NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru. Bashiru Ally Kakurwa,ameishauri Serikali kuhakikisha inachunguza vyanzo vya fedha za Vyama Vya Siasa vyote nchini zitakazotumika katika uchaguzi mkuu ujao kama zinatokana na vyanzo halali vya fedha za vyama hivyo.

Alisema kuna vyama havina wanachama wala mradi ya kuwaingizia kipato lakini wakati wa uchaguzi vinatumia fedha nyingi bila ya kujulikana vyanzo vya upatikanaji wa fedha hizo.

Ushauri huo aliutoa katika mwendelezo wa ziara yake zanzibar katika Mkoa wa Kusini Kichama wakati akizungumza na Viongozi wa ngazi mbali mbali za CCM Mkoani humo.

Dkt.Bashiru,alisema Serikali ihakikishe Vyama vyote vya Siasa ikiwemo CCM vinatumia vyanzo halali vya fedha za uchaguzi mkuu ujao ili kuepuka matumizi ya fedha kutoka vyanzo haramu.

Alisema CCM inajipanga kutekeleza kwa vitendo sheria ya gharama za Uchaguzi kwa kuhakikisha inatumia fedha zake za ndani zilizotokana
na vyanzo halali vya fedha za ndani ya chama hicho.

Alieleza kuwa kuna baadhi ya vyama vya Siasa vimevikuwa na tabia zisizofaa za kupita kila kona wakiomba fedha za kufanya uchaguzi kutoka katika vyanzo haramu kwa lengo la kushindana na CCM.

"Chama Cha Mapinduzi kina wanachama wengi wanaolipa ada hivyo tunao uwezo wa kuendesha uchaguzi bila kutegemea fedha za misaada.

Lazima na vyama vya upinzani viweke wazi vyanzo vyao vya mapato kama tunavyofanya sisi bila kufanya hivyo tutakuwa na mashaka na upatikanaji wa fedha zao katika uchaguzi. "alisema Dkt.Bashiru.

Katika maelezo yake Dkt.Bashiru,alizielekeza kamati za siasa za Mikoa yote ya CCM Tanzania kuanza maandalizi ya kukusanya fedha za uchaguzi kutoka katika vyanzo vya fedha vinavyotambulika kutoka katika mikoa hiyo kwa ajili ya uchaguzi.

Aliwambia viongozi hao wa mikoa kuwa uchaguzi mkuu ujao CCM Makao Makuu haitotoa fedha za uchaguzi kila mkoa utajigharamia na CCM utakuwa na kazi kubwa ya kuratibu uchaguzi ufanyike kwa ufanisi.

Aliongeza kuwa mwaka 2020 CCM kwa mara ya kwanza itafanya uchaguzi wa gharama nafuu kwani hata katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka huu walitumia fedha zisizozidi shilingi Milioni 300 badala ya bilioni 8 zilizokuwa katika bajeti ya awali.

Katibu Mkuu huyo Dkt.Bashiru,akizungumza katika ziara hiyo alizitaka Kamati za Siasa za Mikoa zinazoandaa mapendekezo ya uteuzi wa wagombea Udiwani kuwasilisha katika Halmashauri za mikoa kwa ajili ya uteuzi wa wagombea katika kura za maoni kuepuka hilba na upendeleo kwa kuandaa mapendekezo ya wagombea wenye sifa na wanaokubalika kwa Wananchi.

Pia hata kwa Wabunge na Wawakilishi utaratibu wa kupatikana wagombea wa kupeperusha bendera ya CCM watapita katika mchujo na kuthiminiwa kwa kina ili wapatikane viongozi wenye sifa na uwezo unaokubalika kikatiba na wanaokwenda na kasi ya sasa CCM Mpya.

"Uchaguzi ujao ushindi wa kura za maoni hautokuwa kigezo cha kuwa kiongozi lazima tujiridhishe kwa sifa za kila mgombea kwa kuangalia rekodi yake kiutendaji na uchapakazi wake ndani na nje ya Chama",alisisitiza Dkt.Bashiru.

Kupitia Kikao hicho aliwapingeza Wabunge,Wawakilishi na Madiwani walioanza kujenga majengo ya chama na kununua vifaa mbali mbali kwa ajili ya chama kwani kufanya hivyo ni kuweka alama za kudumu za uongozi katika maeneo yao.

Sambamba na hayo Dkt.Bashiru, aliahidi kuwa CCM kwa kushirikiana na Serikali wataendelea kuandaa mazingira rafiki ya kuwaunganisha Vijana bila ya kujali tofauti zao za kisiasa kupitia sekta za michezo na sanaa ili waepuke dhambi ya kubaguana.

Aliwataka viongozi wa CCM kuwekeza kwa vijana kwa kuhakikisha wanawapatia malezi na makuzi bora ya kuwaeleza historia halisi ya Mapinduzi,Muungano na Uhuru wa Tanzania sambamba harakati za kujikomboa kutoka katika mikono ya ukoloni na usultani ili wapate ujasiri wa kulinda nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...