ya kazi hatimaye akacha kazi rasmi 2010.

Asha baada ya kuacha kazi Shirika la Bima la Taifa (NIC) aliamua kujikita katika Biashara na Siasa.

Kwa upande Siasa, Asha Baraka hivi sasa ni mjume wa National Executive Committee (NEC) kupitia wilaya mpya ya Uvinza, iliyopo mkoani Kigoma.

Anajuvunia kuwa karibu na wanamuziki wake wa African Stars, wana ‘Twanga Pepeta’ kwa kuwa anapata muda wa kuzungumza na kuelewa matatizo yanayoikabiri bendi sanjari kujua mafanikio.

Historia inaeleza kwamba kabla ya kuwa kampuni African Stars Entertainment Tanzania (ASET), kulikuwa na bendi ya African Stars iliyoanza mnamo tarehe 01 July 1994, katika Hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

Baadaye bendi za M.K.Group, M.K. Beat na M.K. Sound zikaanzishwa na Alli Baraka, aliyekuwa mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Zambia (Zambia Airways).

Baadaye akawachia uongozi nduguze Msilwa Baraka, aliyekuwa Mwenyekiti na Asha Baraka akawa Mkurugenzi Mtendaji.

Kampuni ya African Stars Entertaiment Tanzania (ASET) iliyoasisiwa mwaka 2000 , Asha akawa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo.

Kufuatia juhudi za kuongoza kwa umakini mkubwa kundi la vijana wa kiumena kike pasipo kuteteleka, walimpachika jina bandia la ‘Iron Lady’

Alijinasibu kuwa ASET ni mithiri ya Chuo ambacho kinatengeneza vipaji kwa vijana, kisha kuwaruhusu kwenda popote wanapohitajika pasipo masharti.

“Tuna Academy ya kuendeleza vipaji vya vijana, inayoitwa Twanga Pepeta Academy.

Vijana hao walikuwa wakipewa nafasi ya kupiga muziki siku za Jumamosi pale Mango Garden, kabla haijavunjwa wakapiga muziki wao, baadaye bendi African Stars ‘Wana Twanga Pepeta’ kupanda jukwaani” Alisema Iron Lady.

Akiyaelezea mafanikio katika kampuni yake ya ASET, Asha alisema ni makubwa sana licha ya kuwa wana Academy, pia ina wanamuziki wa kuingia na kutoka wapatao 45.

Vilevile wamekwisha tunukiwa tuzo kibao zikiwemo za BBC, BASATA, ile Mascut huko Arabuni ambako kulifanyika festival.

ASET imekuwa mstari wa mbele kuisaidia jamii katika matatizo mbalimbali ya kijamii.

Mojawapo ni lile la Iron Lady Asha Baraka kuandaa onesho maalum la muziki ambalo pesa zilizopatika hapo, alizikabidhi kwa aliyekuwa mwanamuziki mkongwe Maalim Gurumo ambaye hali yake ya kiafya ilikuwa tete, kabla ya kifo chake.

Mwaka 2000 wakati wa shindano la Tanzania Musical Awards, The African Stars Band, ilifanikiwa kuwa bora ya mwaka kwa mwaka 2000/2002. Wimbo wa Kisa cha Mpemba ukawa ndiyo mwibo bora namba mbili.

Asha Baraka ni mmoja wa viongozi wa klabu ya Simba yenye makao yake makuu Msimbazi jiijini Dar es Salaam. 

‘Iron Lady’ Asha Baraka mwaka 2019 aling’atuka akamkabidhi Luiza Mbutu wadhifa wa kuongoza bendi African Stars ‘Twanga Pepeta, baada ya Asha Baraka ‘Iron Lady’ kung’atuka.

Kabla ya kupewa nafasi hiyo, Mbutu alikuwa Katibu wa bendi ambaye amedumu katika bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ kwa zaidi ya miaka 20.


Kila la heri Iron Lady Asha Baraka.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...