Na Leandra Gabriel, Michuzi TV
CHANGAMOTO ya kutoa na kudai/kutoa risiti mara baada ya kununua au kuuza bidhaa imeelezwa kuendelea katika baadhi ya maeneo huku ikishauriwa elimu zaidi kuhusiana na umuhimu wa elimu ya Kodi kuendelea kutolewa  kwa wananchi kote nchini ili kuwawezesha kutambua umuhimu wa kulipa Kodi hiyo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 12 ya Chuo Cha Kodi (ITA) Naibu Gavana wa Benki kuu Julian Raphael  Banzi amesema bado Kuna uhitaji wa kutoa elimu ya kodi kwa kwa wananchi na chuo hicho kina wajibu na kushirikiana na Mamlaka ya Mapato nchini ( TRA) katika kuhakikisha  wanawashawishi na kuwaelimisha wananchi kuhusiana na umuhimu wa kulipa Kodi.

Aidha amesema kuwa Serikali inatekeleza mpango wa miaka mitano 2016/2017 na 2020/2021 wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo ya watu na utekelezaji huo unaenda sambamba  na uthabiti na makusanyo ya kodi.

"Tunatambua kuwa Chuo Cha Kodi kina fursa ya kipekee nchini na hasa kwa kutoa mafunzo ya forodha na Kodi yenye uhalisia wa kiutendaji hivyo basi, Chuo hiki kina wajibu wa kuhakikisha kwamba kinatoa wataalamu walio mahiri katika masuala ya forodha na Kodi ili kuisaidia Serikali kutekeleza vipaumbele vya bajeti na hatimaye kufanikisha dhima ya kujenga uchumi wa viwanda" ameeleza.

Pia amewashauri wataalamu wa Chuo hicho kuendelea kujiimarisha zaidi katika utafiti wa masuala mbalimbali ya Kodi hasa katika sekta maalumu na zinazoibuka ikiwemo gesi, mafuta, kilimo na madini ili kuweza kuongeza makusanyo yatakayosaidia pia kuimarisha miundombinu ya Chuo hicho.

Kwa upande wake Kamishina wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Dkt.Edwin Mhede amewashauri wafanyakazi wa taasisi za umma na binafsi kufanya kazi kwa bidii na kuepukana na rushwa Jambo ambalo limekuwa likikwamisha shughuli nyingi za maendeleo na amekipongeza Chuo hicho kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi ili kuwajengea uwezo zaidi kiutendaji.

Mhede amesema kuwa Serikali kupitia TRA wataendelea kushirikiana na chuo hicho ili kiweze kuendelea kuwa kitovu Cha Kodi katika ukanda wa Afrika Mashariki na amewashauri wahitimu hao kutumia maarifa waliyoyapata katika kuleta tija kwa jamii na taifa me ujumla pamoja kuwa mabalozi bora wa kutoa elimu ya kodi popote watakapokwenda.

Mkuu wa Chuo hicho Profesa. Isaya Jairo amesema wanafunzi wapatao 417 wamehitimu  na kutunukiwa shahada mbalimbali katika ngazi  ya cheti, astashahada na shahada mbalimbali na kusema kuwa wameendelea kukarabati miundombinu kwa kutumia Fedha za ndani na ameishukuru Serikali kupitia  TRA kwa kuendelea kuhakikisha kila mipango ya kutoa wamahiri bora  inakamilika.

Amesema kuwa katika miaka 12 ya Chuo hicho wanajivunia zaidi katika utoaji wa mafunzo ya forodha na Kodi wakiwa ni  Chuo pekee nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini licha ya kuwa na changamoto ya rasilimali fedha.

Prof. Jairo amewashauri wahitimu kutumia mafunzo waliyoyapata kuleta tija kwa Jamii na kuwa wazalendo katika kulitumikia  taifa hasa kwa wakati huu ambao nchi imejikita katika kujenga uchumi wa kati na viwanda.
 Kamishina wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) Dkt. Edwin Mhede akizungumza katika mahafali ya kumi na mbili ya Chuo Cha Kodi (ITA) ambapo alieleza kuwa Serikali kupitia Mamlaka hiyo itaendelea kufanya kushirikiana na chuo hicho ili kuweza kutoa wataalamu mahiri wenye kuleta matokeo chanya kwa jamii, leo jijini Dar es Salaam.
 Wahitimu wa Astashahada ya uzamili ya masuala ya Kodi wakivaa kofia baada ya kutunukiwa shahada hiyo na Naibu Gavana wa benki kuu Julian Raphael Banzi ambaye aliwashauri kutumia maarifa waliyoyapata katika kuleta mabadiliko katika jamii na kuwa mabalozi bora, leo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya wahitimu wa shahada mbalimbali waliohudhurishwa katika mahafali ya kumi na mbili ya Chuo hicho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...